Enrique ana zigo la La Roja

Tuesday July 10 2018

 

HABARI ndiyo hiyo, Luis Enrique amepata kazi. Lakini, safari hii ameondoka kwenye presha zile za mechi za kila wiki baada ya kuchaguliwa kuinoa timu ya taifa ya Hispania.

Kocha huyo wa zamani wa Barcelona ataongoza zama mpya za La Roja baada ya kuboronga kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia 2018. Enrique amesaini mkataba wa miaka miwili na kazi yake itakuwa kubwa kurudisha makali ya timu hiyo baada ya kuonekana kiwango kushuka kwa kasi sana wiki za karibuni. Kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, La Roja ilimfuta kazi Julen Lopetegui baada ya kusaini mkataba wa kuinoa Real Madrid siku chache kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya Russia. Fernando Hierro alipewa kazi ya kuinoa timu hiyo kwenye Kombe la Dunia na hakika matokeo yalikuwa ya hovyo.

Alipokuwa na Barcelona, Enrique alibeba mataji ya La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku kwenye timu ya taifa ya Hispania akiwahi kuitumikia kwenye mechi 62 na alicheza fainali tatu za Kombe la Dunia na alibeba medali ya dhahabu kwenye Olimpiki 1992.

Enrique anakuwa kocha wa saba katika kipindi cha miaka 20 kuwa kocha wa timu ya taifa ya Hispania. Kwenye idadi hiyo ya makocha saba ni wawili tu, Luis Aragones na Vicente del Bosque ndio waliowahi kuwapa mataji Hispania. Aragones aliipa Hispania ubingwa wa Euro 2008, kabla ya Del Bosque kuipa timu hiyo ubingwa wa Kombe la Dunia 2010 na Euro 2012.

Makocha wengine waliokuwa na timu hiyo na hawakufanya chochote chenye majaabu ni Jose Antonio Camacho, aliinoa La Roja kuanzia 1998 hadi 2002, ambapo aliongoza timu hiyo kwenye mechi 44 na kushinda 28, huku kikosi chake kikifunga mabao 105. Baada ya hapo, akaja Inaki Saez, aliyedumu na timu hiyo kwa miaka miwili, 2002 hadi 2004 na kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 23 na kushinda 15, huku kikosi chake kikifunga mabao 44 tu. Aragones aliinoa timu hiyo kwa miaka minne, kuanzia 2004 hadi 2008 na kushuhudia michezo 54, huku akiibuka na ushindi kwenye mechi 38, huku kikosi chake kikishinda mabao 101. Akiwa na kikosi chenye mastaa matata kama Xavi na Andres Iniesta wakiwa kwenye ubora wao, Aragones alibeba ubingwa wa Euro 2008.

Kisha ikaja zamu ya kocha wa zamani wa Real Madrid, Del Bosque kuchukua mikoba ya kuinoa Hispania, ambayo alidumu na timu hiyo kwa miaka minane, kuanzia 2008 hadi 2016. Katika kipindi hicho ameiongoza La Roja kwenye mechi 114 na kushinda 87, huku akishuhudia timu yake ikifunga mabao 254. Amebeba Kombe la Dunia 2010 katika fainali zilizofanyika Kusini na Euro 2012, ikiwa ni mataji ambayo Hispania ilibeba mfululizo.

Baada ya kuondoka Del Bosque akaja Julen Lopetegui, ambaye aliinoa timu hiyo kwa miaka miwili, 2016 hadi 2018. Kwa kipindi chake, Hispania ilicheza mechi 20 tu na kushinda 14, huku kikosi chake kikifunga mabao 61. Maisha ya Lopetegui yaliishia siku chache kabla ya fainali za Kombe la Dunia huko Russia, akafutwa kazi na nafasi yake kujazwa na Fernando Hierro, ambaye ameisimamia timu hiyo kwenye mechi nne tu na kushinda moja, huku kikosi chake kikifunga mabao sita pekee. Hierro ameiongoza La Roja kwa wiki chache sana, kabla ya sasa kibarua hicho kukabidhiwa Enrique, ambaye alikuwa hana timu tangu alipoachana na Barcelona mwaka jana.