Hakuna miujiza kwa Neymar

Friday February 8 2019

 

By Dk. shita samwel

KATIKA usiku wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mchezaji wa kimataifa wa Brazil, Neymar Jr aliwaeleza waalikwa alitamani kupatiwa zawadi ya kifupa kipya cha mguu wake uliojeruhiwa.

Usiku huo ulioitwa usiku wa vazi jekundu ulikuwa ni maalumu kwa staa wa PSG aliyekuwa akitimiza umri wa miaka 27 huku akiwa ni majeruha ya kifupa cha mguu wa kulia kijulikanacho kitabibu kama Metatarsal.

Straika huyo wa PSG ya Ufaransa alipata majeraha haya ya kifupa cha tano cha mguu wa kulia katika mchezo wa Kombe la ligi dhidi Strasbourg mwishoni mwa mwezi uliopita.

Pamoja na jeraha hilo lililomfanya atumie magongo mawili ya kutembelea haikumzia kula bata katika siku yake maalumu ya kuzaliwa ndani ya Jiji la Paris.

Akiwa stejini na magongo yake alicheza kuimba pamoja na wachezaji wenzake Dani Alves na Kylian Mbappe na ndipo alipotoa maneno hayo huku akihuzunika sana kupata majeruha haya.

Alisema hakuna zawadi nzuri ambayo ingemkosha kama kupata zawadi ya kifupa kipya kwani kingemfanya kurudi uwanjani na kuivaa Manchester United Jumatano katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.

Sharobaro huyo akiwa mwenye huzuni iliyofunikwa na furaha ya kuingia umri huo alionekana akiwa nadhifu akitinga suti nyekundu iliyoendana na magongo yake yenye nakshi nyekundu.

Lakini hizo zilikuwa ni ndoto tu, majeraha hayo yatamfanya kuwa nje ya uwanja kwa wiki 10, hivyo kukosa mechi za 16 bora ya UEFA pamoja na mechi za Ligi Kuu ya Ufaransa.

Kifupa kama hiki ndicho kinachomsumbua mara kwa mara kiungo wa zamani wa Arsenal anayekipiga West Ham, Jack Willshere ambaye amewekewa boriti maalumu katika kifupa hicho.

Tofauti na Willshere ambaye alifanyiwa upasuaji, Neymar Jr amekwepa kisu na badala yake anatibiwa bila ya kufanyiwa upasuaji.

Baada ya jopo la madaktari bingwa wa mifupa kukaa na madaktari wa PSG na kujadili kwa kina matibabu ya nyota huyo waliweza kukubaliana kuwa asifanyiwe upasuaji.

Moja ya sababu inayoelezwa kukubaliana na matibabu hayo ni kutokana na jeraha la upasuaji kuchukua muda mrefu kupona ukilinganisha na matibabu ya bila upasuaji ambayo yatachukua wiki 10.

Endapo angelifanyiwa upasuaji ingemlazimu kukaa nje uwanja msimu wote mzima uliobaki jambo ambalo ingewa baya kwa PSG.

Ikumbukwe pia mchezaji huyu ni mmoja kati wachezaji wenye mikataba mikubwa ya matangazo ya biashara ikiwamo ya kampuni za vinywaji na vifaa vya michezo. Kukosekana kwake uwanjani si pigo kwa PSG pekee, bali pia kwa makumpuni yaliwekeza kwenye umaarufu wa Neymar, hivyo matibabu yake si ya mchezo mchezo ni lazima kila kitu kiwe sawa.

KWANINI JERAHA HILI?

Tatizo alilolipata Neymar Jr ni moja kati ya jeraha yanayowapata wanasoka mara kwa mara kutokana na eneo hilo kutumiwa na mchezaji kusakata soka, hivyo kuwa katika hatari ya kujeruhiwa kirahisi.

Vifupa hivyo vilivyopo mguuni eneo la chini huvunjika au kupata nyufa kutokana na kujijeruhi au kuchezewa faulo.

Eneo hili hujulikana kama funiko likiwa pamoja na kifundo cha mguu, eneo ambalo huwa na harakati nyingi wakati wa kucheza ikiwamo kwa kutumika kupiga mashuti, kukaba, kuruka, kukimbia na kucheza faulo.

Eneo hili ndilo ambalo hutumika kupiga mpira ya faulo au mashuti mara kwa mara na vilevile ni eneo ambalo hukanyagwa kirahisi wakati wa mikimiki ya uwanjani ikiwamo kukabana.

VIFUPA VILIVYOJERUHIWA

Vifupa vya metatarsal idadi yake huwa ni vitano. Kabla ya vifupa hivyo huanza vifupa vya mwanzoni ambavyo ndivyo vidole vya mguuni.

Wakati wa kutembea, kukimbia kuruka na kutua, kifundo huweza kutua vibaya na kujipinda hivyo kujeruhi mfupa na tishu laini ikiwamo nyuzi ngumu ambazo hujivuta kupita kiasi na kusababisha kupata majeraha.

Majeraha haya yanaweza kusababisha nyufa katika mifupa, kututumka kwa mfupa na kuvunjika vifupa vidogo ikiwamo ile ya vidoleni mwa mguu.

Uwepo wa mejaraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogo vidogo huweza kuambatana na majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu.

Kurudia kutumia funiko la mguu kupiga mpira ni mojawapo ya jambo linalochangia kutokea kwa majeraha ya funiko la mguu pamoja na kifundo cha mguu kwa jumla.

Vilevile kujirudia kuchezewa faulo eneo la kifundo kunachangia majeraha ya mara kwa mara ya eneo hili. Ni vigumu kwa mwanamichezo kukwepa kuchezewa faulo.

Mfupa aliojeruhiwa Neymar ni mdogo wa tano ambao upo sehemu ya chini ikiunda kundi la mifupa mitano katikakati ya makundi mengine mawili ya mifupa eneo la funiko la mguu.

Kundi la kwanza kitabibu huitwa Pharenges vipo sehemu ya mbele ambayo ni mifupa ya vidole vya mguu na huku sehemu ya nyuma hupakana na kundi la kundi jengine la mifupa ijulikanayo tarsal.

Makundi haya matatu ya mifupa ya mguu yaani sehemu ya chini ndio yanayounda sehemu inayojulikana na wanasoka kama funiko. Sehemu hii ndio inayotumiwa kupiga mpira mara nyingi.

Makundi haya ya mifupa ya miguu sehemu ya chini huweza kuunda maungio madogo kwa vifupa hivi kuungana kama vile mnyororo.

Endapo shinikizo litakuwa kubwa kiasi litazidi uwezo wa mifupa hii kustahimili ndipo majeraha ya kuvunjika yanapojitokeza. Unaweza kuvunjika mfupa mmoja kama ama ikavunjika zaidi ya miwili.

Kuvunjika kwa mifupa hii kunatofautiana katika eneo la mfupa, ukubwa wa jeraha na aina yake ikiwamo kapata nyufa, kutawanyika vipande vipande na kuvunjika na kutoka nje ya ngozi.

Vilevile vinaweza kupasuka na kugawanyika au kutogawanyika sehemu mbili, kuvunjika na pande mbili kupishana na kupinda.

Bahati nzuri mfupa wa Neymar umepata ufa na kujeruhi tishu jirani, hivyo kwa aina ya tiba aliyopewa isiyo ya upasuaji, mfupa utarudishwa katika mhimili wake na mguu huo kutulizwa mahala pamoja kwa kifaa tiba kilicho kama kiatu kwa majuma manne hadi sita ili uweze kupona.

Mara nyingi majeraha ya mifupa haya yana matokeo mazuri, mchezaji hupona kabisa na kurudi uwanjani kuendelea na soka.

Hakuna miujuza wa kupata mfupa mpya na kupona haraka, zaidi ni kusubiri mfupa huu kuunga na kupona wenyewe.