Manchester United kila siku afadhali ya jana!

Monday May 13 2019

 

MANCHESTER ENGLAND.

MANCHESTER City wametinga fainali ya Kombe la FA. Liverpool ipo kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni hivyo pia kwa Tottenham Hotspur, nao wametinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal wametinga fainali ya Europa League, watachuana na wababe wenzao, Chelsea waliotinga hatua hiyo ya fainali kwenye michuano hiyo ya Europa League.

Timu zote hizo zinaunda ile Big Six kwenye Ligi Kuu England. Timu iliyokosekana hapo ni Manchester United, ambayo yenyewe inasubiri kutazama fainali hizo. Inachekesha, lakini huo ndiyo ukweli.

Hakuna taji, hakuna Top Four na hakutakuwapo na Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Old Trafford kwa msimu ujao.

Lakini, unaambiwa hivi kwa msimu huu, uliomalizika hapo jana Jumapili, Man United ina mambo mengi ya kuyasahau, maana ilikuwa ni mwaka wa shida kwao. Wakinolewa na makocha wawili ndani ya msimu mmoja, kwanza Jose Mourinho akaondoka, akaja Ole Gunnar Solskjaer, lakini hakuna ahueni, kila mmoja ni afadhali ya mwingine.

Cheki hapa mambo yanayothibitisha mwaka wa shida katika kikosi cha Man United chenye maskani yake Old Trafford.

Gundu laanzia kwa Mourinho

Gundu lilianzia kwa Mourinho baada ya kuifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kuvuna pointi chache mwanzoni mwa msimu kitu ambacho hakijawahi kutokea kwenye timu hiyo tangu msimu wa 1990-91. Man United ilivuna pointi 26 tu katika mechi 17 za mwanzo kwenye ligi msimu huu. Hiyo ina maana ilipoteza pointi 25. Kwa ujumla wake, Man United imevuna pointi 176 kwenye Ligi Kuu England chini ya Mourinho, ikiwa chache kuliko za vigogo wengine Man City (222), Spurs (202), Chelsea (200) na Liverpool (196) tangu Agosti 2016.

Yateswa kinomanoma na Liverpool

Kwa data zilizokusanywa na Opta kuanzia msimu wa 2003-04, ambapo hadi kufika sasa ni miaka 15 hiyo, Man United ilikuwa haijawahi kucheza na Liverpool na kisha kukutana na mashuti mengi kama ilivyotokea Desemba mwaka jana huko Anfield, ambako Liverpool ilipiga mashuti 36 na kufunga mabao matatu, Man United ikichapwa 3-1. Hiyo ndio iliyokuwa mechi ya mwisho kwa Mourinho kuinoa Man United. Kichapo hicho kiliwafanya Liverpool kuwaacha Man United kwa pointi 19 kwenye msimamo baada ya mechi 17 tu. Haya yalikuwa manyanyaso makubwa kwa Man United kufanyiwa na mahasimu wao hao.

Beki zinaruhusu mabao kama chujio

Hakika kwenye msimu huu wa Ligi Kuu England, Man United imekuwa ikiweka rekodi ambazo hata wenyewe hawazipendi. Man United haijawahi kuruhusu wavu wake kuguswa mfululizo kama ilivyofanya msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 45. Kipa David de Gea na mabeki wake walikuwa wakiruhusu mabao tu kama chujio linavyopitisha maji. Man United ilijikuta ikiruhusu mabao katika mechi 13 mfululizo kwenye michuano yote ikiwa ni mara ya kwanza tangu Agosti 1971. Mbaya zaidi kwa kipindi cha kuanzia Februari hadi Aprili mwaka huu, imeshindwa kufunga bao katika mechi tano.

Wamepigwa mfululizo ugenini

Rekodi za mechi za ugenini baada ya kuanza mwaka 2019, Man United imekuwa mbovu ikiwa ni mara ya kwanza tangu Machi 1981, wakati huo kikosi hicho kilipokuwa chini ya kocha Dave Sexton, ambapo waliruhusu kipigo katika mechi tano mfululizo walizocheza ugenini katika michuano yote. Safari hii ikiwa chini ya Solskjaer rekodi hiyo ilijirudia, ambapo walikumbana na vichapo vitano mfululizo vya ugenini. Vipigo hivyo ni pamoja vya 2-0 kutoka kwa Arsenal, viwili vya 2-1 kutoka kwa Wolves kwenye ligi na Kombe la FA, kipigo cha 3-0 kutoka kwa Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kile cha 4-0 kwenye ligi kutoka kwa Everton.

Kufungwa mabao mengi kwenye ligi

Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Cardiff City, Man United iliandika rekodi yake kwenye Ligi Kuu England kwa kuruhusu mabao mengi zaidi, ambapo yalikuwa 52. Kile kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton huko Goodison Park kiliwashtua wengi, lakini kilithibitisha pia ubovu wa safu ya ulinzi ya timu hiyo na kuruhusu mabao tu. Msimu huu umekuwa wa kwanza kwa Man United kuruhusu wavu wake kuguswa zaidi ya mara 50 kwenye Ligi Kuu England ikiwa ni mara ya kwanza tangu msimu wa 1978-79, ambao walimaliza kikosi hicho kikiwa kimeruhusu mabao 63 kwenye ligi.

Yakutaka na kipigo kingine cha bao nyingi

Wakati wanachapwa 4-0 na Everton mwezi uliopita, hicho kilikuwa kipigo kikubwa cha tano Man United kuwahi kukutana nacho kwenye Ligi Kuu England, lakini kilikuwa cha kwanza tangu mwaka 2016. Mwaka huo, ilichapwa 4-0 dhidi ya Chelsea. Hivyo ndivyo vipigo vikubwa zaidi kwa Man United kuwahi kukutana navyo ndani ya miaka hiyo mitatu. Huko nyuma waliwahi kupigwa nyingi zaidi, wakiruhusu nyavu zao kuguswa mara tano kwenye mechi dhidi ya Newcastle (5-0 mwaka 1996), Chelsea (5-0 mwaka 1999) na Man City (6-1 mwaka 2011).

Guardiola awadhalilisha Old Trafford

Pep Guardiola imekuwa kocha wa kwanza kuibuka na ushindi katika mechi zake zote tatu za kwanza alizokwenda kucheza Old Trafford. Mbaya zaidi ushindi huo wa Guardiola amekuwa akiupata na kikosi cha Man City, mahasimu wakubwa wa Man United. Haijawahi kutokea kocha mwingine aliyewahi kushinda mara tatu katika mechi zake za kwanza kucheza uwanjani hapo, Sam Allardyce na Ronald Koeman, wao walishinda mara mbili tu katika mechi zao zao za hapo Theatre of Dreams. Guardiola amepageuza Old Trafford kuwa mahali kwa kujibebea matokeo tu, akitesa hapo katika kipindi cha Mourinho na hivi karibuni timu hiyo ikiwa chini ya Solskjaer.

Kipigo kizito cha jumla michuano ya Ulaya

Man United ilikuwa na mechi kadhaa za kuburudisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini kipigo kile kizito cha mabao 3-0 uwanjani Camp Nou mbele ya Barcelona, ambao walishinda pia mechi ya kwanza kwa 1-0 Old Trafford imewafanya wasonge mbele kwa jumla ya mabao 4-0. Haya ni matokeo ya hovyo sana ya mechi mbili iliyowahi kupata Man United kwenye michuano ya Ulaya. Matokeo mengine ya kuhuzunisha ni pale walipochapwa 5-2 na AC Milan msimu wa 1957-58 nusu fainali ya Kombe la Ulaya na 4-1 dhidi ya Atletico Madrid kwenye raundi ya 16 bora ya Kombe la Washindi Ulaya msimu wa 1991-92. Kipigo cha huko Nou Camp kilikuwa cha tano kukumbana nacho kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Lakini, pia waliweka rekodi ya kushindwa kupiga shuti lolote kulenga goli tangu mwaka 2005.

Yaharibu ugenini mechi ya mwisho

Man United ingepaswa kumaliza msimu wao vyema kabisa katika mechi yao ya mwisho waliyocheza ugenini na kuwafariji mashabiki wake wakati ilipokwenda kucheza dhidi ya timu iliyoshuka daraja Huddersfield Town. Timu hiyo ilikuwa na pointi 14 tu kabla ya kucheza na Man United na hapo ilikuwa imetokea kupokea vipigo tisa mfululizo. Lakini, cha ajabu Man United ilishindwa kuwafunga na kutoka sare ya 1-1. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011-12, timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Alex Ferguson ambapo walishindwa kupata ushindi katika mechi yao ya mwisho ya ugenini katika msimu. Ingeshinda dhidi ya Huddersfield ingeweka hai matumaini yao ya kumaliza ligi ndani ya Top Four.

Yashindwa Top Four kwa mara ya nne

Msimu huu ni mara ya nne kwa Man United kushindwa kuwamo kwenye Top Four tangu Ligi Kuu England ilipoanza na hivyo kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kitu kibaya zaidi ni kuona timu hiyo ikishindwa kufikisha pointi 70 msimu huu. Kabla ya mechi ya jana walikuwa na pointi 66, ambazo ni chache zaidi kuwahi kuzipata kwenye ligi hiyo, ambapo mara ya mwisho kupata pointi kama hizo ilikuwa mwaka 1992. Lakini, pia imekuwa mara yao ya nne kushindwa kufikisha pointi 70, namba za pointi ambazo zilikuwa zikigalagazwa na timu hiyo katika kipindi ilichokuwa chini ya Alex Ferguson.