Mastaa wa England waliotaka kuzihama timu zao dirisha lililofungwa jana

Friday August 10 2018

 

LONDON, ENGLAND. DIRISHA la usajili Ligi Kuu England umefungwa na yaliyotokea yametokea. Kwenye dirisha hilo la uhamisho wa wachezaji kwenye majira haya ya kiangazi lililofika tamati jana Alhamisi, kuna mastaa kibao kwenye Ligi Kuu England walifichua dhamira za kutaka kuzihama timu zao kwenda kwingineko.

Toby Alderweireld (Tottenham)

Beki Mbelgiji, Toby Alderweireld kwa nguvu zote alitaka kuachana na Tottenham Hotspur na kocha wake Mauricio Pochettino alikuwa tayari kuachana na mchezaji huyo ambaye alikuwa akitajwa sana huko Manchester United.

Dirisha la usajili lilikuwa likifungwa jana na hivyo kilichokuwa kikisubiriwa ni kuona kama beki huyo wa kati atakuwa ametimiza ndoto zake za kuachana na Spurs.

Toby alisugua sana benchi kwenye kikosi cha Spurs msimu uliopita, hivyo hakutaka jambo hilo lijirudie na ndio maana ametaka kuhama.

Danny Drinkwater (Chelsea)

Miaka miwili iliyopita, kiungo Danny Drinkwater alicheza soka la kiwango cha juu sana na kuisaidia Leicester City kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Lakini, huko na huko anakasa uhamisho wa kwenda kujiunga na Chelsea, mahali ambako hakwenda kufurahia maisha mazuri kama alivyokuwa King Power.

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Drinkwater aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kuachana na Chelsea, ambayo ilimtumia kwa dakika 521 tu kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.

Danny Ings (Liverpool)

Ni sahihi kusema tu kwamba bahati haijawahi kuwa upande wa Danny Ings tangu alipokamilisha uhamisho wake wa Pauni 6.5 milioni kutoka Burnley kwenda Liverpool kwenye msimu wa 2014-15. Mambo yake yamekuwa magumu huko kwenye kikosi cha Jurgen Klopp na sasa kwa kuwapo kwa wakali Sadio Mane, Roberto Firmino, Mohamed Salah na sasa Daniel Sturridge mambo yanakuwa magumu zaidi kwa Ings na ndiyo maana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi alichokuwa akitaka ni kuachana tu na Liverpool.

Vincent Janssen (Tottenham)

Alinaswa akitokea AZ kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2016, Tottenham wameshindwa kupata thamani halisi ya pesa zao, Pauni 17 milioni walizolipa kupata huduma ya mshambuliaji huyo wa kimnataifa wa Uholanzi.

Amefunga mara chache sana kwenye ligi, huku straika Harry Kane akionekana kuwa ndiye chaguo la maana kwa kocha Mauricio Pochettino.

Kukwepa kukaa kwenye benchi, Janssen alilazimisha sana kuhama sana kwenye kikosi cha Spurs kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi lililofungwa jana.

Loris Karius (Liverpool)

Mambo yamekuwa si mambo tangu alipofanya makosa mawili yaliyoigharimu timu yake ya Liverpool kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.

Kipa Loris Karius yamemkuta makubwa huko Liverpool ambapo ameletwa kipa mwingine, Alisson Becker, akinaswa kwa pesa nyingi. Kuona hilo, Karius aliona njia pekee ya kujinusuru ni kuachana tu na wababe hao wa Anfield na ndiyo maana alilazimisha sana kuhama Liverpool wakati wa dirisha la usajili lililofika tamati jana. Ametimiza ndoto yake?

Ruben Loftus-Cheek (Chelsea)

Kocha Maurizio Sarri amefichua kwamba Ruben Loftus-Cheek hataondoka kwenye kikosi chake cha Chelsea baada ya kucheza vizuri kwa mkopo huko Crystal Palace msimu uliopita.

Lakini, staa huyo alikuwa na ufahamu wa wazi kabisa kwamba kubaki Stamford Bridge ni kujiweka kwenye matatizo tu kwa sababu kupata namba mbele ya viungo waliopo kwenye timu hiyo hasa baada ya ujio wa Mateo Kovacic na Jorginho, kupata nafasi ya kucheza ni ngumu na ndiyo maana akili yake ilikuwa kwenye kuachana na timu hiyo.

Anthony Martial (Man United)

Winga Mfaransa, Anthony Martial hakutaka kuweka kificho juu ya dhamira yake ya kutaka kuachana na Manchester United kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka huu. Martial alitaka kuachana na timu hiyo inayonolewa na Mreno Jose Mourinho kwa sababu hakuwa akimhakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Wakati dirisha la usajili linafungwa jana kitu kichokuwa kikisubiriwa kwa hamu ni kuona kama winga huyo atakuwa ametimiza ndoto zake za kuachana na Man United mwaka huu.

Danny Welbeck (Arsenal)

Kufunga mabao 15 kwenye mechi 80 za ligi kwa mshambuliaji Danny Welbeck hazitoi wastani sahihi kwa klabu ya Arsenal ambayo ingependa kupata kutoka kwa mchezaji huyo ili kuamini ana kitu cha muhimu kufanya kwenye kikosi chao.

Kutokana na hilo, suala la kumwona Welbeck akisugua benchi kwa muda mrefu msimu ujao ni mkubwa na ndiyo maana mwenyewe alitaka kulitumia dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi kuihama timu hiyo yenye maskani yake Emirates. Akibaki inakula kwake kocha Unai Emery harembi.

Kurt Zouma (Chelsea)

Hali ni mbaya kwa beki wa kati Kurt Zouma huko Chelsea. Lakini, mambo yangekuwa tofauti sana kama Mfaransa huyo asingepata maumivu ya goti, kwa sababu tayari alikuwa ameshaishika Chelsea iliyokuwa chini ya kocha Guus Hiddink.

Msimu uliopita alikwenda kucheza kwa mkopo Stoke City kabla ya sasa kurudi kwenye klabu yake ya Chelsea iliyopo chini ya Maurizio Sarri. Kwa jana, jina lake lilihusishwa na Man United, lakini ukweli Zouma mwenyewe mipango yake ilikuwa kuachana na wakali hao wa Stamford Bridge.

Paul Pogba (Man United)

Kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, ilionekana wazi kwanini Manchester United ililipa Pauni 89.3 milioni kunasa saini ya Paul Pogba. Kiungo huyo alicheza soka la kiwango cha juu sana akitawala kwenye kiungo sambamba na N’Golo Kante na hivyo kuipa Ufaransa ubingwa huo wa dunia. Kwenye kipindi cha usajili huo wa dirisha la majira ya kiangazi, Pogba aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kuihama Man United huku Juventus na Barcelona zikitajwa kuhitaji saini yake. Jana ndio ilikuwa siku ya kuamua yote hayo