Unampigaje virungu mtu mwenye tiketi mkononi?

Tuesday May 21 2019

 

By EDO KUMWEMBE

NILIKUWA Genk pale Ubelgiji kwa staa wetu Mbwana Samatta. Walikuwa wanacheza na Timu ya Antwerp. Moja kati ya mechi ambazo zilikuwa zinaamua ubingwa Genk msimu huu. nikacheka kimoyomoyo ustaarabu wa wazungu.

Kinadada wawili walinipokea nje ya uwanja walipoona nashangaa bila ya mwelekeo. Wakaniuliza kama nataka kupakaa rangi za Genk usoni. Baada ya kufanya hivyo wakatimiza jukumu lao la kunielekeza ninapopaswa kuingilia kwenda uwanjani, hadi katika kiti changu.

Wiki moja baadaye nilikuwa Hispania kutazama Barcelona ikicheza na Getafe. Katika Uwanja wa Nou Camp nikapokelewa na wadada wawili waliovaa fulana zilizoandikwa ‘Ask me’. Walikuwa wanamaanisha kwamba niwaulize kama nina tatizo lolote. Nikawaonyesha tiketi yangu, mmoja akanipeleka hadi katika siti yangu.

Ni utaratibu ule ule ambao nimewahi kuushuhudia katika michuano mikubwa ya Kombe la Dunia. Ni utaratibu ule ule ambao nimewahi kuushuhudia katika mechi mbalimbali ambazo nimewahi kutazama Ulaya. Kilichotokea majuzi Genk na Barcelona ilikuwa ni kukumbushwa tu utaratibu wa wenzetu kwamba bado upo vile vile na ustaarabu wao haujabadilika.

Juzi Jumapili nilienda Uwanja wa Taifa kutazama mechi ya Simba na Ndanda. Nikapokewa na Polisi wenyewe hasira. Wana silaha kali za kivita. Wana Mbwa mwenye hasira. Wanasukuma mstari wa watu wanaotaka kuingia uwanjani. Ni virugu tupu.

Uwanja wa Taifa unaweza kuwa na tiketi yako na bado ukaambulia virungu vikali kichwani. Kuona mpira sio starehe pale Taifa. Ni vita na vurugu. Tunalalamika kwamba watu wamepotea uwanjani kwa sababu ya televisheni. Sio kweli. Watu wastaarabu wamegoma kuja uwanjani. Wanawake wamegoma kuja uwanjani kwa sababu hawana ubavu. Wanaozipenda sana familia zao kiasi kwamba hawawezi kwenda uwanjani bila ya familia nao wamegoma kwenda uwanjani.

Advertisement

Kwanini wafanye hivyo wakati wanaweza kutazama mechi katika Televisheni wakiwa majumbani mwao? Wengi wameachana na ujinga huo na wameamua kulipia ving’amuzi tu.

Ukiwauliza mabosi kwanini kunakuwa na vurugu kubwa wakati wa kuingia uwanjani utaambiwa mashabiki wanapenda kuingia uwanjani muda mchache kabla ya mechi ya kuanza. Najiuliza, kwanini wasifanye hivyo? Kuna starehe gani za kuingia uwanjani mapema pale Uwanja wa Taifa?

Ndani ya Uwanja wa Taifa hakuna baa, hakuna sehemu za chakula, hakuna starehe yoyote nzuri ambayo inaweza kukufanya uingie uwanjani mapema na kusubiri timu zipashe misuli yao moto. Unakwenda uwanjani na kutazama nyasi kwa muda mrefu.

Kwa wenzetu mashabiki hawaendi kulewa katika baa za jirani. Wenye njaa hawaendi kula katika hoteli za nje. Wanakula mle mle uwanjani. Watu wana tenda za vyakula na vinywaji ambavyo vinauzwa katika glasi za plastiki.

Katika mechi kubwa na ndogo, uwanja unapaswa kuingiza pesa kubwa za mauzo ya vinywaji na chakula kuliko zile baa za nje. Hilo halifanyiki na matokeo yake mashabiki wengi wanakaa nje kwa muda mrefu mpaka mechi inapokaribia. Hauwezi kuwalaumu sana. kuna watu wanakuja na watoto wasioweza kuhimili njaa kwa muda mrefu.

Kama utaratibu wa kuingia uwanjani na kutazama mechi ungekuwa mzuri basi watu wengi wangependa kwenda uwanjani kushuhudia mechi ikichezwa mbele ya mboni za macho yao. Lakini kwa Tanzania soka sio starehe. Unaweza kulipa tiketi ya VIP ukaishia kukaa mzunguko. Ukiuliza unaambia siti za VIP zimejaa.

Mechi ya Taifa Stars na Uganda kuna mashabiki wengi walikuwa na tiketi lakini wakaishia kupigwa mabomu katika mageti. Unadhani mtu aliyelipia tiketi yake kwa pesa nyingi baada ya kujinyima kisha akaishia getini anaweza kurudi tena uwanjani? Hawezi.

Tunapolaumu kupotea kwa watu uwanjani tunazungumzia uwepo wa mechi zetu katika televisheni. Mbona Ulaya mashabiki wanajaa na mechi zinakuwa Live katika televisheni? Ni kwa sababu mashabiki wanapata starehe nyingi wakienda uwanjani. Hawana habari ya kupigwa virungu.

Mabosi wetu wa soka kila siku wameshindwa kukabiliana na tatizo hili. Viwanja vya mikoani ni vurugu, uwanja wa taifa ni vurugu. Mtu akijua kuna mechi kubwa anajiandaa kwa vurugu za kuingia uwanjani badala ya kujiandaa kwenda kufurahia dakika tisini za soka na burudani nyingine.

Ukiwa na mgeni wako anayetaka kwenda Uwanja wa Taifa unajiuliza mara mbili mbili kama kuna umuhimu wa kumpeleka. Unaogopa kumuona akihangaika maji ya kufuta macho yake pindi Polisi wakipiga mabomu. Ni kitu kinachosikitisha sana.

Kuna umuhimu wa kuufanya mchezo wa soka starehe. Kuna umuhimu pia wa kuufanya mchezo wa soka kuwa wa kila mmoja wetu. Wanaokwenda uwanjani kwa sasa ni wanaume wenye umri katika ya miaka 20 mpaka 40. Hawa ndio wana nguvu ya kupambana magetini. Tumepoteza mashabiki watoto, wanawake na wazee kwa sababu hawawezi kupambana getini. Hii Bob Marley aliita ‘Struggle for the fittest’.