Michael J Lema : Kinda la Bongo linavyopitia njia ya Obi

Muktasari:

  • Lema anasema mpango wake ni kulitumia taifa hilo kama daraja la kumvusha kwenda kwenye Ligi za mataifa makubwa kama vile Ujerumani, Ufaransa, Hispania na England.

NIGERIA ni miongoni mwa mataifa ambayo wachezaji wake wametapakaa kwenye kila kona ya dunia, jamaa wanajua kutafuta njia za kutoboa kwenye soka na kama unabisha vipi kuhusu yule, Abasalim Chidiebele.
Ndio! Namlenga yule aliyekuwa akiitumikia Coastal Union na baadaye akajiunga na Stand United kabla kutimkia zake Zambia.
Acha na huyo wapo wengine kibao ambao, walipigania nafasi za kutoboa kwenye mataifa yaliyoendelea nje ya Afrika na mwishowe wamekuwa mastaa wakubwa kwenye soka, akiwemo Mikel John Obi.
Kidogo Wabongo tumeanza kuchangamka kwa kuanza mmoja mmoja kwa kuonyesha uthubutu wa kutoka nchini kama ilivyo kwa Wanigeria ambao Wamejaa kuanzia Ulaya, Asia, Amerika ya Kusini, Amerika ya Kaskazini na hadi Australia.
Winga wa Kitanzania, Michael John Lema ni mmoja wa nyota wa Tanzania ambaye ameonyesha uthubutu kwa kupambana na hatimaye kupata pa kuanzia Austria.
Lema anasema mpango wake ni kulitumia taifa hilo kama daraja la kumvusha kwenda kwenye Ligi za mataifa makubwa kama vile Ujerumani, Ufaransa, Hispania na England.
“Bado sijaanza kuwa mchezaji wa kutegemewa kikosi cha kwanza, nina safari ndefu ya kuhakikisha nakubalika na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” anasema  
Lema ambaye ni mzaliwa wa Itigi, Singida anasema anashukuru Mungu maana amekuwa kwenye kiwango bora kwa kufunga mara kwa mara kwenye kikosi cha vijana cha SK Sturm Graz.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19, amefunga mabao 13 kwenye michezo 12 ya Ligi daraja la tatu, akiwa na kikosi B ambacho kinashiriki Ligi daraja la tatu ‘Regionalliga’ kama sehemu ya kuimarisha  wachezaji wa timu hiyo.
“Msimu huu nilipandishwa kikosi cha kwanza cha Sturm Graz lakini  sikuwa  napata nafasi ya kuchezwa kwa hiyo ilibidi kocha wa timu ya vijana aniombe ili niendelee kucheza kwa vijana.
“Ananikubali kwa hiyo aliona nikiwa kikosi cha kwanza kule bila ya kucheza kunaweza kuharibu kipaji changu, nilimwelewa na nikajisemea kuwa lazima nihakikishe nakuwa mfungaji bora ili nimvutie kocha wa kikosi cha kwanza,” anasema Lema.
Akizungumzia ishu za ubaguzi, Lema anasema zipo na amekuwa akikutana nazo na kinachomfanya wanyamaze mbele yake ni uwezo wake wa kufunga kila kukicha.
Mshambuliaji huyo, anasema kuna siku aliwahi kuonyeshwa ubaguzi wa wazi wazi kwenye mchezo wa Ligi huku akiwa jukwani na ugeni wa kaka yake, Erick ambaye alienda kumtembelea akitokea nyumbani Tanzania.
Lema anasema baada ya kuona mazingira hayo alifanya kweli kwa kufunga mabao matatu yani hat trick kwenye mchezo huo ambao ulikuwa Septemba 21 baina ya timu yao ya vijana dhidi ya Völkermarkt.
Baada ya kugunga mabao hayo, kile kikundi cha wahuni waliokuwa wakimwimbia maneno ya kibaguzi hakikusikika tena na badala yake alikuwa akisikia kelele na akaona uso wa kaka yake, ambaye alikuwa akimpigia makofi karibu na eneo la kuchezea.
“Etoo nakumbuka alitupiwa ndizi, alichokifanya nasikia aliimenya na kuamua kuila kwa hiyo nimejiandaa vya kutosha kukubaliana na mazingira ya namna hiyo,” anasema Lema.
Mshambuliaji huyo kinda wa Kitanzania ambaye alizaliwa Septemba 13, 1999 anasema alitua nchini humo kwa gia ya kusoma ambapo marafiki wa familia yao nchini humo walihitaji kumwendeleza.
Alipotua aliamua pia kujihusisha na soka na mwishowe kutupilia mbali masomo pale alipopewa mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa kwenye klabu ya Sturm Graz inayoshiriki Ligi Kuu Austria.