Breaking News
 

MAKALA: Wanakatwa top six

Friday January 12 2018

 

LONDON, ENGLAND

NDIYO kwanza Januari inaelekea katikati na mchakamchaka wa usajili unazidi kupamba moto. Klabu vigogo kwenye Ligi Kuu England nazo zinachuana vikali katika kutafuta wachezaji wa kuongeza kwenye vikosi vyao.

Lakini, hilo la kuongeza likifanyiwa kazi, linaendana pia na wale wa kuwaondoa na hii hapa ni orodha ya wachezaji watano katika kikosi kikosi cha Top Six, ambao wanapaswa kufunguliwa milango ya kutokea Januari hii.

ARSENAL - WACHEZAJI 5

Arsene Wenger tayari ameshamfungulia mlango wa kutokea Francis Coquelin kwenda Valencia kwa ada ya Pauni 12 milioni, hivyo kuna wachezaji wengine wa kuwapiga bei kwenye kikosi chake hasa kwa dirisha hili la Januari. Wachezaji wengine wanaopaswa kufuata nyayo za kiungo huyo ni Mohamed Elneny, Alex Iwobi, Chuba Akpom na Theo Walcott, anayewindwa na Southampton. Arsenal ina wasiwasi juu ya kuwaachia wachezaji wake vijana baada ya kuona Alex Oxlade-Chamberlain anafanya vizuri huko Liverpool.

CHELSEA - WACHEZAJI 5

Straika Michy Batshuayi mambo yake hayaendi kabisa chini ya kocha Antonio Conte kutokana na kutoaminiwa na Mtaliano huyo na hivyo kusugua tu benchi kwenye Ligi Kuu England. Ikiwa ni mwaka wa fainali za Kombe la Dunia, Batshuayi anahitaji kubadili timu kwenye dirisha hili la Januari ili kuweka wazi matumaini yake ya kuwamo katika kikosi cha Ubelgiji kwa ajili ya fainali hizo. Wachezaji wengine wanaostahili kufuatana na Batshuayi kuelekea mlango wa kutokea huko Stamford Bridge ni Baba Rahman, Kennedy, Charly Musonda na Eduardo.

LIVERPOOL - WACHEZAJI 5

Daniel Sturridge anapambana na hali yake huko Liverpool kutokana na kuwekwa benchi na kocha Jurgen Klopp. Fowadi huyo amekuwa akishindwa kulinda kiwango chake cha kiuchezaji na kubwa linatokana na kusakamwa na majeruhi ya mara kwa mara. Sturridge ni miongoni pia mwa wachezaji wanaopigia hesabu fainali za Kombe la Dunia, lakini itakuwa busara pia kwa Liverpool kumpiga bei ili kupunguza bili yao ya mishahara. Wachezaji wengine ambao Liverpool inafaa kuwafungulia geti la kutoka Anfield ni Adam Bogdan, Dejan Lovren, Jon Flanagan na Lazar Markovic.

MAN CITY - WACHEZAJI 5

Kipa Claudio Bravo ameshakuwa wa nyongeza kwenye kikosi cha Manchester City kwa sasa. Kocha Pep Guardiola anaonekana kutokuwa na mipango naye na si ajabu kama ukisikia kwenye dirisha lijalo la usajili akiingia tena sokoni kusajili kipa mpya. Bravo alitua Etihad kumbadili Joe Hart, lakini amedumu msimu mmoja tu kabla ya kuporwa nafasi pia na Ederson. Ukimweka kando Bravo, wachezaji wengine ambao watafunguliwa au wanafaa kufungulia mlango wa kutokea huko Etihad ni Joe Hart, Jason Denayer, Yaya Toure na Patrick Roberts. Guardiola haonekani kuwa na mipango endelevu ya kuwatumia wachezaji hao, hivyo ni wakati wa kuwaondoa kikosi chake haraka ili kupumua.

MAN UNITED - WACHEZAJI 5

Ripoti zinafichua kwamba, Marouane Fellaini amemwambia kocha Jose Mourinho hataki kusaini dili jipya kwenye cha Man United ikiwa na maana kuwa yupo tayari kuachana na timu hiyo itakapofika mwisho wa msimu. Lakini, Mourinho anaweza kumwondoa mchezaji huyo ili kupunguza bili ya mishahara kufanya usajili wa wachezaji wengine usiwe na presha. Wachezaji wote wa Man United wanaopaswa kufunguliwa wote ni wa kikosi cha kwanza na mara kwa mara wamekuwa wakionekana kwenye kikosi cha timu hiyo. Ukimweka kando Fellaini, wachezaji wengine wanaopaswa kufunguliwa lango la kutokea Old Trafford ni Sam Johnstone, Matteo Darmian, Luke Shaw na Daley Blind.

TOTTENHAM - WACHEZAJI 5

Kocha, Mauricio Pochettino ametengeneza kundi bora kabisa la wachezaji kwenye kikosi chake cha Tottenham Hotspur. Lakini, wakati kipindi hiki kikiwa cha usajili, kuna baadhi ya wachezaji anapaswa kuwatema ili kuongeza wengine wapya ambao, watakuwa na maana na faida katika mipango yake. Orodha ni ndefu, lakini mastaa watano ambao hakika Spurs inapaswa kuachana nao kwenye dirisha hili la Januari ni pamoja na Paulo Gazzaniga, Danny Rose, Moussa Sissoko, Erik Lamela na Vincent Janssen. Sissoko amekuwa mzigo tu kwenye kikosi hicho na hana jipya kama alivyokuwa Newcastle.