Dirisha dogo ndio shida zinapoanzia

Friday November 16 2018

 

MUDA wa kucheka na kununa umekwisha wadia, kuanzia tarehe 15/11/2018 hoja nyingi mtaani na mabishano yanayoambatana na utani, kebehi na vijembe vya hapa na pale vitaanza kusikika, kila mmoja akisifia, akijidai na kutamba kutokana na zoezi zima la usajili litakavyokuwa linakwenda. Kwa tafsiri ya moja kwa moja ya matumizi ya fursa hii ya usajili wa dirisha dogo, lengo kuu ni kuzipa timu fursa ya kujiongezea makali ili kuweza kufanikisha malengo yake mara tu msimu huu wa ligi utakapokamilika May mwakani .

Kimsingi hii ni nadharia inayokusudia kuongeza ubora wa ligi kwa kuzifanya timu kutafuta wachezaji zinaowahitaji kulingana na mapungufu na kasoro za kiuchezaji (ufundi na mbinu) zilizojitokeza kwenye mzunguko wa kwanza kiwanjani kwa kuwatathimini mchezaji mmoja mmoja, idara na timu nzima kama kitu kimoja (one unit).

Walimu wote wa Ligi Kuu wakishirikiana vema na wasaidizi wao kwenye benchi la ufundi na viongozi wanalo jukumu moja kubwa na la msingi, kuwasoma na kuwaelewa vizuri wachezaji wao wote kwa lengo la kufahamu uwezo wa kila mchezaji ili hatimaye wafanye uamuzi.

Usajili ni kazi ngumu na nyeti inayohitaji umakini wa hali ya juu, weledi na jicho/ macho ya kiufundi kwa lengo la kupata watu sahihi kwa kazi sahihi, vinginevyo dirisha dogo litageuka kuwa shubiri kwa vingozi na timu nzima kwa ujumla wake.

Dirisha dogo la misimu huu wa 2018/19, linaonyesha kuwa upo uwezekano mkubwa tukashuhudia mambo mengi ya kushangaza lakini pia maigizo mbalimbali kwa kuzingatia jinsi hali ilivyo kwenye klabu.

Tukiwa tumehitimisha mechi zaidi ya 13 kwa timu nyingi, tayari zimeanza kuibuka taarifa mbalimbali kutoka katika klabu zinazohusu wachezaji wapya kusajiliwa na wengine wa zamani kuachwa kutokana na madai au sababu tofauti tofauti. Kwa ligi yetu, hili ni jambo la kawaida kutokea mambo haya, ingawa lazima tukubali kwamba bado hatujakaa sawa kwenye eneo hili la utaalamu, kwa sababu hadi leo tunaendelea kusikia mchezaji kasajiliwa na timu zaidi ya moja, au mchezaji hajasaini kwa sababu hajatimiziwa kile walichokubaliana kwenye mkataba.

Wakati mwingine utasikia mchezaji katoweka kambini hajulikani alip au mchezaji X amefichwa sehemu fulani ili akutane na viongozi wamalizane na mambo mengine mengi kama hayo, kwa ujumla kipindi cha usajili katika soka letu kina vituko vingi ambavyo havifanani navyo.

Kwa bahati mbaya sana, msimu huu mambo yamebadilika kidogo, waswahili walisema kila siku siyo Ijumaa, ikiwa na maana kwamba siku zote hazilingani na wala kufanana.

Mazoea na utamaduni uliojengeaka kwa muda mrefu kuhusu udhamini, TFF ilikuwa na jukumu la kutafuta wadhamini kwa ajili kusaidia kupata fedha za kuendesha ligi.

Hali hii imezua sintofahamu kwenye timu zetu kiasi kwamba dalili na viashiria vya timu kukwama na kushindwa kujiendesha zenyewe zimeaza kuonekana mapema na kusababisha misuguano kwenye klabu, shida mbalimbali na morali ya timu kuporomoka.

Hoja au swali kubwa katika mazingira kama haya ni je? Iwapo wakati huo ligi ilipokuwa bado inafadhiliwa misimu mingi iliyopita mambo yalikuwa ni vurugu tupu, na sasa hakuna wafadhili kabisa itakuwaje?

Kwa namna yoyote ile kitendawili hiki hakiwezi kupata wa kukitegua kwa wakati huu, ni dhahiri ladha na mvuto tulioutarajia kuuona kwenye mzunguko wa pili hautakuwepo kwa baadhi ya timu kati ya 20 za Ligi Kuu.

Hali mbaya ya kifedha kwenye timu nyingi hata kabla ya mzungunguko wa kwanza kumalizika ni jawabu la mwisho kwamba ligi imeyumba na maisha ya wachezaji na watendaji ndani ya timu si rafiki, na kwa mantiki hiyo tusitarajie kuona ubora na viwango vya wachezaji tulivyovitarajia ( quality and competent players ).

Kwa desturi ya soka la sasa na hata la wakati huo, thamani ya ligi inatokana na aina ya wachezaji na watendaji wazuri ndani ya timu.

Lakini pia umahiri na weledi wa benchi la ufundi na mwisho wake uhakika wa maisha ndani ya timu iwapo kila kitu kinakwenda kwa mujibu wa mipango iliyowekwa .

Usajili ni chaguo la wengi, hivyo kzi hii inahitaji fikra za kibiashara, kutokana na ukweli kwamba mpira wa sasa ni biashara kubwa, hivyo mtaji wa kila timu kwa maana ya fungu ndiyo utakaokuwa msingi na msaada kwa viongozi kwenda sokoni kutafuta wachezaji wazuri wanaowahitaji. Aidha usajili wetu unatakiwa kutafsiri vizuri kiwango cha mpira tulichofikia kwa sasa.

Nadharia iliyopo kwa sasa duniani na hata hapa nyumbani kwetu ni kwamba mpira ni kazi, sifa ya kazi yoyote ile ni pale tu mfanyakazi anapopata uwezo wa kujikimu kwa kupata mahitaji yake ya msingi ya kila siku yeye binafsi na wanaomtegemea, kwa mantiki hii kukosekana kwa vyanzo mbadala vya pesa za kuendesha klabu ni mwanzo wa kukosa dira ya soka katika timu zetu katika madaraja yote, hali ambayo itazidisha ukosefu wa utulivu kwenye soka na kuwafanya wachezaji kuhangaika na kufikiria kuhama hama kutoka timu moja kwenda nyingine au kukata tamaa kabisa na kuamua kufanya shughuli nyingine tofauti na kucheza mpira.

Kwa timu za Ligi Kuu zitakuwa kwenye hatari ya kushindwa kucheza kama inavyokusudiwa kwa vile wachezaji wanayo mahitaji makubwa zaidi kulingana na daraja walilofikia.

Soka letu halijawa la kulipwa kwa asilimia 100 lakini utaratibu wa sasa wachezaji wanaishi kwa kutegemea mishahara kwa kuwa muda wao mwingi wapo kazini kwenye timu zao.

Imefikia mahali ambapo suala la madai ya mishahara na posho za wachezaji siyo siri tena kwa vile limekuwa ni kubwa na linazihusu karibia timu zote, ukiziondoa chache ambazo zinaonekana kuwa na uchumi uliotengamaa kwa kiasi fulani kama vile Azam, Simba na hizi za taasisi za umma na mashirika kama vile Mtibwa na Kagera Sugarpamoja na timu za majeshi.

Tofauti ya uwezo kifedha kati ya timu na timu, italeta madhara ya aina mbali mbali, moja kubwa ni suala la wachezaji kuzibagua timu,pili kukubali kusajiliwa katika timu fulani kwa kuwa ina pesa bila kujitathimini viwango vyao kama vinastahili kuingia mkataba na timu hiyo hususani kwenye timu za Simba, Yanga na Azam, tatu timu zisizokuwa na uwezo kifedha zina hatari ya kuwakosa wachezaji wazuri zinaowahitaji, lakini pia hatima yake viwango vya wachezaji vitadumaa kwa kuwa hawachezi mara kwa mara katika ubora unaotakiwa , hii ni hatari kwa mustakabali wa vipaji vyetu.

Katika kipindi hiki kigumu cha timu kushindwa kujiendesha, medani ya uongozi na utawala wa soka ni eneo jingine litakaloathirika kwa sababu hakuna rasilimali pesa za kutosha, inawezekana weledi na maarifa vikawepo, watendaji wazuri pia wapo lakini hao wachache wenye uwezo wa kuongoza wakapata hofu ya kubeba dhamana hiyo, kwa kuwa mipango yao mingi mizuri itashindikana kutekelezeka.

Katika utamaduni na zama mpya za kusimamia soka kwa jumla, kuna umuhimu mkubwa wa kujizatiti kikamilifu kwa kujaribu kutafuta kila njia ili kuokoa soka letu.

Kimsingi ubunifu mkubwa wenye kuiweka karibu zaidi elimu ya biashara na masoko katika mpira unahitajika mno kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya soka la Tanzania.

Kwa jumla dirisha hili dogo la usajili, linaweza kuonekana kama dirisha kubwa kwa viongozi kuonja machungu ya kuendesha klabu na zoezi lenyewe la usajili kwa kuwa itabidi watumie nguvu kubwa kuwashawishi wachezaji, na kwa upande mwingine, wachezaji nao kazi haitakuwa nyepesi, kwani kiwango cha pesa kitaongezeka na thamani yao pia.