Kwangu siku hazigandi ila kwa Boban zinaganda!

NAKUMBUKA mwaka 1990 nikiwa Darasa la Tatu Shule ya Msingi Kazima, Tabora, nilicheza halaiki kwenye shughuli ya kuzimwa kwa Mwenge wa Uhuru zilizofanyikia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini humo.

Shughuli hii ndio ilikuwa ya kwanza rasmi kufanyika kwenye uwanja huo na ilitumika kuuzindua rasmi, japo kabla ya hapo, ulishatumika kwenye ziara ya Papa Yohana Paulo wa Pili.

Shule niliyosoma, Kazima ilikuwa kwenye Kijiji cha Kazima kilichopo nje kidogo ya Tabora Mjini, barabara ya kwenda Nzega. Hapo kuna bwawa kubwa lililokuwa likipeleka maji Tabora mjini. Baba yangu alikuwa akifanya kazi hapo.

Kiijiji hiki kilianzishwa na Mtemi Mirambo, wakati akipigana vita na Waarabu (miaka ya 1880) waliosaidiwa na Henry Morton Stanley, ambaye alikuwa safarini kumtafuta Dk Livingstone.

Mirambo alikuwa akikaa Urambo, lakini alipozinguliwa na Waarabu, akaja kuwasubiri Tabora, ili wakati wakitoka Pwani kwenda Ujiji, awafundishe adabu.

Alipowanyoosha mara ya kwanza, akahisi watarudi tena, hivyo akaenda pembeni kidogo ya mji wa Tabora na kuwasubiri, watakaporudi awanyooshe tena. Hapo alipokwenda ndipo hadi sasa ni kijiji cha Kazima.

Hii ndio vita iliyomfanya Stanley kumbatiza Mteni huyo jina la “The African Bonaparte”.

Baada ya vita hii na Mirambo kurudi kwake Urambo, Kijiji cha Kazima kikahamiwa na wakazi wengine.

Wakati huo Kazima ilikuwa ndani ya Wilaya ya Tabora vijijini, kata ya Itonjanda, Tarafa ya Uyui, tofauti na sasa imehamishiwa Tabora mjini na Uyui imechukua nafasi ya wilaya ya Tabora Vijijini.

Nilikuwa nikipenda sana mpira, hasa timu ya Milambo. Lakini kijijini pale sikuwa nikipata furaha niliyoitaka, hivyo kila wikendi nilikuwa nikienda mjini na familia yangu ilikuwa ikiishi huko kabla ya kuhamia kikazi Kazima.

Nyumba yetu ilikuwa mtaa wa Migazi, jirani na alipokuwa akiishi nyota wa zamani wa Milambo, Dadi Phares.

Phares ndiye aliyenifanya nisifurahie maisha ya kukaa Kazima kwa sababu nikiwa mjini, namwona yeye na wachezaji wengine kibao, akiwemo Athumani Tippo (Zizzou Fashion), waliokuwa wakija pale kumtembelea mwenzao. Hawa walikuwa mashujaa wangu.

Hii sasa ilishakuwa 1992 na nakumbuka siku Phares anafunga bao la ushindi kwa kichwa dhidi ya Mount Meru Warriors kwenye fainali ya Kombe la Taifa na timu ya Mkoa wa Tabora, Mashujaa wa Unyanyembe, ilishinda 1-0.

Wachezaji wengi wa Mashujaa walitoka Milambo, akiwemo Said Sued ‘Scud’, ambaye mwaka mmoja uliopita yaani 1991, alikuwa Yanga.

Wakati sisi tukipata umaarufu kwa kucheza halaiki, kuna mwanafunzi mwenzetu wa darasa la tatu kama sisi, lakini shule tofauti, alikuwa maarufu zaidi yetu kwa kucheza mpira.

Mwanafunzi huyu alikuwa akisoma Shule ya Msingi Gongoni, pale pale Tabora mjini. Zaidi ya yeye mwenyewe kuujua mpira, mwanafunzi huyu pia alikuwa maarufu zaidi kwa sababu mbili;

Kwanza, alikuwa mtoto wa Mzee mmoja maarufu sana pale mjini, aliyefahamika kama Moshi TT. Wakati huo pale Tabora kulikuwa na Moshi watatu maarufu.

1. Moshi Traffick, aliyekuwa shabiki mkubwa sana wa Yanga. Siku ikija Yanga, alikuwa akiendesha baiskeli ya njano, akivaa kofia ya pama ya njano. Mawani ya njano na kila kitu cha njano.

2. Moshi Shamba, aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule moja ya Msingi (nimeisahau).

3. Moshi TT, ambaye ndiye baba yake na yule mwanafunzi wa Gongoni.

Pia, mwanafunzi huyu alikuwa maarufu kwa sababu kaka zake walikuwa maarufu zaidi.

Mwanafunzi huyu alikuwa akiitwa Haruna Moshi na kaka zake walikuwa kina Yahaya, Mrisho na Idd. Hawa walikuwa watu wanaoujua mpira balaa pale Tabora. Yaani ni mafundi hasa wa mpira hadi inatia raha.

Ukiwaondoa kaka zake ambao walishakuwa wakubwa, majina mengine ya kati yalikuwa Ally Mayay Tembele kutoka Mihayo Sekondari.

Pia, kulikuwa na watoto wa Mwanza Road kama Mohamed Banka. Walikuwepo kina Alfred Kidao na wengine wengi ambao walivuma kweli kweli.

Mwaka ule, 1990, nilishiriki UMITASHUMTA na nikachaguliwa timu ya kata yangu ya Itonjanda kwenda kwenye mashindano ya tarafa yetu ya Uyui. Huku nikakutana na Shamba Moshi, mtoto wa Moshi Shamba, yule mwalimu mkuu aliyekuwa maarufu.

Mashindano yalifanyika Shule ya Msingi Upuge na katika mchezo wetu dhidi ya Kata ya Ikolongo, mchezaji mwenzangu wa kata ya Itonjanda ambaye nilikuwa nikisoma naye darasa moja Kazima, alianguka na kukanyagwa tumboni na mchezaji wa timu pinzani.

Utumbo ukapasuka na akalazwa hospitali ya mkoa, Kitete. Akafanikiwa upasuaji lakini haikuwa bahati, akafariki dunia. Hapo moyo wangu ukatumbukia nyongo kuendelea tena kucheza mpira, niliona mchezo wa hatari na ilinisumbua sana akili.

Bahati mbaya zaidi kwangu, nilihama Tabora mwaka 1993 nikiwa darasa la sita. Mambo yote ya kimtaa kuhusu Tabora sikuyajua tena.

Miaka mingi baadaye, nikawa nalisikia jina la Haruna Moshi tena likiwa limeongezeka na jina la tatu la BOBAN.

Sikuwahi kudhani huyu ndiye yule Haruna, mtoto wa Moshi TT, hadi nilipokutana na mwanahalaiki mwenzangu niliyekuwa nikisoma naye Shule ya Msingi Town School kabla sijahamia Kazima.

Akaniambia yule Haruna wa Gongoni Star ndiyo huyu Boban. Hiyo ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mwaka huu, 2018, ni miaka 24 tangu nikiwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kazima. Sasa nina miaka 40 lakini mwanafunzi mwenzangu wa darasa la tatu mwaka 1990, aliyekuwa Shule ya Msingi Gongoni, Haruna Moshi, mtoto wa Moshi TT, bado damu inamchemka na anajiunga na klabu kubwa zaidi hapa nchini, Yanga SC.

Hajiungi kama kocha au kiongozi, bali kama mchezaji tena anayesubiriwa kwa hamu kubwa sana.

Mimi nazeeka, Haruna anazidi kuwa kijana. Kwangu siku hazigandi, kwa Haruna zinaganda tu.