Mbio za ubingwa EPL na hofu ya Klopp

KOCHA wa Liverpool Jurgen Klopp amepatwa na kigugumizi baada ya kuulizwa vipi kuhusu beki wake Majeruhi Dejan Lovren kama atacheza mchezo wa ligi dhidi ya Manchester United Keshokutwa Jumapili.

Beki huyo wa kati ambaye amepata majeraha ya misuli ya paja na hakuwemo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Buyern Munich iliyopigwa siku ya Jumanne na kutoka suluhu. Kocha huyo alizingumza huku akisita sita na kuonekana kama mwenye hofu kwani kukosekana kwa beki wake huyo ni pigo katika mchezo huo muhimu wa EPL.

Klop aliwaeleza wanahabari kuwa Lovren hataenda Old Trafford kwa sababu bado majeraha yake hayajakaa sawa na ndiyo maana hakujumishwa katika mchezo wa uliochezwa jumanne. Kila mpenda soka anajua mechi ya keshokutwa ilivyo muhimu kwa Liverpool ambayo ina kiu ya kubeba kombe la ligi ambalo hawalijaligusa kwa zaidi ya miaka 20.

Haishangazi kukosekana kwa beki huyu wa kimataifa kutoka nchini Croatia kumpa hofu kocha wake, hii inatokana na ushirikiano pacha wa beki ya kati uliotengenezwa pamoja na beki mwingine Virgil van Dijk. Ukuta wa Livepool unakuwa imara zaidi wanaposimama pacha hawa, hivyo kukosekana kwa Lovren kunaweza kuwapa mwanya wa washambuliaji wa Man United kuipenya ngome hiyo kirahisi.

Pamoja na kutokufungwa katika mechi ya UEFA dhidi ya Buyern Munich bado ushirikiano wa beki Joe Matip ambaye ndiyo Mbadala wa Loveren haukuonekana kama ni imara zaidi.

Lovren alipata majeraha ya misuli ya nyuma ya paja dakika ya tano ya mchezo wa mechi ya FA dhidi ya Wolves mwanzoni mwa mwezi uliopita mchezo ambao walifungwa 2-1.

Majeraha haya ambayo kitabibu hujulikana kama Hamstring injury huwa yanahusisha majeraha ya Tendoni (kano) yalionyesha kama vile yameishapona.

Lakini siku ya jumatatu kabla ya mechi ya Buyern beki huyo wa alishindwa kufaulu majaribio ya mwisho ambavyo yalifanywa ili kujua kama yuko fiti kucheza mechi ya Jumanne. Ingawa wapo wanaodhani pengine kusema kuwa mchezaji huyo hata cheza siku ya jumapili ni moja ya mbinu ya kimchezo ya kisaikolojia lakini Kloop amepinga akisema kuwa anachokisema ni kweli kabisa.

Misuli ya Hamstring inahusisha kundi la misuli mikubwa mitatu ambayo iko nyuma ya paja ambayo mara nyingi wanasoka hupata mchaniko au michubuko au mvutiko wa Tendoni kupita kiwango. Misuli hii ni nyenzo kubwa kwa mwanasoka kwani anaitegemea kufanya mambo mengi uwanjani kwa kutumia mguu.

Je, nini kitajiri Lovren akicheza?

Ni kawaida mchezaji akiwa na muhimu na huku klabu inakabiliwa na mechi ngumu jopo la ufundi linaweza hata kumlainisha daktari amruhusu acheze hivyo hivyo. Mambo kama haya hayatokei katika soka la bongo pekee bali pia hata soka la ulaya hayo yanatokea.

Nikwel Lovren tangu aumie ameishapitisha takribani mwezi ambao kwa majeraha ya misuli ya nyuma ya paja ambayo ni ya kati huenda akawa amepona vinginevyo yawe makubwa.

Maumivu yanaweza yasiwepo katika misuli hiyo lakini ndani kwa ndani misuli inaweza isiwe na ustahimilivu wa kumudu mikikimiki ya uwanjani na hii ndiyo maana jumatatu alifeli majaribio ya kitabibu.

Kucheza kabla ya kupona jumla sio sahihi kiafya kwani kunaongeza hatari kujijeruhi upya, na ikitokea jeraha limetoneswa huchangia kuchelewa kupona. Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi hudhani kuwa maumivu yakupungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza bila ya kujua kuwa ndani kwa ndani bado kupona kamili. Hivyo inawezekana kabisa Lovren kupona na maumivu yamepungua au kuacha kabisa, akadhani kuwa anaweza kucheza mchezo wa keshokutwa wenye upinzani mkali.

Mara yingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo uwapo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.

Wataalamu wa tiba za afya za michezo huweza kugundua majeraha ambayo hayajapona vizuri kwa kuyatathimini madhara yake kiujumla na kutoa ushauri endapo kuna hatari ya kujijeruhi tena.

Wataalam wa afya walimbaini katika majaribio ya kitabibu kuwa Lovren hayuko fiti kucheza mechi ya Jumanne, hivyo kuleta picha kuwa bado majeraha yake hayajapona kwa asilimia 100. Viongozi na mashabiki wanakawaida ya kushinikiza wachezaji muhimu kuchezeshwa hata kama majeraha hayajapona vizuri. Ndiyo maana yapo matukio ya wachezaji aina ya Lovren kupewa matibabu ya sindano au vidonge maumivu ili kuwawezesha kucheza hata kama hawajapona.

Dawa hizo za huondoa maumivu na kumpa utulivu kwa muda tu na si kuponesha na kuimarisha misuli hiyo iliyojeruhiwa. Hata pale mchezaji majeruhi anapocheza katika hali hiyo hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa kwani tishu hizo zinapungua uimara.

Kwa majeraha ya misuli ya nyuma ya paja yanaweza kuchukua wiki 2-6 kupona na pia itategemeana yako daraja lipi la uanishaji. Haikuwekwa bayana kuhusu jeraha la Lovren lipo daraja lipi lakini kwa namna yoyote ile kucheza keshokutwa na akiwa hajapona vizuri uwezekano wakuongeza ukubwa wa jeraha ni mkubwa.