Kinachoiponza Manchester City hiki hapa

KASI ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester City ilipunguzwa kwa kiasi kikubwa, tena kwa ajabu ya kufungwa mfululizo.

Baada ya kushangazwa kwa kufungwa na Crystal Palace 3-2 Desemba 22, siku tatu tu kabla ya Krismasi, walipigwa tena 2-1 na Leicester kwenye Boxing Day na kuacha watu wengi vinywa wazi, huku kocha wao, Pep Guardiola akionekana akiishia kupatwa na kigugumizi akishika kichwa.

City baada ya kupigwa mara mbili walijikuta matumaini yao ya kutwaa ubingwa yakitiwa doa japokuwa Guardiola alisema bado kuna mechi nyingi za kucheza na kuzoa alama. Waliiacha Liverpool ikichekelea ikimaliza mwaka pasipo kupoteza hata mechi moja.

Imekuwaje Man City iliyoanza kwa moto hivyo, ikifunga mabao mengi na kushinda karibu kila mechi iangukie pua hivi tofauti kabisa na ilivyotarajiwa? City ina kikosi kipana na cha ghali ambapo katika karibu kila nafasi wapo wachezaji wawili wazuri kabisa.

Moja ya matatizo ninayoona ni kupwaya kwa mabeki wa pembeni; mmoja wao akiwa ni Fabian Delph. Ungeweza kumaizi hili vizuri kabisa iwapo ungetazama nusu ya kwanza ya mechi dhidi ya Leicester.

Guardiola alimweka benchi Kyle Walker baada ya kuwa na wakati mbaya uwanjani kwa muda na badala yake akamweka Danilo ambaye alishindwa kuonesha chochote kipya kilicho chanya, bali ni wazi alizidiwa upande huo.

Kule kushoto, Delph ambaye amekuwa kwa jumla akimshikia nafasi hiyo Benjamin Mendy kutokana na majeraha kimsingi na kwa asili si beki wa pembeni kushoto na ilidhihirika jinsi alivyozidiwa maarifa na kina Andros Townsend na Ricardo Pereira katika vichapo hivyo vya karibuni vilivyofikisha idadi ya mechi walizofungwa kuwa tatu kwa msimu huu tu kwenye EPL.

Na kwenye mechi dhidi ya Leicester Delph akaishia kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, ikimaanisha atakuwa nje zaidi na hivyo kuongeza maumivu zaidi kwa kikosi cha Guardiola.

Ghafla tu imetokea Man City imekuwa dhaifu kwenye wingi zote. Huko nyuma makocha wa timu pinzani wakitambua hilo walifanya upesi kuwaelekeza wachezaji wao kutumia udhaifu huo kushambulia na kweli wakapata mabao na ushindi.

Kutokana na hali ngumu kwa mabeki wa pembeni, imebidi mabeki wa kati wajaribu kutupa macho huko kuokoa jahazi. John Stones akijielekeza upande wa kulia na Aymeric Laporte kule kushoto. Unajua matokeo yake ni nini? City imebaki ikiwa hovyo hapo kati, hivyo kutoa mwanya kwa washambuliaji na mawinga kufanya yao; wakalala mechi hizo mfululizo.

Kukosekana kwa Fernandinho kwenye kikosi cha Man City kumeonesha wazi hali ilivyo mbaya kwa sababu haina aina ya mpiganaji sampuli ya mzima moto kama N’Golo Kante wa Chelsea mwenye mtindo wa aina yake. Anayeweza kukabiliana na kuchukua mipira eneo lolote la kiungo. Anayemkaribia kwa hapo Etihad ndiye Fernandinho, lakini Mbrazili huyu aliyepelekwa kulia kucheza sehemu ya Walker alishikwa.

Mabadiliko yamewaona wakali kama Kevin De Bruyne na Ilkay Gundogan kwenye kiungo cha kati nao wakishindwa kufanya mambo mazuri. Guardiola hakufanya siri, kwani alisema kiangazi angetaka kusajili kiungo mkabaji, Fred akikaribia na baada ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2018 kule Urusi, alikuwa na wasiwasi kwamba Fernandinho angeweza kuwa na hali ngumu hata kwa majeraha madogo tu ya tishu.

Hata tukienda kwa washambuliaji, tunaona kuna upotezaji wa mipira mingi sana kwa washambuliaji wale watatu wa mwisho pale mbele ambapo jamaa aliyekuwa akiwika sana katika Sergio Aguero naye akawa akipoteza mipira hovyo baada ya kuwa na maumivu ya mara kwa mara ya misuli. Ni kana kwamba anapata ‘kutu’ kwa jinsi anavyocheza, akifunga mabao matatu tu kutokana na michomo 15 aliyopiga tangu mwanzo wa Novemba hadi kipondo kutoka kwa Leicester. Alikosa mabao ya wazi kama mawili hivi.

Si huyu tu mwenye hatia kutokana na hali mbaya ya City, kwani kuna Raheem Sterling aliyetumwa kucheza pembeni lakini anaonekana kutofurahia wajibu huo huko. Leroy Sané alikuwa na kawaida ya kuleta vitu adimu kwa nyakati muhimu lakini sasa ameelekea kufanya makosa ya hapa na pale.

Guardiola anaweza kudai De Bruyne ndio kwanza anarejea baada ya kuwa nje kwa muda mrefu huku David Silva ambaye ni shujaa asiyesifiwa sana akiwa pia na majeraha yake. Ni wazi haya yangekuwa mapigo makubwa kwa timu yoyote ya Ulaya kwani ndio wabunifu na wanaozalisha mipira ya mabao.

Guardiola anajua mambo haya ni magumu wala hatarajii ataonewa huruma na watu wake na mashabiki, kwa sababu ni kocha wa moja ya vikosi ghali zaidi duniani, hivyo hata wawili au watatu wakikosekana basi ingetarajiwa wengine wazibe mapengo, hasa inapokuwa dhidi ya timu za kawaida kabisa kama Leicester na Palace.

Kilichodhihirika ni kwamba City inafungika ni kiasi cha wapinzani wao kujipanga tu na si ajabu ikashindwa kutetea ubingwa wake, tofauti na Guardiola alivyozoea na kufanya Ujerumani na Hispania akiwa an Bayern Munich na Barcelona mtawalia.