SPOTI DOKTA: Haya yamechangia kifo cha Athumani Chama ‘JOGOO’

Muktasari:

  • Kitabibu, zipo sababu nyingi zinazochangia tatizo la kuwa na moyo mpana, lakini mara nyingi uwepo wa shinikizo la juu la damu la muda mrefu au uwepo wa matatizo ya mishipa inayotawanya damu katika misuli ya moyo ndiyo inasababisha tatizo hili.

MWAKA mpya umeanza kwa pigo kwenye medani ya soka nchini, baada ya kumpoteza mwanasoka nguli, Athumani Juma ‘Chama’ maarufu pia kama Jogoo.

Mwanasoka huyu aliyewahi kutamba na klabu ya Yanga miaka ya 1980 alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili siku chache tu zilizopita.

Marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo kwa muda mrefu kama ilivyoelezwa kwenye vyombo vya habari na alizikwa Jumanne katika makaburi ya Kisutu na kuhudhuriwa na mamia ya wadau wa soka nchini.

Mwanasoka huyu aliyekuwa beki wa kati na kupata umaarufu alipokuwa akiichezea Yanga, mpaka anafariki alikuwa ni mmoja wa wadau wakubwa wa soka nchini.

Ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wakimjulia hali alipokuwa akiugua walielezwa kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo ambao ilikuwa ni moyo kuwa mpana na kujaa maji.

Naomba nizungumzie tatizo hili kidogo. Kitabibu, zipo sababu nyingi zinazochangia tatizo la kuwa na moyo mpana, lakini mara nyingi uwepo wa shinikizo la juu la damu la muda mrefu au uwepo wa matatizo ya mishipa inayotawanya damu katika misuli ya moyo ndiyo inasababisha tatizo hili.

Uwepo wa matatizo kama haya ndiyo yanayosababisha moyo kushindwa kufanya kazi yake ya kusukuma damu mwilini. Matatizo kama haya yanahitaji matibabu ya muda mrefu ili kulidhibiti tatizo.

Kifo huweza kutokea pale tatizo linapokuwa kubwa pamoja na kujitokeza madhara mbalimbali, ikiwemo moyo kushindwa kufanya kazi.

Magonjwa ya moyo ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiwapata mamilioni ya watu duniani ni pamoja na shinikizo la damu, moyo kushindwa kufanya kazi na shambulizi la moyo.

Katika kona hii leo nitatoa ufahamu wa jumla juu ya magonjwa ya moyo lengo ni kukujuza juu ya viashiria mbalimbali vya magonjwa ya moyo ili kuweza kuwa na tahadhari dhidi ya magonjwa haya.

VIASHIRIA NA DALILI

Pengine una umri wa zaidi ya miaka 45 na unajikuta unapiga hatua chache tu unahisi kuchoka haraka na kupumua kwa shida isivyo kawaida.

Kiashiria kama hiki si cha kupuuzia hata kidogo hasa kwa watu wenye umri wa miaka 45-60 kuendelea, wenye unene uliopitiliza, kisukari, kiwango kikubwa cha lehemu mbaya (Cholestrol) na shinikizo la damu.

Sababu kubwa ni uwezekano wa viashiria hivyo kuwa ni vya magonjwa ya moyo, ingawa mara nyingi dalili zake huwa zinajificha. Mtu hujistukia ghafla amedondoka na kupoteza fahamu bila kuwa na dalili yoyote.

Magonjwa ya moyo yameshika kasi kwa sasa na yanashika namba moja katika kusababisha vifo vya ghafla hivyo ni vizuri kujihami mapema angalau kwa kupata ufahamu wa viashiria vyake.

Moja ya kiashiria muhimu vya mtu yoyote kufahamu ni kuchoka kwa urahisi baada ya kupiga hatua chache, hali hii huambatana na kubanwa au kukatika kwa pumzi.

Mfano mzuri ni pale mtu anapopanda ngazi na kuhisi kuchoka huku akitweta na kupumua kwa tabu.

Uwepo wa maumivu ya kifua ni kiashiria ambacho hakiepukiki kupuuzwa kwa watu wazima. Maumivu hayo yanaweza kuwa ya kubana au kukamua. Unaweza kuhisi kama kuna uzito fulani kifuani mfano kama vile kuna mtu anakukanyaga kifuani.

Maumivu hayo ya kifua yanaweza kuongezeka wakati mwili unapojongea au kufanya zoezi na vilevile kunapokuwepo na badiliko la hisia za kimwili (Emotional stress).

Maumivu hayo huwa zaidi upande wa kushoto wa kifua na yanaweza kusambaa katika bega na kushuka chini ya mkono wa kushoto.

Maumivu hayo yanaweza kutulia kwa dakika kadhaa pale unapoacha kufanya kazi au zoezi.

Kwa baadhi ya watu hasa wanawake wanaweza kupata maumivu makali yanayosambaa katika shingo, taya, mgongo na mkono.

Mabadiliko ya mapigo ya moyo kama vile kudunda kwa kasi isiyo ya kawaida au kudunda hovyo hovyo ni kiashiria kinachoweza kujitokeza pale kunapokuwa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Maumivu makali ya kichwa yanayoambatana na kuona mawimbi au giza na kupoteza fahamu ghafla.

Kupata kichefuchefu, kuhisi kujaa tumbo na kupata kiungulia pasipo uwepo wa matatizo ya mfumo wa chakula. Kukoroma kusiko kwa kawaida wakati wa usingizini.

Kutokwa la jasho la baridi pasipo sababu maalumu na kupata kikohozi kisichoisha na kujaa/kuvimba miguu ikiwamo katika vifundo vya miguu.

Ni vizuri kwa yeyote atakayekuwa na viashiria na dalili hizi kufika katika huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi, matibabu au ushauri.

Tumempoteza nguli wa soka kwa matatizo haya moyo, nyuma yake mbele yetu. Vizuri tujihami na matatizo haya mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.

Jenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa jumla wa kiafya angalau mara moja kwa miezi sita.