Ilikua hivi nje ya dk 90

UUKIACHANA na matokeo ya ushindi wa Simba dhidi ya watani wao jadi, Yanga katika mechi ya dabi iliyochezwa juzi Jumamosi kulikuwa na mambo yasiyokuwa ya kawaida nje ya dakika 90 yaliyowashangaza wengi.

Licha ya timu hizo kongwe kutakiwa kufanya mambo yenye mfano wa kuigwa na klabu nyingine changa lakini zilifanya mambo yasiyo ya kawaida katika mchezo soka.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya matukio yasiyo ya kawaida katika soka ambayo yalitokea katika mchezo huo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga.

YANGA KUJA NA MAGARI MAWILI

Kikosi cha Yanga wakati kinawasili uwanjani saa 7:20 mchana kilitanguliza gari ambalo ndio siku zote hutumika kuwabeba wachezaji wake katika kila mechi lakini katika mchezo huo wa Simba ilikuwa tofauti.

Ilikuwa hivi, gari hilo lilifika uwanjani lakini wakati mlango ukifunguliwa huku waandishi wa habari wakitega kamera zao kupata picha za wachezaji wa Yanga wakishuka haikuwa hivyo, walioshuka walikuwa ni watu wengine wasiokuwa wachezaji wa klabu hiyo. Baada ya muda mfupi kikosi cha Yanga ndipo kilipowasili uwanjani kikiwa katika gari lingine aina ya Toyata Costa ambalo tangu likiwa getini makomandoo wa timu hiyo hawakutaka mtu yeyote alisogelee.

SIMBA, YANGA KIVINGINE

Yanga iliwasili kwanza uwanjani na ilipofika haikutumia mlango ambao unatumiwa na wachezaji na makocha kuelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo. Walishuka wote na kupita mlango mdogo ambao upo pembezoni mwa mlango mkubwa ambao ndio unaotumika kila siku.

Msafara wa Simba nao ulipowasili saa 8:30 mchana wakiwa katika gari jipya aina ya Higer ambalo lilikwenda moja kwa moja katika mlango mdogo ambao hutumika na waandishi wa habari. Makomandoo wa Simba waliwazuia waandishi kuingia ndani hadi wachezaji na watu wa benchi la ufundi la Simba walipopita katika mlango huo na kuacha mlango mkubwa ambao ndio unaotumika kila siku wanapocheza mechi hapo.

YANGA NJIA NYINGINE

Mara baada ya kumaliza kupasha misuli timu zote mbili zinaingia uwanjani kwa ajili ya utambulisho, wachezaji wa Yanga walifanya tukio lingine ambalo si utamaduni wa soka.

Katika mchezo huo kulitengwa eneo maalumu la wachezaji wa timu zote mbili kupita ili kuingia uwanjani. Simba ilifanya hivyo ila jambo la kushangaza wachezaji wa Yanga hawakutumia njia hiyo ambayo ilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

YANGA WAGOMA

Mara baada ya kuingia uwanjani wachezaji wa Yanga kutumia mlango mwingine na si ule maalumu ambao umetengwa kwa ajili ya kazi hiyo,pia hawakutumia chumba cha kubadilishia nguo kilichotengewa kama tararibu zilivyo. Yanga ilitayarishiwa chumba cha kubadilishia nguo uwanjani hapo lakini jambo la kushangaza haikukitumia chumba hicho na kwenda kutumia mahala pengine ambapo hapakuwa rasmi kwa ajili ya matumizi hayo.

AJIBU NA YONDANI

Tukio lingine ambalo lilikuwa la kushangaza ni wakati wa utambulisho wa wachezaji wa timu zote mbili, Simba walikuwa wa kwanza na kazi ya kutambulisha wachezaji kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe ilifanywa na nahodha wake, John Bocco.

Upande wa Yanga ambao ndio waliokuwa wenyeji wa mchezo huo, nahodha Ibrahim Ajibu ndiye aliyewatambulisha wachezaji wenzake huku akiwapa mikono lakini alipofika kwa beki, Kelvin Yondan alikataa kumpa mkono kisha akamuangalia usoni na kuachana naye na beki huyo mkongwe kumpa mkono wake Mwekyembe.

simba WaZIMIA

Mbali ya Simba kuondoka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Meddie Kagere katika dakika 71, mashabiki wengi wa Simba walipoteza fahamu na kuzimia na watu wa huduma ya kwanza waliwabeba kwenda kuwapatia matibabu ya awali.

Ilitegemewa kuwa kutokana na timu yao kuwa mbele kwa bao hilo, basi ni mashabiki wa Yanga ndio wangepoteza fahamu na kuzimia lakini mambo yalikuwa tofauti.

SIMBA KIBENDERA

Wachezaji wa Simba nao walitoa kali wakati wanatoka vyumbani kuingia uwanjani kupasha misuli hawakupita moja kwa moja katika eneo la katikati ya uwanja na badala yake walikwenda mpaka kwenye goli la Kusini. Baada ya kufika katika goli hilo wachezaji wote walipita kwa kuzunguka katika kibendera cha kona.