George Masatu: Mkoba wa Simba uliosaka mkwanja kibabe, ukaishia kuishi kwa mateso

Monday May 13 2019

 

By MWANAHIBA RICHARD

Nyuma ya usukani, kwenye siti ya dereva wa gari la mizigo amekaa baba mtu mzima flani hivi.

Anajiandaa kupiga tripu za maeneo mbalimbali ya jiji lililojaa misongamano ya magari la Dar es Salaam kwa ajili ya kusambaza bidhaa kwenye maduka.

Ukimuangalia usoni utaona tabasamu kidogo. Ni tabasamu la kiungwana tu, lakini ni la kulazimisha kutoka kwa mtu aliyesongwa na mawazo mengi huku akijaribu kuficha ukweli. Ukweli unaouma na hakika unaomtesa kwelikweli. Ni ukweli unaomsumbua, George Magere Masatu, kwa sababu alikuwa bonge la supastaa wa soka nchini akikipiga klabu ya Simba hadi timu ya taifa, Taifa Stars. Yaani ni bonge la staa.

Na alicheza hadi soka la kulipwa kwa miaka saba nchini Indonesia ambako alikuwa akilipwa dola 5,000 (Sh. 11 milioni) kwa mwezi.

Kwa kipato hicho ungeratajia kumuona Masatu akila matunda ya uwekezaji uzeeni, lakini mambo ni tofauti kabisa. Anasota.

Anaishi kwenye chumba cha kupanga. Analazimika kuamka mapema asubuhi kwenda katika ajira yake ya kuusaka mkate wa kila siku akiwa dereva wa gari la kusambaza bidhaa. Anafanya kazi katika kampuni ya mfadhili wa zamani wa klabu yake ya zamani ya Simba, Azim Dewji, ambaye anamuona kama mwokozi wa maisha yake.

Nini kilimsibu beki tano huyo wa kihistoria nchini hadi kutaka kujiua na hatimaye kuishia kuwa dereva wa gari la mizigo jijini Dar es Salaam?

Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Masatu, anafunguka kila kitu kuanzia safari yake ya Indonesia na jinsi alivyoingia kwenye ajira yake ya sasa.

SAFARI YA INDONESIA

Kwanza kabisa anaanza kusimulia jinsi alivyoondoka nchini kwenda kucheza soka la kulipwa Indonesia.

“Wakati huo walikuwa hawaruhusu sana wachezaji kutoka nje, vikwazo vilikuwa vingi, mimi nilikuwa na rafiki yangu aliitwa Ally Shaha alizichezea timu za Sigara na Prisons, yeye tayari alikuwa amepata dili huko.

“Sasa aliponisaidia kupata timu, kazi ilibaki kwangu, naondokaje sina hata kibali? Nakumbuka tulikuwa tunakwenda kucheza dhidi ya Kagera Sugar, niliona huo ndiyo wakati pekee wa kuchomoka. Kwa vile tulikuwa tunaenda Kanda ya Ziwa niliwadanganya viongozi wangu wa Simba kuwa nauguliwa na baba yangu mzazi.

“Niliomba ruhusa ili nitangulie kumwona mzee halafu nitaungana nao huko huko, nilikubaliwa hiyo ruhusa, niliyemuaga na kumwambia ukweli kwenye timu alikuwa Madaraka Selemani tu na tulikuwa kambini wakati huo.

“Nilichokifanya ni kupanda basi moja kwa moja hadi nchini Kenya maana ningesema nipande ndege hapa Dar es Salaam ingegundulika kuwa nasafiri nje ya nchi, hivyo nilikwenda kupandia ndege jijini Nairobi. Nilipofika Indonesia nilipokewa vizuri na wenyeji wangu.

ALIFOJI KIBALI

“Sasa baada ya kufika kule tatizo likawa kwenye kibali cha uhamisho (ITC) kutoka kwenye shirikisho langu la soka (TFF), maana niliondoka nchini bila kufuata utaratibu na wakati huo TFF pale alikuwapo Ismail Aden Rage ambaye ni mtu wa Simba, lazima angezuia kama angejua mpango huo mapema.

“Kilichofanyika, nilitumia kibali cha Shaha kwa maana ya kwamba tulifoji. Shaha alikuwa na kibali, hivyo tulifuta sehemu yenye jina lake kuandika jina langu halafu tulimtumia mtu, ambaye yupo hapa Tanzania (jina alilihifadhi).

“Haikufika TFF, maana kule walikuwa wanataka waipokee ITC kwa email, hivyo huyo mtu akawatumia shirikisho la Indonesia kwa njia hiyo ili ionekane imetumwa kutoka TFF, waliipokea na mimi nilianza kazi sasa ya kucheza.

“Ningepaswa kulipia hicho kibali dola 2,000 pale TFF, lakini kutokana na vikwazo nilivyovihofia na ukizingatia nilitoroka ndiyo maana nililazimika kumpa dola 500 mtu tuliyemtumia huku kwa ajili ya kuwatumia watu wa Shirikisho la Soka Indonesia, hiyo pesa ilikuwa kama ahsante yangu tu,” anasema.

ACHEZA KIMAZABE

Nchi kadhaa ulimwenguni ambazo zinafuatilia zaidi masuala ya kodi ni lazima hata wachezaji walipe kodi kulingana na kipato chao cha mshahara, lakini kwa Masatu haikuwa hivyo.

“Nilicheza miaka saba nchini humo katika timu tofauti, Peres Raja, Cgre, Peresija Bandaache zote za Daraja la Pili bila kulipa kodi na nilikuwa nalipwa mshahara wa dola 5,000 (Sh. 11 milioni) kwa mwezi, nilicheza miaka mitatu bila kibali cha kazi, ni nchi ambayo wanaishi kimafia fulani hivi, hivyo wenye timu wanazungumza na watu wa uhamiaji maisha yanaendelea freshi tu.

“Katika kipindi chote hicho cha miaka saba niliwahi kuja nchini mara moja tu, sikuja mara kwa mara kutokana na jinsi nilivyoondoka na maisha ya kule,” anasema Masatu.

PESA ZIKO WAPI

Mambo ndani ya familia yake yalikuwa mazuri wakati Masatu anaondoka nchini kwenda Indonesia, akimuacha hapa mkewe na binti yao mmoja. “Unajua kule sikuwa na familia, nilimwacha mke na mtoto hapa, hivyo kiasi kikubwa cha mshahara wangu nilimtumia mke wangu ili kuendesha maisha ya kawaida ya familia pamoja na mambo mengine kama ujenzi wa nyumba yetu.

“Lakini, hata wakati naondoka hapa nilimwachia miradi mingine kama saluni ya nywele, magari mawili aina ya Toyota Hiace na duka la vinywaji (grocery). Hivi vitu nilivipata nikiwa nacheza soka hapa, hivyo pesa niliyotuma ilisaidia kuendeleza biashara yetu, nilimwamini sana mke wangu.

“Mara nyingi hizo pesa nilikuwa nazituma kupitia kwa Idd Pazi maana ndiyo ilikuwa rahisi kumfikishia,” anasema huku akidai hakuwa na shaka yoyote juu ya matumizi ya pesa hizo.

Anasema baada ya kukaa huko kwa miaka saba aliamua kurejea nyumbani na hiyo ni baada ya kuamua mwenyewe.

“Sikulazimishwa na mtu kuacha kucheza soka nchini humo, yalikuwa maamuzi yangu kwani nafasi ya kucheza ilikuwapo ila sikutaka kuendelea maana hata vibali vyenyewe sikuwa navyo kabisa.

“Nilikuwa naogopa kurudi na pesa nchini kwamba niitunze mwenyewe kwani ningefuatiliwa ukizingatia sikuondoka vizuri, ndiyo maana nilikuwa natuma tu pesa nyumbani.

“Hapo ndipo lilipoanza timbwili la kuharibika kwa maisha yangu. Nikiwa huko nilikuwa nawasiliana vizuri tu na mke wangu hata taarifa ya kurejea nilimweleza, lakini baadaye hali ikawa tofauti baada ya kufika hapa.”

ATUA USIKU MNENE

“Ilikuwa bahati mbaya siku ambayo nilitakiwa kurudi nchini, safari iliahirishwa ilibidi nije siku iliyofuata, hivyo mke wangu alijua kuwa nimeahirisha, baadaye wakati nataka kufanya naye mawasiliano hakupatikana hewani hadi nafika Dar usiku wa saa saba sikuelewa nafikia wapi maana tayari jiji lilikuwa limebadilika na nilitarajia kuikuta familia yangu ikinisubiri uwanja wa ndege.

“Ilibidi niwasiliane na rafiki yangu alikuwa anakaa Tandika, aliniambia niende kwake kama mke wangu hapatikani hewani, bahati nzuri dereva taxi niliyemchukuwa walikuwa wanafahamiana na huyo rafiki yangu hivyo ikawa safari rahisi, muda wote huo simu ya mke wangu ilikuwa haipatikani, nilichanganyikiwa sana.

“Nilipofika kwa rafiki yangu, ambaye pia alikuwa anafahamiana na mke wangu alimpigia simu kwa kutumia namba nyingine kumbe alikuwa na namba mbili, alimpata hewani ila alipomweleza kuwa nipo pale kwake alishituka na kukata simu. Hapo hapo akili ilianza kuhisi kuna jambo baya linaendelea juu ya mke wangu, hata yeye nahisi alichanganyikiwa maana hakutarajia kama ningerudi siku hiyo hadi niwasiliane naye, alichukizwa pia na kitendo cha kupokewa na rafiki zangu.

“Na wakati wote huo kumbe alikuwa amehamia Mbeya bila ya kunitaarifu na alitaka nimfuate huko. Sikuwa tayari kufanya hivyo bila kuambiwa sababu za yeye kuhamia Mbeya. Wakati wote huo nilikuwa naishi hapa kwa kubebwa na rafiki zangu tu, kuanza maisha mapya ni ngumu sana. “Ni hali ambayo ilinitesa sana na kila muda nilijiuliza nini kimetokea mbona hawa jamaa zangu wote ni kama wanaelewa kinachoendelea ila wanaishi na mimi kwa kuniliwaza na kunificha?. “Baadaye mke wangu akaanza kudai talaka. Nikapima, nikaona huo ni mtihani mkubwa,” anasema.

KUHUSU MALI ZAO

Masatu anasema mali zao zilileta mgongano mkubwa hasa nyumba kwani ilijengwa kwenye kiwanja ambacho walipewa zawadi na mama mkwe pia nyumba iliandikwa jina la mke wake.

“Sijapata mali yoyote, kiukweli ilileta shida sana suala hili hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi, ingawa nyumba tulijenga kwenye kiwanja tulichopewa kama zawadi na mama yake.”

Unafahamu kilichompata baada ya mgogoro huo wa mali, unajua kwamba Masatu alitaka kujitoa uhai wake kwa sababu ya majanga na je nini kimeendelea kuhusiana na mali zake. Ilikuwaje akakutana na kupewa kazi na Azim Dewji? Fuatilia ndani ya Mwanaspoti kesho Jumanne.

“Hicho kiwanja, kwanza mama mkwe alitaka kutapeliwa sasa aliponieleza wakati huo nacheza Simba nilikwenda moja kwa moja kwa bosi mmoja wa Wizara ya Ardhi, wakaenda kukagua eneo na kubaini kwamba, kweli anataka kudhulumiwa, hivyo walikiokoa kiwanja hicho.

“Mama mkwe alifurahi nimemsaidia hivyo aliona atupe kama zawadi, lakini ndiyo hivyo mwenzangu aliamua kufanya maamuzi yake.”

ATAKA KUJIUA

Anasema kitendo cha mkewe kudai talaka kilimfanya aingiwe na hofu kwamba pengine mkewe amepata mtu mwingine hivyo anataka kuwa huru, jambo ambalo lilimzidishia ‘stress’.

“Yaliponitokea hayo nilikuwa sioni sababu ya kuendelea kuishi kwa kweli sikufikiria mbali kabisa niliona ni bora nife tu, niliona kifo ndiyo suluhisho, sikujali familia yangu wala watoto, kiukweli nilichanganyikiwa sana sikuwa na mwanzo wowote wa maisha, maisha yangu yaliharibika ghafla, hadi nikitembea ama kukaa nilijikuta nazungumza peke yangu.

“Yeye alikuwa anataka nitoe talaka jambo ambalo sikuwa tayari kulifanya, mimi niliamua kumuoa, yeye anadai talaka, nikamwambia basi atoe yeye hiyo talaka kama inawezekana. Matokeo yake hivi sasa kila mtu anaishi kivyake, talaka haijatoka.

TIPPO AMUOKOA

Wakati amekata tamaa ya maisha na kujiona hafai kabisa kuendelea kuishi huku rafiki zake wakiwa bega kwa bega kumsaidia, mfanyabiasha maarufu nchini Tippo alichangia kumuweka sawa Masatu.

“Achana na rafiki zangu wengine walionibeba wakati nipo kwenye kipindi kigumu, lakini Athuman Tippo alinisaidia sana, kila muda alitaka niwe pamoja naye maana alijua naweza kufanya maamuzi gani. Mambo mengi Tippo aliyafanya kwa ajili yangu ili mradi tu nikae sawa, kiukweli namshukuru sana pamoja na rafiki zangu wote waliokuwa nami bega kwa bega wakati huo nimekata tamaa, sina hali yoyote.”

AZIM DEWJI AMPA DILI

“Kuna siku nilikuwa napitapita zangu Posta kule, niliingia kwenye mgahawa mmoja ndipo nilionana na mfadhili wangu wa zamani Azim Dewji, alistuka kuniona, aliniuliza nafanya shughuli gani nikamweleza sina kazi yoyote, akanihoji maswali mengi na kunitaka niende ofisini kwake akanipe kazi.

“Kweli siku niliyoambiwa niende nilienda na siku hiyo hiyo nilikabidhiwa gari ambapo aliniambia nichague gari lolote la kuendesha kama ni kwenda mikoani ama hapa hapa, nami nilichagua hapa, magari makubwa nilikataa.

“Hivyo kuanzia hapo maisha yangu sasa yalianza kubadilika kwani napata mshahara na ninaweza kuendesha maisha mwenyewe.

“Kupitia ajira hii nimeweza kununua viwanja huko Kigamboni (anatoa hati za viwanja hivyo) ambavyo ni kwa ajili ya wanangu maana mimi sina mpango wa kujenga kwasasa, nitaishi kwenye nyumba za kupanga maana sina familia, wanangu ndiyo wanapaswa kutengeneza familia zao,” anafafanua Masatu.

Dewji ambaye alikuwa mfadhili wa Simba miaka ya nyuma amekuwa bega kwa bega na mchezaji huyo kwani hata alipoumia mguu akiwa na timu ya taifa alichukua jukumu ya kumtibu kwa gharama kubwa.

Dewji aliamua kuchukua jukumu hilo baada ya Masatu kusikia maumivu makali huku ndugu zake wakitaka kumpeleka kwa mganga wa kienyeji visiwa vya Ukerewe, lakini haraka alitumiwa tiketi ya ndege ili aje kutibiwa Muhimbili na safari ya kwa mganga iliishia hapo.

“Unajua Azim Dewji amekuwa na msaada mkubwa katika maisha yangu, nakumbuka wakati huo nilipoumia mguu alitoa pesa yake kunitibu, niliumia nikiwa timu ya Taifa, majeraha ambayo yalimfanya asuse kuitumikia timu hiyo kwani sikupata msaada ingawa baadaye Dewji aliniomba nirejee kikosini Stars.

Usikose sehemu ya pili kesho Jumanne uone Masatu akifunguka kuhusu ushirikina klabuni Simba.