CLETUS CHAMA: Fundi wa mpira aliyevunja ndoa ya Niyonzima na mashabiki wa Simba

Muktasari:

  • Kama kawaida Mwanaspoti ndio lililofichua ujio wake. Hata siku wachezaji wa Simba walipopimwa afya kwenye Taasisi ya Jakaya Kikwete pale Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alifanyiwa vipimo na majibu yake yalionyesha yupo kamili gado kukimbizana na kina Kelvin Yondani, Andrew Vincent (Yanga), Aggrey Morris (Azam FC) na Yusuf Ndikumana wa KMC.

USAJILI wake ulifanyika dakika za mwisho ikiwa ni saa kadhaa kabla ya Simba kupaa zake Uturuki kuweka kambi ulidhaniwa kuwa ni wa kawaida.

Kama kawaida Mwanaspoti ndio lililofichua ujio wake. Hata siku wachezaji wa Simba walipopimwa afya kwenye Taasisi ya Jakaya Kikwete pale Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alifanyiwa vipimo na majibu yake yalionyesha yupo kamili gado kukimbizana na kina Kelvin Yondani, Andrew Vincent (Yanga), Aggrey Morris (Azam FC) na Yusuf Ndikumana wa KMC.

Lakini kabla ya hapo mashabiki wa Simba walikuwa hawaifahamu shughuli yake kwani, mabosi wao walifanya dili lake kimyakimya. Huyu anaitwa Cletus Chama.

Jamaa ni fundi wa mpira kwani, anafahamu jinsi ya kuuchezea na kubwa zaidi ni uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho. Katika mechi ya kirafiki kati ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana kwenye Tamasha la Simba Day, ndipo mashabiki wa Simba wakaelewa ni kwa nini mabosi wao walifanya usajili wa Chama bila ya makelele mengi.

Chama alicheza dakika zote 90 za mchezo huo ikabainika ni kwa nini mashabiki wa Simba hawana mzuka tena na kiungo wao fundi waliyemnasa kutoka Yanga, Haruna Niyonzima. Mzambia huyo amemuondoa kabisa Niyonzima kwenye mioyo ya mashabiki na viongozi wa Simba kwani, shughuli yake uwanjani sio ya kitoto unaambiwa.

Fundi wa Pasi

Katika mechi moja tu ambayo Chama amecheza huku akiwa amesajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja ameonesha ni fundi wa kupiga pasi kama zinavyotakiwa kwa mastraika wake.

Dhidi ya Asante Kotoko

Alikuwa ikipiga pasi za chini ambazo zilifika mahala husika na hata muda mwingine alikuwa ikipiga pasi ndefu kwa mawinga wa kushoto na kulia.

Umahiri wa kukaba wa viungo wakabaji wa Simba, James Kotei na Jonas Mkude ulimfanya Chama kuonekana fundi zaidi katika eneo hilo kwani, kwenye mchezo huo mashabiki walikuwa wakipagawa kila Chama alipokuwa na mpira.

Chama ni mzuri katika zile pasi za kampa kampa tena ambazo zinaweza kupigwa katika viwanja vichache tu hapa Tanzania kwani, vingi havina maeneo mazuri ya kuchezea na huenda akishindwa kuonekana bora katika hilo.

Pasi za mwisho

Upele ulipata mkunaji katika mechi ya Asante Kotoko, Chama alipiga pasi za mwisho takribani tano ambazo washambuliaji wa Simba walichotakiwa kufanya ni kupasia tu nyavuni kisha kukimbia kwenye kona kushangilia na mashabiki.

Chama amemuonyesha Kocha Patrick Aussems kuwa ana vitu adimu kwenye miguu yake na ambavyo vikitumika vizuri, basi ukikutana na Simba utapigwa bao za kutosha tu kama ataendelea kuwa kwenye kiwango kama cha juzi Jumatano.

Uwezo wa kuachia mipira na kuupitisha kwenye eneo lolote analotaka ili kumfikia mshambuliaji anayemtaka. Hilo litakuwa likiwaumiza sana mabeki wa timu pinzani. Pasi za Chama ni sahihi na zina macho.

Fundi wa kukokota

Ni wazi kabisa kiungo yeyote bora wa ushambuliaji lazima awe na uwezo wa kumiliki mpira ili kuanzisha mashambulizi kwa timu pinzani. Kwa hili Chama utamtaka ubaya kwani analifanya tena kwa ufasaha zaidi. Chama ana uwezo wa kumiliki mpira akianziwa kutoka kwa viungo wakabaji au mabeki na mara chache kupoteza mipira hiyo.

Wakati akipokea mipira, ana uwezo wa kukokota kwa hatua 20 kutoka nyuma na kwenda mbele au kubadili kutoa upande mmoja na kupeleka mwingine.

Kwa chenga pia mbaya

Chama mbali ya uwezo aliokuwa nao wa kumiliki, kukokota na kupiga pasi ana kitu kingine cha ziada kwa kuwa na uwezo wa kupiga chenga.

Katika mechi dhidi ya Kotoko, Chama aliwapiga chenga mabeki na kupiga pasi za maana, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wa Simba jukwaani kupiga kelele tu kila wakati wakishangilia.

Hata hivyo, Kocha Aussems atakuwa na kazi ya kuhakikisha hampi majukumu mengi ya kupiga chenga kwani hilo linaweza kuwa na madhara kwa Chama akikutana na Yondani anaweza kuingia kwenye orodha ya majeruhi.

Kama Pogba tu

Kiungo wa Kifaransa wa Manchester United, Paul Pogba ni bonge la mchezaji lakini, amekuwa akitifuana na kocha wake, Jose Mourinho kila wakati.

Moja ya mzozo wao hutokana na kukataa kubebeshwa majukumu ambayo sio yake uwanjani, kukaba.

Mourinho anamtaka Pogba akabe, achezesha timu na kusukuma mashambulizi mbele jambo ambalo anatakiwa kulifanya kwa wakati mmoja uwanjani.

Hilo, linaweza kuwa tatizo kubwa kwa Chama, ambaye uwezo wake wa kukaba bado unaonekana ni tatizo.

Chama sio mzuri wa kukaba pindi timu inapopoteza mpira na katika mchezo huo, hilo lilionekana wazi kabisa.

Sio fundi wa kupoteza mipira, lakini inapotokea mpira uko chini ya timu pinzani, basi Chama huonekana akikimbiakimbia tu badala ya kusaidia kukaba kama anavyokuwa kwenye kushambulia.

Kwa kile kilichotokea dhidi ya Kotoko, huenda Kocha Aussems akafanya mabadiliko ili kumwezesha Chama kucheza eneo huru kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi.

Msimu mpya haujaanza lakini Chama ameonyesha atakuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Kocha Aussmea na huenda angekuwa mchezaji wa kawaida ama kukaa benchi kama angekuja wakati wa Mfaransa Pierre Lechantre, ambaye ni muumini wa soka la kujilinda zaidi.