Jinsi ya kuepuka majeraha ya nyonga kwa wachezaji

KIUNGO wa Totenham, Moussa Sissoko amepata majeraha mapya katika mchezo wa juzi Jumatano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City.

Alilazimika kutolewa mwishoni mwa kipindi cha kwanza, ambapo ingawa aliombewa machela abebwe, alijitahidi kuchechemea na kutoka nje.

Mpaka sasa haijalezwa kwa kina nini kimemsibu ingawa taarifa za awaali zinaonyesha ni misuli ya makutano ya nyonga.

Itakumbukwa mchezaji huyu amekuwa akipata majeraha ya mara kwa hasa katika misuli ya maeneo ya nyonga na paja. Mwezi wa kwanza alipata majeraha ya nyonga na kinena yaliyomweka nje kwa wiki mbili.

Leo nitawapa ufahamu juu ya majeraha ya nyonga na njia za kupunguza majeraha haya.

Majeraha ya nyonga ni moja ya majeraha ambayo yanawakumba sana wanasoka wakiwamo pia wanamichezo wengine.

Tatizo hili pia ndiyo kikwazo kwa wanasoka kuwa nje ya mchezo kutokana na majeraha haya kuwafanya kukosa uwezo na kushindwa kukimbia kwa kasi ya kawaida.

Mara nyingi mchezaji anaweza kushiriki mchezo, lakini pale anaputumia nguvu sana hujikuta akijijeruhi na ataonekana akishika kona za pajani kutokana na hisia za maumivu makali na katika nyonga.

Sissoko ni mmoja wa viungo wa kati anayekaba na kushambulia akitumia nguvu hivyo kumfanya kuwa katika hatari ya kupata majeraha haya.

Majeraha ya nyonga hayakwepeki kwa mwanasoka. Hii ni kutokana na umuhimu wake kwani misuli ya eneo hili ndiyo inahusika kumwezesha mchezaji kucheza soka ikiwamo kukaba na kutoa pasi.

Hii ndiyo misuli ambayo inakufanya kuweza kutanua mguu kwa mwelekeo wa nje yaani kama vile kupiga msamba. Hata ukitazama mtindo wa ukabaji katika soka utaona kunahusisha kutanua miguu. Wakati wa kucheza mchezo wa soka, misuli mitano ya nyonga itahitajika kukunjuka na kujikunja ili kujongesha mwili katika mitindo tofauti.

Ikumbukwe mwanasoka anahitaji kupiga mashuti, kukaba, kukimbia kwa kasi na kuruka, mambo haya yote yanahitaji kufanyaka kazi misuli iliyojipachika katika nyonga.

Si wanasoka pekee yao wanaopata majeraha ya nyonga bali hata watu wa kawaida wasio wanamichezo wanapata.

Je unaifahamu nyonga?

Nyonga ni sehemu ya makutano baina ya paja na kiuno eneo la ndani, ni eneo ambalo sehemu ya tumbo linapoishia na ndiyo eneo miguu inapoanzia.

Eneo hili lina misuli mitano inayoshughulika na kushirikiana kuijongesha miguu kwenda pembeni.

Misuli hii ndiyo inawezesha kurudisha mguu kutoka pembeni na kurudi mguu sawa.

Eneo hili ndipo ulipo mpaka ambao una mfereji uitwao kitabibu ‘inguinal canal’, eneo ambalo ngiri (hernia) hutokea kwa wachezaji na watu wengine wasio wanamichezo.

Maumivu yoyote katika eneo hili nimatokeo ya shughuli za kimwili na michezo. Kupata vimichubuko vya ndani kwa ndani, kuchanika kwa misuli hii na kujivuta kulikopitiliza ni majeraha yanayowapata sana wanamichezo wengi

Maumivu haya ama majeraha yanaweza kumpata mtu yeyote na si lazima yawapate wanamichezo pekee.

Maumivu ya eneo hili yanaweza yakawa ni kujeruhiwa kwa bunda la misuli au nyuzi ndogo za misuli, nyuzi ngumu zinazoshika mfupa mmoja kwenda mwingine. Nyuzi ngumu za miishilio ya misuli inayojipachika katika mifupa.

Wanamichezo wanaocheza michezo kama mpira wa miguu, riadha, mpira wa kikapu na kuruka viunzi hupata sana majeraha haya na ndio kundi linaloongoza kupatwa na majeraha ya nyonga.

Mara nyingine maumivu haya yanaweza kusababishwa na ngiri kitaalam ‘inguinal hernia’ yaani ni hali ya sehemu ya utumbo kutoka katika pango lake na kwenda kujipachika katika pango la mfereji wa nyonga.

Ukiacha sababu nyingine za kujitoke za kwa maumivu haya kama vile maradhi ya tumbo na maradhi ya korodani leo tutajifunza zaidi dalili za majeraha ya nyonga yale yanayohusu majeraha ya michezoni.

Dalili na viashiria

Dalili ya majeraha ya eneo hili huwa ni pamoja na maumivu madogo mpaka makubwa katika nyonga, kuvimba, kubadilika rangi kuwa kama nyekundu, misuli kukakamaa, kuhisi misuli inavuta kwa ndani, kuchechemea au kushindwa kuutumia vema mguu.

Sissoko alionekana kushikilia eneo zaidi la makutano ya paja yaani eneo la kinena.

Mchezaji anashauriwa kuomba msaada haraka pale unapoona maumivu ya kwenye nyonga yanasambaa katika mgongo, kifua au tumboni na kama anapata homa.

Uchunguzi

Wataalam wa michezo huweza kuchukua historia ya mgonjwa kwa kina na kisha kumfanyia uchunguzi wa kimwili. Hapa ndipo mgonjwa hufanyiwa majaribio ya kimwili kuweza kubaini ishara za uwapo wa tatizo katika nyonga.

Sissoko anarajiwa kufanyiwa uchunguzi kwa kina kwa kupigwa picha za scan ambazo zinabaini majeraha ya kina ya tishu.

Matibabu yake na muda wa kupona utategemeana na uainishaji wa jeraha baada ya uchunguzi ingawa yapo majeraha ya aina tatu za majeraha ya nyonga.

NAMNA YA KUZUIA

Zipo hatua chache zinazoweza kuchukuliwa ili kuzuia majeraha haya kujitokeza kwa wanamichezo. Mojawapo ni kupasha mwili moto kabla ya kuingia mchezoni.

Mazoezi ya kunyoosha mwili kwa mazoezi mepesi ya mwili na viungo, kufanya hivi kunasaidia nyuzi laini za misuli, nyuzi ngumu za tendon na ligaments kulainika hivyo kuwa rahisi kukunjuka.

Ni vema kudhibiti uzito wa mwili nakutoruhusu kuongezeka uzito wa mwili kiholela.

Baada ya kupona mchezaji anapaswa kufuata mpango mzima wa mazoezi ya viungo na mafunzo ili kuweza kumrudisha katika uchezaji wake kwa kawaida.

Mojawapo ya zoezi maarufu la kunyoosha nyonga ni lile zoezi la kuwekewa mpira mkubwa katikati ya mapaja na kisha mchezaji huhitajika kuubana na kuachia mpira huo.

Zoezi hili jepesi husaidia kunyoosha misuli hiyo na kuiwezesha kuimarika kila siku.

Kwa mwanamichezo ambaye amejeruhiwa nyonga aepuke kurudi mapema uwanjani kabla ya muda uliopangiwa.

Ulaji wa mlo kamili uliozingatia kanuni za afya husaidia kuwa na mwili imara wenye afya njema. Zingatia ulaji wa vyakula vyenye protini kwa wingi ikiwamo maharage ya soya na samaki.

Kufika mapema katika huduma za afya pale dalili zinapojitokeza inasaidia ugunduzi wa majeraha ya nyonga mapema hivyo hatua madhubuti kuweza kuchukuliwa kabla ya jeraha kupata madhara zaidi.

Shikamana na ushauri wa madaktari, wataalam wa mazoezi ya viungo.