Kumbe Firmino alifungwa lensi

Muktasari:

  • Alifunga bao dakika za majeruhi na kuifanya klabu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya PSG katika mchezo uliochezwa Anfield.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Roberto Firmino katika mchezo dhidi ya Totternham Jumamosi aliumia jicho lakini Jumanne wiki hii alicheza na kufunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alifunga bao dakika za majeruhi na kuifanya klabu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya PSG katika mchezo uliochezwa Anfield.

Kabla ya hapo alikuwa katika sintofahamu kutokana na kuumia jicho baada ya kugongana na Jan Vertonghen katika mchezo wa Ligi Kuu (EPL).

Majeraha hayo hayakuwa tatizo kwake kwani mara tu baada ya kuingia kipindi cha pil akitokea benchi aliipa ushindi muhimu klabu yake dhidi ya PSG.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazili alikosa mazoezi ya Jumatatu kutokana na majeraha hayo na alipumzishwa ili kutoa nafasi ya kupona na kuendelea na matibabu.

Katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara baada ya kunyanyuliwa na kupasha mwili alishika jicho lake la upande wa kushoto lililojeruhiwa na kidole cha Vertonghen. Hii ilikuwa kama ishara ya kujipa hamasa ya kufunga.

Alipofunga alishangilia kwa furaha na kuliziba jicho hilo kwa kiganja cha mkono na kuungwa mkono ushangiliaji huo na wenzake akiwamo Sadio Mane.

Hii inadhihirisha Firmino kwake Liverpool kwanza, majeraha ya jicho baadaye, hakujali hali aliyokuwa nayo zaidi ya kujituma na kupiga bao katika mchezo mgumu.

Lakini katika mechi hiyo Ligi ya Mabingwa hakupangwa kiholela ili acheze tu, bali kuna hatua zilizofanyika kuhakikisha hapati madhara yoyote kwa kushiriki mechi hiyo.

Moja ya hatua muhimu zilizofanyika ni kuwekewa lenzi maalumu ndani ya jicho ambayo ilikuwa na kazi ya kulilinda jicho na kumwezesha kupata taswira nzuri.

Lenzi za kupachika ndani ya jicho huvaliwa pia na kipa wa Manchester United, David De Gea hii ni kutokana na tatizo lake la kutoona mipira ya mbali.

Je, unajua jicho linavyofanya kazi?

Jicho ni mojawapo ya kati ya ogani kuu tano za fahamu inayotuwezesha kuona vitu mbalimbali ambavyo hupata tafsiri katika ubongo.

Majeraha ya jicho huwa yanauma sana pale yanapojitokeza kutoka na kiungo hicho kuwa laini na kuzungukwa na mishipa ya fahamu sehemu ya nje na ndani.

Kwa kawaida ni mawili upande wa kushoto na kulia na huwa na umbile ka kama yai yakijizungusha katika pango maalumu katika fuvu.

Ndani ya jicho huwa na lenzi ambayo huwa na kazi ya kuikuza miale yenye taswira ya vitu mbalimbali kisha huisafirisha mpaka eneo maalumu katika seli zilizopo kuta za nyuma ya jicho.

Hapo hupokewa na seli hizo na kusafirishwa na mshipa mkuu wa fahamu unapokea taarifa za picha na kuzipeleka katika ubongo kwa ajili ya kupata tafsiri.

Jicho linapopata majeraha ya kugongwa huweza kuambatana na maumivu, kubadilika rangi na kuwa jekundu, kumwaga machozi, kuwa na joto na pia kuvilia damu.

Sababu ya kuvikwa lenzi za kupachika?

Jicho linapopata majeraha kama ilivyokuwa kwa Firmino huweza kupata dalili nilizotaja, lakini kipindi cha jeraha kama lile vipo vitu ambavyo huwa vinaongeza jicho kuuma ikiwamo mwanga.

Firmino alivalishwa lenzi zijulikanazo kama Contact Lenses kwa lengo la kumpunguzia bughudha ya mwanga wa taa ambao mara nyingi husababisha maumivu katika jicho lililojeruhiwa.

Contact Lens hufanya kazi ikiwamo kudhibiti mwanga mkali (UV Light), kusahihisha hitilafu za kushindwa kuona vitu ikiwamo vya mbali au karibu.

Vilevile huwa na kazi nyingine ikiwamo kama urembo hutumika zaidi na wasichana na kubadili mwonekana wa jicho na kuwa wa kutisha kama zile zenye kutoa miali zinazotumiwa na waigizaji.

Ingawa kuna lenzi za aina mbili yaani lenzi mbonyeo (concave lens) na lenzi mbinuko (convex lens) zinazosaidai kusahihisha uoni hafifu.

Lakini kwa upande wa contact Lenses ambazo zinaweza kuwa lenzi mbonyeo au mbinuko kuna takribani aina tano za lenzi za kupachika jichoni ambazo zimetengenzwa kwa malighafi tofauti.

Zipo lenzi laini zilizotengenezwa kwa plastiki yenye majimaji kwa ndani ijulikanayo kama lenzi laini kitabibu soft lenses ambazo hizi ndo za awali kutengenezwa duniani.

Aina ya pili ni lenzi za Silikoni hizi ni za kisasa zaidi huwa na matundu ya kupitisha hewa ndani ya jicho kupitia eneo la jicho lijulikanalo kama Cornea.

Aina ya tatu ni lenzi zenye kupenyeza gesi inafanana kidogo lenzi za Silikoni nayo hupenyeza gesi na maji maji.

Aina ya nne ni lenzi mchanganyiko ijulikanayo kitabibu Hybrid Contact Lenses na aina ya tano ni lenzi za PMMA ambazo zimetenengezwa kwa plastiki ngumu ijulikanayo kama Polymethyl Methacrylate.

Katika aina hizi za lenzi zipo zinazoweza kuvaliwa kila siku na kutolewa na zipo ambazo zinavaliwa usiku mzima na huweza kukaa hata kwa siku saba mfululizo. Tofauti na lenzi zilizo katika miwani ya kuvisha nje ya macho ambazo huonekana kwa nje Contact Lens huwezi kuziona kama mtu amevaa kwani hutumbukizwa ndani ya jicho na kushikamana na jicho.

Lenzi alizovaa Firmino ni zile ambazo lazima kuvaa na kuzivua kila siku na kupachika unapofanya kazi za kila siku hizi hujulikana kitabibu kama daily wear. Mane alimtania Firmino kwa kusema haitaji macho ili kuweza kufunga. Firmino alimaliza salama mechi hiyo na anaendelea na uangalizi wa karibu na madaktari wa timu wakishirikiana na madaktari bingwa wa macho wa jijini Liverpool.