Makula, Huche wajipange na wakali hawa

Sunday April 15 2018

 

By OHANA CHALLE, ARUSHA

BAADA ya kuonyeshana ubabe kwa siku 11 tangu yalipoanza mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Australia Aprili 4, kwenye Uwanja wa Carrara, sasa mipango mipya inapaswa kuanza.

Katika Michezo hiyo Tanzania haijafanya vyema hadi sasa na katika michezo minne ambayo tumewakilishwa tumeambulia patupu na matarajio pekee yamesalia leo kwenye marathon.

Tanzania iliwakilishwa katika michezo ya tenisi, ngumi, kuogele na riadha na leo Jumapili Watanzania watatu watafunga pazia katika mbio ndefu, mwanamke akiwa Sarah Ramadhan pekee wakati wanaume akiwemo Saidi Makula, na Stephano Huche.

USHINDANI MKALI

Sio kazi nyepesi kwa wanariadha hao kuondoka na medali kutokana na ushindani na rekodi mbalimbali za wawakilishi wa Kenya na Uganda ambao wamepeleka timu iliyokamilika katika riadha.

Kwa haraka unaweza kusema tumaini la kubeba medali ya aina yoyote ni asilimia chache kwenda kwa Tanzania licha ya lolote kuweza kutokea katika michezo.

Kenya na Uganda pamoja na kutopeleka wanariadha wenye majina makubwa lakini imejipanga kwa kuwapatia fursa wawakilishi wengine kuonyesha uwezo wao katika mashindano hayo huku bingwa namba mbili katika mashindano yaliyopita (2014) Stephen Chemlany akiwa hajashiriki kwa awamu hii.

Bingwa wa mashindano ya dunia ya mwaka jana huko London, Geofrey Kipkorir ambako Alphonce Simbu aliibuka namba tatu na kunyakua medali shaba huko London naye hajashiriki, pia Daniel Wanjiru Bingwa wa London Marathon ya mwaka uliopita hatashiriki.

WAKALI WAO

Mbali na kutowapeleka wanariadha waliotamba mwaka uliopita, Kenya imetuma kikosi kazi ambacho wana uhakika wa kuleta ushindani na hata medali katika mashindano hayo. Rekodi zao ni matata na Watanzania kama wanataka kuwatikisa lazima wajipange vilivyo. Orodha yao hii hapa;

KENNETH MBURU

Alizaliwa Septemba saba mwaka 1973 huko Limuru Kenya. Alitwaa medali yake ya kwanza mwaka 2008 katika mashindano ya Prague huko Jamuhuri ya Czeck akitumia saa 2:11:06, miezi minne baadaye alishinda tena katika mashindano ya Toronto Water Marathon huko Canada 2:11:00 mashindano ambayo alishinda mara nne mfululizo.

Mwaka 2009 alikuwa mshindi katika mashindano ya Mumbai Marathon huko India akitumia saa 2:11:51, Desemba 2010 alikuwa bingwa Singapore Marathon na kunyakua Dola 50,000, lakini muda wake mkali zaidi ni ule wa saa 2:07:36 aliouweka Jamhuri ya Czech Mei 8, 2011 katika mashindano ya Prague.

JULIUS KARINGA

Pamoja na kuwa mkongwe kwenye mchezo huu bado hana rekodi za kutisha katika anga za kimataifa lakini lolote linaweza kutokea kwenye michezo. Baadhi ya mashindano aliyoshiriki ni nusu marathon huko Dubai akitumia saa 1:02:22, na marathon akimaliza kwa saa 2:08:01 yote mwaka 2012.

NICHOLAS KAMAKYA

Mfukuza upepo huyu alizaliwa Januari Mosi 1985. Ni Mwanariadha wa mbio ndefu, mwaka 2009 alimaliza wa pili mashindano ya nusu Marathon ya Prague akitumia saa 1:00:09 pia alimaliza nafasi kama hiyo kwenye mashindano ya Beijing Marathon.

Mwaka 2011 alishinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Gold Coast Marathon akitumia saa 2:10:01, kabla ya kuboressha zaidi muda wake huko Uholanzi mwaka huo katika mashindano ya Amsterdam akitumia saa 2:06:34 alipomaliza wa nne. Mwaka 2012 alikimbia Berlin Marathon na kumaliza nafasi ya nne akitumia saa 2:08:28.

SARAH AJIPANGE

Kwa upande wa Wanawake Tanzania ikiwakilishwa na mwanariada Sarah Ramadhan pekee katika mbio ndefu huku muda wake bora anaotamba nao ni saa ni 2:33.08 aliouweka huko Ujerumani mashindano ya Dusseldorf Aprili 30, 2017.

Kenya itawakilishwa na Sheila Jerotich ambaye muda wake bora ni saa 2:27:34 katika Marathon aliouweka Oktoba Mosi mwaka jana huko Slovakia na saa 1:19:25 katika nusu marathon yaliyofanyika Septemba 25 mwaka juzi huko Lexembourg.

Mfukuza upepo mwingine ni Hellen Nzembi ambaye alizaliwa Januari 3, 1987 na mara nyingi alikuwa akipenda kushiriki mbio fupi lakini Desemba 9, 2009 alitamba katika nusu marathon huko India akitumia saa 1:10:50 kabla ya mwaka 2014 kujitosa kwenye marathon huko Poland na kumaliza akitumia saa 2:35:58.

Mwingine ni Shelmith Nyawira ambaye hajavuma sana kwenye riadha lakini anaweza akafanya maajabu kwani Oktoba 14 mwaka jana alifanya mambo makubwa katika mashindano yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam akitumia saa 1:15:31 kwenye nusu marathon.

Kwa upande wa wakilishi wa wanawake kwa namna moja au nyingine unaweza kuona Sarah Ramadhan ana unafuu kama atakuwa amejipanga ipasavyo kuliko Makula na Huche.

UGANDA HAWATANII

Ukisikia fulu mziki ndicho walichokifanya Uganda kwa wawakilishi wa marathon na yupo Robert Chemonges huyu alikuwa mwakilishi wao katika mashindano ya dunia mwaka jana na Simbu aliibuka na medali huko London.

Chemonges mwenye miaka 21 alimaliza nafasi ya 43 akitumia saa 2:21:24. Bado umri unamruhusu kufanya mapinduzi kwa kuwa anaonekana kijana ambaye taifa lake linamwamini kwa kuzidi kumpatia nafasi kwenye mashindano ya kimataifa.

Mpaka jana Uganda walikuwa na jumla ya medali 18 katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola.

SOLOMON MUTAI

Mutai ni Bingwa namba tatu katika mashindano ya dunia ya mwaka 2015 yaliyofanyika Beijing China akitumia saa 2:13:29.

Mwaka 2014 aliiwezesha nchi yake kushika nafasi ya tano katika mashindano ya dunia ya nusu Marathon alipomaliza nafasi ya 26 katika mashindano yaliyofanyika Bulgaria na alimaliza nafasi ya nne katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka huo.

Mfukuza upepo mwingine ni Alex Chesakit huyu mwaka 2010 katika mashindano ya ndani ya nusu marathon aliweka muda bora wa saa 1:03:49 kabla ya mwaka jana oktoba 22 kwenda huko Canada na akatumia saa 2:12:32 katika marathon wakati muda bora wa Huche ni aliweka Tunisia mwaka juzi ni saa 2:14.18 na Makula ni saa 2:12.01 alioweka kwenye mashindano ya Daegu Aprili 3 mwaka juzi.