Mbabe wa FA anatoka hapa

UNAAMBIWA kwenye Michuano ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) utamu umenoga baada ya wanaume wanane kupenya hatua ya robo fainali huku watetezi Mtibwa Sugar wakiendeleza gundu la mabingwa wa michuano hiyo tangu ifufuliwe upya mwaka 2016.

Mtibwa imelitema taji mapema baada ya kung’olewa Raundi ya Tano na KMC kwa mikwaju ya penalti, ikifuata nyayo za Yanga ilipotemeshwa taji robo fainali mwaka 2017 na Simba iliyotia aibu kwa kulitema kombe raundi ya awali tena kwa timu ya Daraja la Pili (SDL).

Baada ya kupigwa mechi hizo za 16 Bora vidume vinane vimepenya zikiwamo Azam, Yanga, KMC, Alliance, Kagera Sugar, Lipuli na African Lyon na sasa wanasubiri kujua watavaana nani na nani kwenye droo ya hatua hiyo wiki ijayo kabla ya kuvaana mwishoni mwa Machi.

Timu zote zilizoingia hatua hiyo kama zitachanga vyema karata zake zinaweza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, lakini zipo ambazo kwa jicho la kawaida zimekuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya hivyo na nyingine hazipewi sana nafasi ya kutwaa taji japo lolote linaweza kutokea.

Makala haya yanakuletea tathmini juu ya nafasi kwa kila timu kati ya hizo nane, kutwaa ubingwa kulingana na ubora wa vikosi pamoja na ufanisi wa timu husika kwenye Ligi Kuu kwa mgawanyo wa alama chini ya kumi.

YANGA- 9/10

Msimu uliopita ilipoteza nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa na kuziachia Simba na Mtibwa, hii ni baada ya kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu na Kombe la ASFC.

Yanga inaonekana imejifunza kutokana na makosa, kwani imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mashindano hayo yote mawili ili irudi tena kwenye mashindano ya kimataifa.

Katika kundi la timu nane zilizotinga robo fainali, yenyewe ndio ina kikosi chenye wachezaji wanaoweza kupambania zaidi matokeo lakini pia ina jeuri ya kuwa na Kocha Mwinyi Zahera ambaye ni mtaalamu wa kuzisoma timu pinzani na kung’amua haraka mbinu za kukabiliana nazo.

Safari yake ilianzia kwa Tukuyu Stars iliyoifumua mabao 4-0 kisha Biashara United na kuimaliza Namungo juzikati kwa bao 1-0.

AZAM FC- 8/10

Imekuwa haifanyi vizuri kwenye Ligi Kuu ambako ni kama tayari imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa, hivyo ni wazi nguvu zake itazielekeza kwenye Mashindano ya ASFC ambako sasa inatakiwa ishinde mechi tatu tu ili iweze kuiwakilisha nchi msimu ujao kwenye mashindano ya kimataifa.

Silaha yake kubwa ni wachezaji wazoefu na wenye kiwango bora walionao kikosini lakini mabadiliko waliyofanya kwenye benchi la ufundi pia yanaweza kuwaongeza morali ya kufanya vizuri kwenye kombe hilo. Safari ya Azam FC ilianzia kwa kuzing’oa Madini, Pamba kisha Rhino Rangers.

KMC- 7/10

Imepanda daraja msimu huu lakini imekuwa ikileta ushindani kwenye Ligi Kuu na kwenye ASFC na kwa kuingia hatua ya robo fainali huku ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Ina Kocha Etienne Ndayiragije na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya mtoano kama Azam Sports Federation Cup, kama vile Emmanuel Mvuyekure, Yusuph Ndikumana, Juma Kaseja na George Sangija ambao wanaweza kuwa chachu kwao ya kushangaza watu.

Hii ilianza na Tanzania Prisons, kisha Pan Africans halafu ikaivua taji Mtibwa Sugar kwa matuta baada ya dakika 90 kumalizika kwa bao 1-1.

ALLIANCE FC- 7/10

Inaweza ikawa timu itakayoshangaza kwenye mashindano hayo (surprise package) kutokana na jinsi ilivyoimarika katika miezi ya hivi karibuni na ishara ya hilo ni mtiririko wa matokeo mazuri inayopata kwenye Ligi Kuu.

Ubora wa kikosi chake kinachoundwa na kundi kubwa la wachezaji wenye umri mdogo pamoja na mbinu za Kocha Malale Hamsini vinaweza kuibeba. Yenyewe iliing’oa Mufindi United, kisha La Familia ya Kilimanjaro ikainyoosha Dar City kwa mabao 3-0 juzi kati pale Nyamagana.

KAGERA SUGAR- 6/10

Imekuwa haifanyi vizuri kwenye ligi jambo linaloweza kuifanya nguvu zake izielekeze kwenye Mashindano ya Kombe la ASFC ambapo wanaweza kutwaa ubingwa iwapo ikipata ushindi kwenye mechi zake tatu tu.

Ina kundi kubwa la wachezaji wenye uzoefu ambao wamewahi kucheza mashindano ya kimataifa, hivyo hamu ya kuweka rekodi ya kushiriki kwenye mashindano hayo ikiwa na timu ya kawaida inaweza kuifanya ipambane zaidi.

LIPULI- 6/10

Ina wachezaji wazuri na washindani ambao wanachagizwa na Kocha Selemani Matola ambaye huwa hana hofu ya kukutana na timu kubwa na amekuwa akiiongoza timu hiyo kupata matokeo mbele ya timu hizo.

Hata hivyo, Lipuli haikupata changamoto kubwa hadi kufika hapo ilipo kwani imezitoa timu za madaraja ya chini tu jambo linaloweza kuifanya isijue udhaifu wake. iliitoa Laela ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, ikaitupa nje Polisi Tanzania na juzi iliitoa Dodoma FC.

SINGIDA UNITED- 4/10

Haifanyi vizuri kwenye Ligi Kuu ambako inashika nafasi ya 18 kwenye msimamo lakini imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya ASFC. Ina kundi kubwa la wachezaji wa kawaida ambao wanaweza kuwa kwao kuipa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

AFRICAN LYON- 2/10

Inashika mkia kwenye msimamo wa ligi na miongoni mwa timu nane zilizotinga robo fainali, inaonekana mnyonge kuliko zote. Kwa kuangalia kikosi chake kilivyo na kundi kubwa la wachezaji wasio na uzoefu, kuna uwezekano finyu kwao kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.