HASOMEKI:Hali ya cavan bado tete PSG

KATIKA mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Jumanne kati ya PSG dhidi ya Manchester United, mshambuliaji Edson Cavani hakuwepo katika mechi hiyo ambapo timu yake ya PSG iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kama Cavani na Neymar wote wangekuwepo katika mchezo huo wa kwanza wa 16 bora uliochezwa jijini Manchester basi ingekuwa shari zaidi.

Wahenga wa Pwani wanasema heri nusu shari kuliko shari kamili maana kama wangelikuwepo pamoja katika mchezo huo pengine dozi ingekuwa kubwa zaidi kwa Man United.

Pamoja na PSG kuwakosa mastaa hao kutokana na majeraha waliweza kuwahangaisha ‘bwege’ vijana wa Kocha Ole Gunnar Solskjaer wakiwa nyumbani na kuwachapa bila huruma.

Cavani aliungana na Neymar katika bechi la majeruhi wa PSG baada ya mwishoni mwa wiki katika Ligi ya Ufaransa kujijeruhi mwenyewe wakati akipiga penalti iliyowapa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Boedeaux.

PSG imethibitisha mshambuliaji huyo amepata majeraha ya kano ya nyonga ya upande wa kulia lakini mpaka sasa haijaeleweka ukubwa wa majeraha hayo na muda wa kurudi uwanjani.

Kutoeleweka huku kunasababisha sintomfahamu kwani mpaka sasa hakuna taarifa ya kitabibu inayowekwa bayana muda wa Cavani kupona na kurudi uwanjani.

Majeraha haya ndiyo yalimfanya mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Uruguay kutokuwepo katika msafara wa kwenda Manchester na hivyo kukosa mchezo huo.

Majeraha ya kano ya nyonga hujulikana kitabibu kama Hip Tendon injury ndiyo yamempata mshambuliaji huyu mwenye uchu wa mabao akidumu uwanjani kwa kiwango cha juu na kwa kipindi kirefu.

Majeraha haya ambayo yako katika eneo lenye kano za misuli mingi inayounda ungio kubwa la nyonga bado haijawekwa wazi ni msuli upi alioumia.

Sintofahamu hiyo inaongezeka zaidi kutokana na mchezaji husika na klabu kutoweka bayana ukubwa wa majeraha wala bainisho la kano (Tendon) iliyojeruhiwa.

Ingawa kwa jicho la kitabibu kuna taswira inayoonyesha ni jeraha la wastani au la kati kutokana na mchezaji huyo kujijeruhi mwenywe kwa uzito wake wakati alipopiga mkwaji huo wa penalti.

Aliteleza katika mlalo usio rafiki na kumsabaishia kupata majeraha hayo na kumfanya kutolewa nje kipindi cha kwanza dakika 42.

Vilevile bado haijawekwa wazi na jopo la madaktari wa PSG kuwa ni aina gani ya matibabu atakayopatiwa wala haijaelezwa ni tendoni ya msuli gani ambayo imejeruhiwa ni jeraha la daraja gani.

Kwa kawaida majeraha ya kano za mwili huanishwa katika daraja la kwanza, la pili na la tatu.

Kitabibu kano au tendoni kama tulivyozoea ni muishilio wa msuli ulio kama mkia ambao ndiyo unaunganisha msuli kwenye mfupa na huwa ni ngumu sana.

Nyuzi hizi za kano ziko kama kamba za plastiki huwa ni ngumu sana zenye uwezo wa huvutika na kurefuka kiasi ikitokea kiwango cha uvutikaji kimezidi kupita kiwango hukatika au kuchomoka katika mfupa.

Majeraha ya kano hutokea pale moja ya misuli inayosaidia uimara wa ungio hili kuvutika kupita kiwango cha mtanuko wake mara baada ya kwenda mjongeo hasi na kupata shinikizo kubwa.

Wakati Cavani anakwenda kupiga penalti hiyo kwa ustadi mkubwa kwa lengo la kumhadaa kipa ilijipinda sana kiasi cha kuteleza na kwenda uelekeo hasi hali iliyosababisha nyuzi hizo kujivuta sana.

Kano inaweza kutokea kuendana na matukio na ukubwa wa shinikizo la eneo hilo, yanaweza kuwa majeraha ya wastani, ya kati na makubwa.

Lakini majeraha ya wastani ya kano kama yanavyojulikana kitabibu kama ‘strain’ ndiyo ambayo yanatokea mara kwa mara kwa wanamichezo ikiwamo wanasoka.

Mfupa mkubwa wa paja na wa nyonga ndiyo inayotengeneza ungio la nyonga na ndipo ambako misuli mbalimbali ya tumboni, kiunoni, makalioni na mapajani imejikita kutengeneza ungio hili.

Moja ya mambo ambayo yanamweka kwenye hatari mwanamichezo kupata majeraha haya ni pamoja na kuwahi kupata majeraha eneo hilohilo, mkazo wa misuli, kushindwa kupasha vizuri kabla ya mechi na kujaribu kucheza kwa kiwango cha juu sana.

Hapa unaweza kupata picha kuwa hata Edi huenda vihatarishi hivi alikuwa navyo aidha viwili au zaidi ndiyo maana alipoteleza alipata majeraha hayo kirahisi.

Kwa kawaida dalili za majeraha haya ni pamoja na kupata maumivu unapoutumia mguu huo, uvimbe, kushindwa kuutumia ungio la nyonga kufanya kazi yake na eneo hilo kukosa nguvu

Majeraha haya yanaweza kufanyiwa uchunguzi kwa picha ya X-ray ili kuthibitisha kama kuna kuvunjika au kuteguka kwa mifupa ya nyonga na pia kujua ukubwa wa jeraha

Vipimo vya juu zaidi ambavyo ni picha za uchunguzi zinazotoa picha nzuri zaidi kuliko X-ray ni pamoja MRI na CT.

Vipimo hivi vinaweza kuleta bainisho sahihi la aina ya tendoni ambayo Edi amejeruhiwa.

Kwa kawaida misuli ya eneo la nyonga ina umuhimu kwa mwanasoka kucheza na katika matendo mbalimbali ikiwamo kupiga hatua mbele, kutanua mguu kwenda pembeni au kwa ndani, kujizungusha na kuvuta misuli ya paja kwenda nyuma na mbele.

Mambo haya yote ni muhimu kufanyika kwa mwanasoka ili kucheza kwa ufanisi.

Cavani mpaka sasa ameishatupia mabao 22 katika mashindano yote msimu huu inaelezwa kuwa bado yuko katika hatihati ya kutocheza mechi ya marudiano wiki mbili zijazo jijini Paris.

Mshambuliaji huyo kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa timu akiendelea na matibabu ambayo hayajawekwa wazi.

Cavani anaweza kucheza mchezo wa pili kama tu jeraha la tendoni ni la daraja la kwanza kwani aina hii ya jeraha huitaji siku 3-7 kupona.

Tusubiri tuone mwisho wa sintomfahamu hii ya majeraha ya kano ya nyonga yajulikanayo kitabibu kama Hip Tendon injury yaliyompata mshambuliaji huyu ambaye huwa ni chachu ya mabao ya PSG.