Ishu ya Gaucho KMC, eti Kaseja anahusika-2

Muktasari:

  • JUZI Jumanne tulianza makala ya kiungo fundi wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Abdulhalim Humoud 'Gaucho' aliyekuwa akiichezea KMC juu ya mgogoro wake dhidi ya mabosi wake waliomtuhumu ishu za kumendea wake wa wenzake.
  • Humoud aliweka bayana kila kitu juu shutma hizo na kufunguka mambo mengi yaliyochangia kuibuliwa kwa ishu hiyo aliyodai inawadhalilisha hata viongozi wenyewe kwani wameonyesha walishindwa kujipanga kumpakazia kitoto.
  • Leo Alhamisi tunamalizia mahojiano yaliyozaa makala na Humoud ambapo anamtaja kipa mkongwe, Juma Kaseja eti anahusika kwa sehemu kubwa kumharibia KMC. Kivipi? Endelea naye...!

TATIZO HILI HAPA
Gaucho anasema tangu ikiwa Daraja la Kwanza, alikuwa na KMC ya Fred Minziro na kufichua kocha huyo aliyepo Arusha United ni kiboko kwelikweli.
“Kukaa na kocha kama Minziro inahitaji mchezaji uwe timamu na haijawahi kutokea hata siku moja kupata shtuma kama hii, leo amekuja kocha wa kigeni kwa muda mfupi tu napewa shutma kama hizo.
“Kingine nataka watu waelewe tumepambana na ile timu ya KMC na wenzangu ambao wengi waliondolewa, lakini nilikuwa kati ya miongoni mwa wawili watatu ambao wamebakia kwa katika timu, kwa muda wa miaka yote walishindwa kupanda ila nilipofika hiki kichwa changu ndio kilifunga goli ambalo limeipeleka timu Ligi Kuu,” alieleza kwa hisia kali Gaucho.
Gaucho anasema yote hayo, viongozi wa KMC wameyasahau na aliamua alipaswa  kulipwa kama shukrani ya kuipeleka timu Ligi Kuu na hakustahili kuondoka katika mazingira kama haya.
"Kinachouma badala ya kupewa shukrani, lazima wamenipa kashfa ya vitu ambavyo sijafanya," anasema.
Anasema tatizo limekuja kwa vile dirisha dogo (linalofunguliwa leo) lilikuwa jirani na walikuwa na watu wao wanaowataka wawaingize kikosini ndipo wakaamua kumtengenezewa zengwe lisilo na mashiko.
“Viongozi wa KMC wameamua kufanya hivyo kwa sababu ya dirisha la usajili linakariabia kufunguliwa ndio wakaamua kunichafua wakati nilishaondoka katika timu zaidi ya mwezi mmoja na nusu nyuma,” anasema.
“Wamenikashfu pamoja na familia yangu wao wanaishi kwa amani, huku walipo wakati mimi nikiishi katika mazingira magumu na familia yangu na inawezekana katika kipindi hiki naishi tofauti na mke wangu kama asingekuwa mkakamavu.
“Lakini naawambia viongozi wa KMC watambue kama si mke wangu, meneja wangu na familia yangu kiujumla ningekuja mbele ya umma kusema mambo yao ambayo wanayafanya katika timu na siwezi kuzungumza kwani ni miongoni ya mambo ambayo si sahihi."
 
ETI, KASEJA ANAHUSIKA
Gaucho anasema nawashukuru mashabiki wake kwa kumuunga mkono katika kipindi kigumu alichonacho bila kuwasahau mkewe na meneja wake, huku akisisitiza kama mabosi wake wataendelea kumchafua atayaanika madudu yao.
Katika mahojiano hayo, Gaucho anasema katika kipindi cha muda mfupi ambacho aliishi KMC ikicheza Ligi Kuu, hakuwa na mahusiano mazuri na mchezaji wenzake Juma Kaseja.
Anasema tofauti zao hazikuanzia KMC tu, bali kumbe tangu walipokuwa wote Simba na kufichua;
"Unajua Kaseja ana tabia fulani hivi zilizoo tofauti na wengine na sio mimi tu, bali hata kwa wachezaji wengi wanaomfahamu wanaelewa na hakuna anayependezwa naye."
Anafichua mambo mengi juu ya tabia za kipa huyo mkongwe (Mwanaspoti imeshindwa kuanika moja kwa moja kimaadili), lakini akidai kipa huyo anapenda kuonekana bora kuliko wenzake.
"Yapo mengi na zipendezwi naye ndio maana tumekuwa hatuivi pamoja naye tangu tukiwa Simba, kule niliwahi kutaka kumpiga kwa ajili ya mambo yake hasa kutokana na ukaribu wake wa viongozi na kusikilizwa chochote akisemacho."

VITA YA UNAODHA
Hata hivyo Gaucho anajishtukia na kusema mpaka anaondoka, KMC hajajua kama fitina za Kaseja ndizo zilizomvua unahodha katika klabu hiyo ama;
"Sitaki kufahamu kama alinizunguka na kwenda kupewa unahodha nikiwa KMC kwani ndio tabia zake za kwenda kupenda kukaa kwa kocha na kuzungumza na kocha kuanzia asubuhi hadi jioni."
"Hivyo suala la kuvuliwa unahodha na kupewa mimi wala sijali maana hata nilipofika KMC timu ikiwa daraja la kwanza sikuwa nahodha ila nilipewa baadaye na Kaseja alivyokuja akapewa na wala sikuumia  ila nilichomiumiza ni kupewa shutuma hizo na kunichukulia amani yangu," anasema.
Gaucho anasema kama ni ishu ya utovu wa nidhamu, mbona hakuwahi kuingia matatani Taifa Stars ilipokuwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo?
"Nataka nikuambia kitu kimoja tangu yupo Maximo sijawahi kupata shida ya kinidhamu mpaka anaondoka hapa nchini sasa makocha wetu wengine hawa na viongozi baadhi hawataki kuona kuna mchezaji ambaye yupo katika mastari hawataki," anaongezea Gaucho.
Gaucho anasema wengine hawajazoea kuzunguka nahisi hilo ndio linamtesa lakini kuhusu nidhamu si la kweli hilo jambo labda sikubali kuona mchezaji anapewa nafasi wakati uwezo wangu na wake ni tofauti

AMPA KIFYAGIO MEYA SITTA
"Naondoka hapa KMC nikijivunia kuiweka sehemu salama ambayo wao wenyewe walikuwa wakiangaika kwa muda mrefu kingine sikuwahi kugombana na kiongozi yeyote akiwamo Meya Benjamin Sitta,  nimpongeze mno kwani nilikuwa nikiishi naye vyema kama ndugu," anasema.
"Naondoka hapa KMC, lakini kikubwa ambacho nitakumbuka hapa ni mambo haya ambayo wamenifanyia katika kipindi hiki kwa sababu hiki walichonifanyia hayakuwa sahihi na hata kama naondoka nilitakiwa kuondoka kwa amani." anaongeza Gaucho.
Gaucho kabla ya kutemeshwa mzigo KMC, aliwahi kukipia katika timu kadhaa zikiwamo JKU, Polisi zote za Zanzibar, Ashanti United na baada ya hapo alienda Oman kabla ya kukipiga Mtibwa Sugar, Simba, Azam, Jomo Cosmo ya Afrika Kusini, Sofapaka ya Kenya, Coastal Union na Majimaji.
Nyota huyo anasema kwa sasa anasubiri kuona ataibukia wapi kwa kuamini kuwa kipaji chake ca soka kinamwezesha kokote kucheza, huku akishikilia msimamo wake daima huwa hataki kuburuzwa ndio maana anaonekana mkorofi.