Mikel Arteta apona corona

MMOJA kati ya watu maarufu katika medani ya soka kupata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona alikuwa ni kocha wa klabu ya Arsenal, Mikel Arteta inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL).

Arteta alikuwa ni mmoja wa kati ya watu wa kwanza kupata maambukizi hayo, sasa amethibitika kupona ugonjwa huo ambao tayari umeshaambukiza watu 300,000 duniani.

Ugonjwa wa Corona unasababishwa na virusi vya Corona vinavyoshambulia mfumo wa hewa na kusababisha homa ya mapafu kitabibu unajulikana kama COVID 19.

Kisa cha kwanza duniani kiliripotiwa Desemba 31, 2019 jijini Wuhan, China wakati hapa nchini kisa cha kwanza kilithibitishwa Machi 16, 2020 mjini Kilimanjaro.

Kocha huyo aliyepata maambukizi baada ya kuchangamana na bosi wa Olympiacos ambaye alikuwa na maambukizi ya virusi vya Corona alitengwa kwa muda wa siku 14 na huku pia wachezaji wote wa Arsenal nao walitengwa.

Inaelezwa kuwa tangu kuchangamana na bosi huyo Arteta alianza kujisikia vibaya akiwa na dalili za homa, mafua, kikohozi na uchovu na baada ya siku tatu hadi nne alianza kupata ahueni kidogo.

Arteta aliyaeleza haya wakati akihojiwa na kituo cha luninga cha Kihispania cha La Sextra na aliwaambia kuwa sasa anajihisi amepona ugonjwa huu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) kati ya watu 100 wenye maambukizi ya Corona, 80 hupona wenyewe bila matibabu yoyote.

Hivyo hata Arteta anaingia katika kundi la wale ambao wamepata maambukizi ya Corona na kupona mwenyewe kwa uwezo na uimara wa kinga yake ya mwili.

Kwa mujibu wa WHO mpaka sasa Corona haina tiba wala kinga ila matibabu saidizi hutolewa kumpa nafuu mgonjwa na hutengwa ili asiambukize wengine na huwa katika uangalizi maalum.

Je, hatua gani zilifanywa na klabu ya Arsenal?

Moja ya hatua muhimu za kudhibiti ugonjwa huu zilizofanywa na klabu ya Arsenal ilikuwa ni kumtenga kocha wake.

Hatua ya pili ilikuwa pia kuwatenga wachezaji wote ambao kwa namna moja ama nyingine walichangamana na kocha huyo.

Kocha huyo na wachezaji walitengwa kwa muda wa siku 14 kipindi ambacho endapo kitapita pasipo kuonyesha dalili zozote huwa ni ishara kuwa hawakupata maambukizi au aliyeumwa amepona.

Klabu hii ya kaskazini mwa London haikuishia hapo kwani walihakikisha wale wote wanaowahudumia wachezaji wanajikinga kwa kuvaa barakoa (mask) pamoja na mavazi maalum ya kitabibu.

Waliwawekwa chini ya uangalizi maalum wa jopo la madaktari wenye ujuzi wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ambao walisimamia pia utoaji wa elimu ya afya ya namna ya kujikinga.

Eneo la klabu hiyo lilipuliziwa dawa na vifaa vimewekwa kila kona kwa ajili ya unawaji wa mikono ikiwamo maji na sabuni ya mani pamoja kimiminika cha kitakasa mikono yaani sanitizer.

Programu zote za mazoezi za klabu hii zilisitishwa kabisa na walitarajia kuanza tena mazoezi baada ya siku hizi 14 kupita lakini pamoja na kuisha wameonelea si sahihi kwa sasa kuanza mazoezi kwani hali bado hali si shwari.

Wachezaji wafanye nini kulinda viwango vyao?

Kwa sasa ligi nyingi zimesimama kutokana na janga hili la kidunia na wachezaji wengi wameshauriwa kuwa ndani majumbani mwao hasa kwa wale ambao kuna visa vingi vya Corona.

Ikumbukwe kuwa kipindi hiki mchezaji anaweza kuwa katika hatari ya kushuka kiwango kutokana na kusimama kwa mazoezi ya jumla ya klabu.

Mchezaji mwenye kiwango ni yule mwenye kasi, nguvu na ustahimilivu. Vitu hivi anapaswa kuvilinda kwa kuzingatia mienendo na mitindo mizuri ya kimaisha.

Anatakiwa kipindi hiki kutojihusisha na ulevi, matumizi ya tumbaku na ulaji holela wa vyakula hasa vya mtaaani.

Akiwa kwake binafsi anatakiwa kufanya mazoezi rahisi ya kunyoosha viungo na kuimarisha misuli ya mwili kwa kufanya ubebaji wa vitu vizito vya wastani.

Mazoezi mepesi binafsi anayoweza kufanya kipindi hiki ambacho wameambiwa watulie ndani ni pamoja na kuruka kamba, ni zoezi rahisi lisilohitaji eneo kubwa.

Zoezi hili litakuwa na tija endapo tu litafanywa kwa muda wa dakika 30-60. Zoezi hili lina msaada mkubwa katika kulinda uzito wa mwili wa mchezaji.

Umakini unahitaji kwa mchezaji kuhakikisha kuwa anazingatia ratiba ya chakula aliyopangiwa na daktari au mtaalam lishe za wanamichezo.

Ulaji holela kipindi kama hiki inaweza kuchangia kupata uzito mkubwa hivyo kumweka katika hatari ya kuharibu kiwango chake.

Mchezaji kama mwananchi mwingine nao pia wanaweza kupata maambukizi ya Corona kama ilivyotokea kwa wachezaji wa italia na Uingereza ambao wameugua Corona hivyo anatakiwa kujikinga.

Njia za kujikinga

Osha mikono kila mara kwa maji safi yanayotiririka na sabuni au kwa kitakasa mkono (sanitizer) chenye kilevi dawa asilimia 60% na tumia angalau sekunde 30 kuosha mikono yako.

Epuka kugusa maeneo ya usoni

Tumia barakoa (mask) ikiwa unatoa huduma kwa visa vya Corona

Vaa barakoa kwa usahihi na usirudie kuitumia unapoisha muda wake

Epuka kukumbatiana, kugusana na kubusiana

Epuka kuwepo sehemu za misongamano isiyo na lazima.

Kaa umbali wa zaidi ya mita moja au futi sita kutoka kwa mgonjwa wa Corona au mwenye dalili za Corona

Zuia chafya au kikohozi kwa kutumia kitambaa safi au eneo la mbele la kiwiko.

Fuatilia taarifa zinazotolewa na wizara ya afya na Shirika la Afya Duniani.