CHEKA: Bilionea huyu alinipa fedha nyingi niache ngumi ila...

Muktasari:

  • JANA tulianza sehemu ya kwanza kuyaangazia maisha ya Bondia Francis Cheka na misukosuko aliyopitia katika maisha yake.
  • Cheka alipitia maisha magumu ya kuishi na mama wa kambo na akaingia katika kazi ya kuzoa takataka. Huku alikutana na misukosuko kibao. Kisha akaamua kukimbilia Morogoro. Nini kilitokea? Fuatana na Mwandishi wa makala haya IMANI MAKONGORO.

AANZISHA BIASHARA YA KUOKOTA CHUPA

Cheka anasema akiwa Morogoro wakati ule hakukuwa na mtu aliyekuwa akifanya biashara ya chupa za plastiki, hivyo zilikuwa nyingi zikizagaa kama takataka kila sehemu.

“Biashara ya chupa wakati ule ilikuwa imeshamiri zaidi Dar es Salaam tu, hata wakati nazoa takataka katika Manispaa ya Kinondoni, ile ndiyo ilikuwa kazi yetu ya pembeni ambayo tulikuwa tunaifanya, nilipofika Morogoro hakuna aliyekuwa akiifahamu.

“Niliongea na Kocha Comando, akanipa eneo pale nyumbani kwake niwe nakusanyia chupa, niliingia mtaani na kuanza kuziokota chupa mwenyewe,” anasema.

Bondia huyo anasema alikuwa na ratiba ya kuamka kila siku saa 11 alfajiri ambapo alikwenda kwenye kibarua chake cha usafi pale Msamvu stendi kama kawaida na saa 12 asubuhi aliingia mtaani kuanza kuokota chupa za plastiki huku jioni akifanya mazoezi kwa Kocha Comando.

“Nilikusanya chupa hadi zikafika tani tano pale kwa Comando, hakuna aliyekuwa akifahamu umuhimu wa chupa pale Morogoro wakati ule, kuna Mhindi mmoja anaitwa Satia ni mfanyabiashara mkubwa wa chupa za plastiki Dar es Salaam alipata habari zangu akanifuata Morogoro.

“Yule Mhindi alikuja kuwa rafiki yangu mkubwa na ndiye aliyeniuzia mashine ya kusaga chupa ambayo ninanyo hadi leo.

CHEKA NA TAJIRI WA KIHINDI ILIKUWAJE?

Kwanza yule Mhindi alinunua mzigo wote wa chupa tani tano ambao Cheka alikuwa amekusanya, kila kilo alimuizia Sh 500.

“Kwa mara ya kwanza nilipata fedha nyingi ambayo sikuitarajia, yule Mhindi alinipenda na alitaka tufanye kazi ya chupa, tulikwenda naye Dodoma, Singida na Iringa kuangalia soko la chupa za plastiki.

Bondia huyo anasema wakati huo wala hakufikiria kuacha ngumi, kwani tayari alikuwa ameshacheza pambano la kwanza la ngumi za kulipwa dhidi ya Mbwana Ally, Februari 2000, pambano ambalo alilipwa Sh 30,000 kama malipo yake.

“Mhindi alinishawishi niachane na ngumi, lakini nilimkatalia kwani niliona kama mafanikio yangu yako kwenye ngumi, hivyo niliendelea kuokota chupa, lakini sikuacha kucheza ngumi.”

MAISHA YA KUPANGA

Cheka anasema, baada ya kulipwa fedha ya chupa ambayo ilikuwa Sh 2.5 milioni, aliamua kutoka kwa kocha na kuanzisha maisha ya kujitegemea, alitafuta chumba na kwenda kupanga maeneo ya Kilimahewa.

“Ilikuwa ni fedha nyingi mno kwangu kuishika kwa mara moja, Kocha Comando alikuwa kama baba yangu, alinishauri mambo mengi na nilimshirikisha suala la kwenda kupanga, aliliridhia nikatafuta chumba cha bei nafuu, nikalipia kodi ya mwaka nikanunua baadhi ya vitu nikaanza maisha mapya.”

Anasema aliendelea kuwasiliana na yule Mhindia ambaye alikuwa akiitwa Satia ambaye alimtaka aachane na ngumi aingie katika biashara yake ya chupa, lakini Cheka aliendelea kumkatalia.

“Niliendelea kukusanya chupa, lakini nilipanua wigo zaidi ambapo nilitafuta watu wengine wa kunikusanyia na nikawa nanunua chupa kwao. Nilipata mzigo mkubwa na biashara ikalipa.

“Nilinunua kiwanja Kilimahewa ambako nilijenga nyumba ya kawaida sana lakini kwa maisha niliyokuwa nimepitia ile ilikuwa ni hatua kubwa sana kwangu.

“Kwa kuokota chupa mtaani hadi kujenga nyumba kutokana na biashara hiyo, hakuna aliyeamini na hapo ndipo watu wa Morogoro wakastuka na wao kuanza kuifanya biashara hiyo ya kuokota chupa.

USO KWA USO NA KUSAGA

Cheka anasema alicheza mapambao manne mwaka 2000 na mabondia tofauti. Hadi mwaka 2002, Oktoba 8 alipocheza kwa mara ya kwanza na Maneno Oswald aliyekuwa hasimu mkubwa wa Rashid Matumla na kumpiga kwa pointi pambano lilifanyika mkoani Morogoro.

“Baada ya miezi miwili nilifuatwa ili nirudiane na Maneno Dar es Salaam, nakumbuka Oktoba 27, 2002 ndiyo ilikuwa siku ya pambano la marudiano.

“Wakati ule nilikuwa nalipwa elfu 20 kwa pambano na kuna mapambano mengine sikuwa nikilipwa ila nilicheza kwa mapenzi tu, pambano na Maneno la Dar es Salaam nililipwa Sh 30, 000.

“Baada ya pambano, kuna mwandishi anaitwa Majuto Omary (sasa ni Mwandishi wa Citizen) alinifuata akanitambulisha kwa Joseph Kusaga ambaye alikuwepo ukumbini siku hiyo. Kusaga alinisalimia akaniuliza pambano lile nimelipwa Sh ngapi, nikamwambia 30,000.

“Akaniuliza nikikuandalia pambano na Rashid Matumla utakuwa tayari kucheza? Nikamjibu ndiyo sababu napenda ngumi na Matumla wakati ule alikuwa na jina, hivyo bondia ukiambiwa ucheze naye, wala hujivungi.”

Cheka anasema baada ya miezi mitatu, kweli Kusaga aliandaa pambano lile ambalo ndilo lilikuwa pambano lake la kwanza kulipwa fedha nyingi kwenye ngumi.

MATUMLA AFUNGUA MILANGO

Ilikuwa Januari 23, 2003 ambapo Cheka licha ya kupigwa kwa Technical Knock Out (TKO) na Matumla lakini aliingiza kitita cha maana ambacho hakuwahi kukifikiria kupata katika mchezo wa ngumi.

Unataka kujua alilipwa shilingi ngapi? Usikose Gazeti la Mwanaspoti kesho Jumamosi.