Akili za Mwaikimba, Babi zinapotuma miguu yao

Muktasari:

  • Wakati Mwaikimba akitikisa kwa ufungaji katika kikosi cha Boma FC, pale Mawenzi Market kuna mkongwe mwingine, Abdi Kassim naye ni moto wa kuotea mbali.

HUKO kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL), yule straika wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Gaudence Mwaikimba anawatesa vilivyo makipa na mabeki wa timu pinzani katika kufumania nyavu.

Akiwa na kikosi cha Boma FC iliyopo kwenye Kundi B la ligi hiyo, Mwaikimba kwa sasa ni miongoni mwa wafungaji bora akiwa amepachika jumla ya mabao manne katika mechi sita walizocheza hadi sasa.

Sawa na straika wa Mawenzi FC, Hassan Mbande, Enock Jiha wa Mlale pamoja na Issah Nelson wa Mbeya Kwanza ambao kila mmoja amefunga idadi hiyo ya mabao wakiwa kwenye vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Kama sikosei, Mwaikimba ambaye alikuwa kipenzi cha aliyewahi kuwa kocha wa Taifa Stars kipindi cha nyuma, Marcio Maximo kwa sasa ana umri usiopungua miaka 35.

Wakati Mwaikimba akitikisa upande wa ufungaji, pale kwenye kikosi cha Mawenzi Market ambacho nacho kinashiriki Ligi Daraja la Kwanza kuna mkongwe mwingine, Abdi Kassim ‘Babi’ naye hashikiki.

Ndiye amekuwa mtambo wa kuzalisha mabao ya timu hiyo ambayo kwa sasa inaongoza Kundi A la ligi hiyo ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza michezo sita dhidi ya timu za Mufindi United, Mbeya Kwanza, Dar City, Kiluvya United, Njombe Mji na Mlale FC.

Unaweza kujiuliza kuna siri gani iliyojificha nyuma ya pazia ambayo inawafanya, Abdi Kassim na Mwaikimba leo hii watambe kwenye Ligi Daraja la Kwanza licha ya umri wao mkubwa ambao unawafanya waonekane wazee na kumbe bado wana vitu vya kujivunia kwenye soka wanaloonyesha.

Ni jibu rahisi tu Mwaikimba na Abdi Kassim wamejitunza vyema na wamejiepusha na tabia pamoja na mienendo ambayo ingeweza kuathiri vipaji vyao kama ilivyotokea kwa baadhi ya wenzao ambao leo hii wameshaachana na soka.

Wanafanya vizuri ndani ya kwa sababu hawana presha kubwa na wanacheza kwa uhuru mkubwa kwani jukumu lao ni kuwapa uzoefu vijana waliopo kwenye timu zao kutokana na wasifu wao kwenye mpira wa miguu hapa nchini. Wamejigundua hawawezi kushindana na vijana wadogo ambao damu zao bado zinachemka hivyo wameamua kutumia zaidi akili zao ndani ya uwanja badala ya matumizi ya nguvu ambayo kwa umri wao wasingeweza kumudu kwenye ligi hiyo.