Breaking News
 

MAKALA: Kwa mauzo yao, unabeba majembe ya maana tu

Friday January 12 2018

WASHKAJI : Kwa muda mrefu Neymar alitamani

WASHKAJI : Kwa muda mrefu Neymar alitamani kucheza na Coutinho kikosini Barcelona, lakini kwa sasa dili limekubali ila wanapishana. 

LONDON, ENGLAND

BADO hatujasahau kwamba Mdachi Virgil van Dijk ndiye beki ghali zaidi duniani kwa sasa. Hii ni baada ya kusaini Liverpool kwa dau la Pauni 75 milioni akitokea Southampton, kabla na wao kumuuza Philippe Coutinho kwa mkwanja mnene wa Pauni 145 milioni.

Uhamisho wa Coutinho umekuwa bonge la biashara kwa sababu umeleta faida kubwa kwa wababe hao wa Anfield. Wao walimnunua Mbrazili hiyo kwa Pauni 8.5 milioni tu miaka michache iliyopita.

Basi kama ulikuwa hujui, hii hapa orodha ya wachezaji waliouzwa kwa faida kubwa kwenye timu zao wakati wao walinunuliwa kwa pesa kiduchu tu.

PHILIPPE COUTINHO Pauni 136.5milioni

Liverpool wanachekelea tu kwa sasa baada ya kupiga faida ndefu kwenye mauzo ya staa wa Kibrazili, Coutinho. Kumpata mchezaji huyo, Liverpool ilitumia Pauni 8.5 milioni tu kumng’oa Inter Milan, lakini wao wamemuuza kwa Pauni 145 milioni kwenda Barcelona.

Kwa pesa hiyo, Liverpool imeingiza faida ya Pauni 136.5 milioni, pesa inayotosha kabisa kumsajili staa kama Paul Pogba akatua Anfield na chenji ya maana ikabaki benki.

NEYMAR PAUNI 120.42milioni

Wanasema kila mjanja na mjanja wake. Barcelona imepigwa pesa kibao kwa Philippe Coutinho na Ousmane Dembele, lakini yenyewe iliipiga pesa za kutosha tu PSG baada ya kuwauzia supastaa Neymar na kuingiza faida ya Pauni 120.42 milioni.

Barcelona yenyewe ilimnunua staa huyo kutoka Santos kwa Pauni 79.38 milioni kisha ikamuuza PSG kwa Pauni 199.80 milioni. Faida iliyopatikana inatosha kumsajili Thomas Lemar kutoka pale Monaco kisha ukabaki na chenji ndefu tu.

PAUL POGBA Pauni 93.7milioni

Wakati kiungo Mfaransa Paul Pogba anaondoka Manchester United kwenda Juventus, hakuwa ameuzwa kwani aliondoka bure kabisa. Lakini, kutokana na utaratibu uliowekwa na Fifa (Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani) kwa Pogba kukulia Man United, basi Juventus ilibidi kulipa fidia ya mchezaji huyo kukuzwa na timu nyingine na hapo iliwabidi kulipa Pauni 800,000 tu.

Miaka minne baadaye, Man United imerudi kumtaka staa wao huyo wa zamani, ndipo Juve ilipowauzia kwa Pauni 94.5 milioni na hivyo kupata faida ya Pauni 93.7 milioni, pesa ambayo unamsajili Riyad Mahrez na pesa nyingine inabaki.

OUSMANE DEMBELE  Pauni 81 milioni

Baada ya kumuuza Neymar kwa pesa nyingi huko PSG, Barcelona nao walilazimika kwenda kufanya usajili wa pesa nyingi. Walienda Borussia Dortmund kumsajili Ousmane Dembele. Ripoti zinadai kwamba Barcelona ililipa Pauni 94.5 milioni kumsajili Mfaransa huyo, ambaye Dortmund wao walimnasa kwa Pauni 13.5 milioni tu miaka michache iliyopita akitokea Stade Rennais. Jambo hilo limewafanya Dortmund kuingiza faida ya Pauni 81 milioni, pesa ambayo inatosha kuwasajili akina Alexis Sanchez wawili kwa mpigo.

GARETH BALE Pauni 77.6milioni

Bale alivunja rekodi ya dunia wakati alipohama Tottenham Hotspur kwenda Real Madrid kwa ada iliyoripotiwa kuwa ni Pauni 85 milioni. Lakini, imedaiwa pesa halisi ambayo Real Madrid ililipa ilikuwa Pauni 90.9 milioni. Spurs wao walimnunua Bale kutoka Southampton kwa ada ya Pauni 13.3 milioni, hivyo kwenye mauzo hayo walipiga faida ya Pauni 77.6 milioni, pesa ambayo kimsingi inatosha kumsajili Sergio Aguero.

CRISTIANO RONALDO  Pauni 67.5milioni

Manchester United iliripotiwa kumuuza Cristiano Ronaldo kwenda Real Madrid kwa Pauni 80 milioni. Lakini, kinachobainisha kwamba dili hilo lilikamilika kwa ada ya uhamisho ya Pauni 84.6 milioni. Kumbuka, Man United wao walimnasa Ronaldo kutoka Sporting CP kwa ada ya uhamisho ya Pauni 17.1 milioni, hivyo kuwafanya waingize faida ya Pauni 67.5 milioni katika mauzo hayo. Faida hiyo inafaa kabisa kumsajili Alexandre Lacazette.

VIRGIL VAN DIJK Pauni 62milioni

Bonge la faida kwa Southampton na ile staili yao ya kusajili wachezaji mafungu, inawakuza na kisha inawauza kwa pesa nyingi, kwa pesa hiyo wataweza kupata wachezaji wasiopungua watatu. Saints yenyewe ilimsajili Van Dijk kutoka Celtic kwa ada ya Pauni 13 milioni tu kabla ya Januari hii kumuuza Liverpool kwa Pauni 75 milioni, jambo lililowafanya kuingiza faida ya Pauni 62 milioni. Pesa hiyo inatosha kumng’oa Henrikh Mkhitaryan Man United.

ROMELU LUKAKU Pauni 58.2milioni

Usajili wake umekuwa gumzo kwa sasa huko Everton baada ya bosi wa timu hiyo kudai Romelu Lukaku mwanzoni kabisa alikuwa na mawazo ya kuhamia Chelsea kabla ya kubadili mawazo na kwenda Man United kwa kile alichokidai kwamba, amepokea ujumbe wa kichawi kutoka Afrika.

Lukaku anataka kumshtaki bosi huyo. Lakini, Everton ilimsajili fowadi huyo kwa Pauni 31.82 milioni kutoka Chelsea na kumuuza Man United kwa Pauni 90 milioni, tofauti na ambavyo imekuwa ikiripotiwa kuwa Pauni 75 milioni. Hapo Everton wamepiga faida ya Pauni 58.2 mlioni, pesa ambayo inatosha kumsajili Raheem Sterling.

RAHEEM STERLING Pauni 55.62milioni

Kwa sasa amekuwa bonge la staa huko Manchester City. Lakini, Raheem Sterling huyu huyu miaka michache iliyopita wakati Liverpool ilipomsajili kutoka QPR ililipa Pauni 630,000 tu kabla ya kumtumia mchezaji huyo na kisha kumuuza kwa pesa ndefu, Pauni 56.25 milioni ilipowapiga mkwanja mrefu Manchester City. Mauzo hayo yameifanya Liverpool kuingiza faida ya Pauni 55.62 milioni, pesa ambayo washambuliaji kama Christian Benteke unawapata wawili kwa mpigo.

LUIS SUAREZ Pauni 49.7milioni

Ilikuwa nafasi nyingine ya Liverpool kupiga faida kwenye mauzo ya staa wake wa maana kikosini. Hapa ilimuuza pia Barcelona, wakati wababe hao wa Nou Camp walipokwenda Anfield na Pauni 73.55 milioni kuhitaji saini ya straika huyo. Lakini, Liverpool yenyewe miaka michache iliyopita ilikuwa imemsajili Suarez kutoka Ajax, ambapo ililipa Pauni 23.85 milioni tu na hivyo kuwafanya kupiga faida ya Pauni 49.7 milioni, pesa ambayo inafaa kumsajili Mohamed Salah kwenye kikosi chako.

WACHEZAJI WENGINE

Kuna orodha ndefu ya mastaa waliouzwa kwa faida kubwa na timu zao na miongoni mwa kwa kuwataja kwa uchache ni John Stones, ambaye aliipa Everton faida ya Pauni 46.89 milioni ilipomuuza Man City , wakati Anthony Martial, aliipa AS Monaco faida ya Pauni 49.5 milioni ilipomuuza Man United, Luis Figo aliipa Barcelona faida ya Pauni 51 milioni ilipomuuza kwenda Real Madrid, huku Zinedine Zidane akiipa Juventus faida ya Pauni 63 milioni ilipomuuza kwenda Real Madrid.