HISIA ZANGU : Amunike ana kesi za msingi za kutujibu

Muktasari:

  • Mbwana Samatta alikosekana lakini hauwezi kusema timu haikufunga bao au ilipoteza mechi kwa sababu Samatta hakuwepo.

TULITAKA nini pambano dhidi ya Lesotho juzi? Tulitaka ushindi na tungeweza kuupata. Lesotho sio Cameroon, sio Ghana, sio Nigeria. Lesotho ni Lesotho tu. Nilikuwepo uwanjani na ungeweza kuona mioyo yao ikitembea na hofu wakati Taifa Stars ikimiliki mpira.

Pamoja na Stars ilikuwa ugenini lakini ukweli ni kwamba ilihitaji ushindi. Umiliki wa mpira wa Taifa Stars ulikuwa mzuri. Tatizo nadhani Kocha Emmanuel Amunike ana kesi ya kujibu. Katika mechi hii bado alikuwa na mbinu nyingi za kujihami kuliko kushambulia.

Saimon Msuva na Shaaban Idd Chilunda walijikuta wametengwa na wenzao. Muda mwingi walikuwa wanapigiwa mipira mirefu ya juu. Kwanini? Kwa sababu kulikuwa na shimo kubwa kati yao na viungo. Timu ilikuwa chini zaidi.

Kocha Amunike anawapanga Gadiel Michael na Himid Mao kama mawinga. Lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanaingia kwa ndani na kuubana uwanjani. Timu inakosa moto wake wa kawaida katika kushambulia.

Ndio maana alipotoka Gadiel na kuingia Shiza Kichuya timu ilipata uhai mkubwa upande wa kushoto. Upande wa kulia sikuamini macho yangu kwanini Himid Mao alimaliza mechi. Sio kama alicheza ovyo, hapana, haikuwa siku ya majukumu kama yale kwake.

John Bocco angeweza kuanza katikati halafu Saimon Msuva akacheza kama winga wa kulia, Himid angepumzika. Ni siku ambayo tulihitaji kushinda. Kwanini tusingeweka timu ambayo inashambulia na kujilinda kwa nidhamu? Kama tungekuwa tunacheza dhidi ya Nigeria au Cameroon nadhani mbinu za Amunike zingekuwa mwafaka, lakini hawa walikuwa Lesotho. Tungeweza kufunguka kwa nidhamu na kushinda mechi. Mbinu dhidi ya Uganda ugenini haziwezi kulingana na mbinu dhidi ya Lesotho ugenini. Lesotho wapo katika uzito wetu.

Upande wa kulia alicheza Abdalah Kheri ambaye kiasili ni beki wa kati. Alikuwa hanyumbuliki vema kutokana na umbile lake lilivyo. Alikuwa sio mwepesi kama beki wa pembeni anavyopaswa kuwa. Katika benchi kulikuwa na Hassan Kessy pamoja na Salum Kimenya, miongoni mwa mabeki bora wa pembeni kwa sasa nchini. Kwanini Amunike hakumpanga Kessy?

Upande wa kushoto haukuwa na matatizo sana na walau Ally Sonso alionekana kupiga krosi mbili tatu. Tatizo ni kwamba hata yeye mwenyewe katika timu yake ya Lipuli anacheza kama beki wa kati. Mohamed Hussein Tshabalala ana nafasi katika timu hii.

Alipoingia Feisal Salum ‘Fei Toto’ akabadili kabisa upepo katika eneo la katikati. Kwanini Amunike huwa hampangi kuanzia mwanzo? Haieleweki. Katika pambano la marudiano dhidi ya Cape Verde, Fei aliingia uwanjani na kutamba. Mechi hii alianzia nje tena wakati ni wazi Mudathir Yahaya alionekana kutokuwa mchezoni tangu mwanzo.

Nilimsifu Kocha Amunike kwa mbinu zake hizi katika pambano dhidi ya Uganda lakini hazikuwa mbinu za kutumika katika pambano dhidi ya Lesotho. Wakati mechi ya kwanza tuliiuza kwa kuipeleka Uwanja wa Chamazi huku Lesotho wakicheza soka la kujihami, hii ilikuwa mechi ambayo tuliamua kujikaba wenyewe.

Mbwana Samatta alikosekana lakini hauwezi kusema timu haikufunga bao au ilipoteza mechi kwa sababu Samatta hakuwepo.

Hapana. Tulipoteza mechi kutokana na mbinu zetu wenyewe. Chilunda alionekana kuwa tayari kuziba pengo la Samatta lakini hakupata huduma za kutosha.

Lesotho hawakuwa tishio kwa Stars. Bao walilopata lilitokana na makosa ya kipa Aishi Manula kushindwa kuukamata vema au kuupanchia mbali mpira wa kona. Vinginevyo mabeki wa Stars waliliweka lango lao mbali na hatari kwa muda mwingi wa mchezo. Tatizo lilibakia kuwa muundo wa mashambulizi yetu. Basi.

Kocha alipaswa kujua uzito wa Lesotho kabla ya mechi. Alipaswa kujua ni timu ya aina gani. Sio kila mechi inachezwa kwa mpango mmoja. Tanzania ni wanyonge wa wengi katika soka la Afrika lakini si kina Lesotho na Burundi.

Na sasa tumebakia kupiga hesabu za vidole. Ni kosa kubwa katika soka. Hatuwezi kufuzu kwa kutegemea matokeo ya wengine. Stars ilikuwa na muda wa kuamua hatima yake yenyewe bila ya kutegemea matokeo ya Cape Verde dhidi ya Lesotho katika mechi ya mwisho. Lakini pia mechi yetu ya mwisho ni dhidi ya Uganda iliyofuzu. Wakiamua kucheza kwa roho mbaya ni wazi Watanzania watakuwa na wakati mgumu kufuzu kwa sababu Waganda wanatuzidi uwezo. Mechi ya kufuzu ilikuwa hii dhidi ya Lesotho katika uwanja wowote wa soka duniani. Kocha akaufyata.

Mbaya zaidi mechi dhidi ya Uganda ipo mbali, hatujui morali itakuwaje, hatujui wachezaji watakuwa katika hali gani. Hatima yetu haipo mikononi mwetu tena. Huu ni wakati ambao tulikaribia zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule lakini ni wazi tumejiangusha siye wenyewe.