Kante awanyima raha Chelsea

Muktasari:

  • Uimara wa Kante (27) kwenye safu ya kiungo ulikuwa chachu katika kikosi cha Ufaransa ambacho miezi mitatu iliyopita kilifanikiwa kutwaa taji la Ubingwa wa Kombe la Dunia lililofanyika huko Russia akishirikiana vyema na Paul Pogba na Blaise Matuidi.

LONDON, ENGLAND.CHELSEA kijasho kinawatoka kwa sasa kutokana na kuhaha kumpa mkataba mpya kiungo wao mkata umeme, N’Golo Kante kufuatia Mfaransa huyo kuwekwa kwenye rada za Real Madrid.

Si jambo la kificho, Real Madrid wanahitaji huduma ya Kante wakiamini akitua kwenye timu yao mambo yatakaa sawa. Na katika kufanikisha jambo hilo, wametenga kabisa Pauni 80 milionni za kufanya biashara na Chelsea.

Jambo hilo limewatoa Chelsea kwenye usingizi na sasa wanataka kumsainisha mkataba mpya ili isije ikafika Januari akawaacha na kutimkia zake Bernabeu. Hali ya Real Madrid kwa sasa ni mbaya na huenda kwenye dirisha la Januari wakafanya usajili wa fujo kuweka sawa msimu wao.

Kante bado ana miaka mitatu kwenye mkataba wake huko Stamford Bridge ambao unamshuhudia kiungo huyo anayekaba hadi kivuli akilipwa Pauni 150,000 kwa wiki.

Mtu mmoja aliyekaribu na Kante alisema kiungo huyo kwa sasa akili yake ni kuitumikia Chelsea ndio maana aligoma kwenda kwenye timu za Paris Saint-Germain na Juventus zilizoonyesha nia na dhamira ya kumsajili, lakini mwenyewe haonekani kama atagoma kuhama Stamford Bridge kama Los Blancos wataleta ofa. Kante amekuwa maarufu kutokana na kazi yake ya kukaba anayofanya ndani ya uwanja na amekuwa hivyo tangu alipokuwa na kikosi cha Leicester City na kukisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England 2016. Alikuwa mchezaji bora wa Chelsea msimu uliofuatia baada ya kuachana na Leicester City. Chelsea wanafahamu pia Real Madrid wanamtaka mchezaji wao mwingine, Eden Hazard, lakini dili hilo haliwezi kufanyika Januari.