AH! Ndumba zimemaliza vipaji tu

Friday December 7 2018

 

WAKATI dunia ikiwa imetawaliwa na akili zinazokimbia kuona kesho kutakuwa na kitu gani kipya, kama hatua ya kuendelea kuyatafsiri mazingira yetu kuyafanya mazingira kuwa rafiki kwa njia za kisayansi zinazoweza kutupatia majibu ya wazi na yanayopimika kuhusu jambo fulani kuwezekana au kutowezekana.

Inasikitisha kuona bado kuna watu wa michezo wanaowaza kupata mafanikio kwa kuamini mila na utamaduni zinazokumbatia ushirikina.

Michezo kama inavyoonekana kwenye macho ya kila mmoja mpenda michezo na asiyeipenda, unaweza kuitafsiri kwa lugha rahisi, ni kitendo kinachomhitaji mtu kufanya mijongeo mingi mbalimbali akitumia viungo vyake vya mwili kwenye eneo maalumu ama nafasi maalumu akiwa anahitaji pia kutumia nguvu nyingi au kidogo ili kukamilisha mahitaji ya msingi ya mchezo husika.

Zipo faida lukuki katika tasnia hii, ndiyo maana kwa sasa michezo ni kazi.

Wadau na wapenzi wa soka hapa nyumbani umefika wakati tunalazimika kubadilika kifikra na kimtizamo kuhusu imani za kutegemea nguvu za giza ili tupate mafanikio kwenye mpira wa miguu.

Haya ni mambo ya kusadikika tu lakini hakuna taifa lolote duniani lililofanikiwa na kupiga hatua kubwa kwenye soka kwa kupitia njia hiyo.

Vitabu vyote na majarida makubwa ya kimataifa yanazungumzia mabadiliko na maendeleo ya mchezo huu unaopendwa duniani yamekuja na yatazidi kupatikana kutokana na kufanya mambo kwa njia za kisayansi na kitaalamu na siyo kwa kuamini ushirikina.

Hii ndiyo sababu hata hapa nyumbani kila mwaka klabu zetu na timu za taifa zinatafuta wataalamu wa kutoka nje kwa ajili ya kupata weledi wao ili watusaidie kuendeleza soka letu na hivyo kututoa hapa tulipo.

Mara nyingi kwenye soka letu hususan katika klabu, sauti na minongono, imekuwa ikisikika watu wakitoa shutuma na lawama kuhusu timu zetu kuonyesha vitendo vinavyoashiria imani potofu za kuamini ushirikina michezoni.

Huu ni utamaduni mbovu kwa sababu haujawahi kutusaidia kupiga hatua ya maendeleo katika soka.

Ni jambo la kufurahisha na kutia moyo tangu zama za FAT na sasa TFF wameendelea kusimamia jambo hili na kuchukua hatua stahiki dhidi ya timu, kikundi au mtu inapobainika kuna vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina kwenye viwanja vyetu wakati wa michuano ya ligi au mashindano yoyote yale, ingawaje licha ya juhudi zote hizo bado mambo haya yapo na tunayashuhudia.

Haifurahishi na wala haipendezi kusikia baadhi ya watu, wadau au mashabiki waliopewa dhamana ya kusimamia timu wanahangaika na kutumia muda mwingi, fedha kutafuta ushindi kwa njia za mkato na kulazimika kuunda kamati maalumu inayoitwa ya ‘ufundi’ mahususi kwa ajili hiyo ya ushirikina.

Inawezekana hizi ni imani za watu wachache, lakini kwa nini wanapewa nafasi kwenye timu na kuendelea kushiriki katika mambo yasiyo na tija kwenye soka? Ni fedhea na ni aibu kwa nchi na mchezo wenyewe.

Ni mara nyingi kwenye ligi ya Tanzania kusikia timu fulani imekataa kupitia kwenye mlango unastahili wakati wa kuingia uwanjani.

Badala yake wachezaji wameruka ukuta au kupitia mahali ambapo siyo rasmi kwa mujibu wa wenye mamlaka na kiwanja husika walivyopanga. Au kuegesha gari la wachezaji sehemu isiyo stahili ili wateremke na mengine mengi.

Haya ni mambo ya ajabu na ya hovyo kwenye soka letu. Kimsingi hata viongozi wenye jukumu la kusimamia taratibu na mipango yote wakati wa michezo wanapata wakati mgumu kusimamia kwa weledi kazi zao. Mwisho wake ni kuibua fujo na vurugu zisizokuwa na maana wala faida kwa yeyote.

Lazima jamii ibadilike ili iuone ukweli wa taaluma katika kuupeleka mpira mbele.

Wakati kiwango cha soka hapa nchini kikiwa bado ni cha kusuasua, wiki iliyopita kilitokea kihoja kingine kwenye pambano la Ligi Kuu, miongoni mwa vioja vingi vinavoashiria bado tuna tatizo kubwa la kuamini ushirikina katika soka.

Kwenye mchezo kati ya Simba na Lipuli uliofanyika Uwanja Mkuu wa Taifa, mara baada ya kukamilika kwa dakika 45 za kwanza, kama kawida timu zote na waamuzi walitakiwa kuelekea ndani kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na hii ni kanuni popote pale duniani.

Kwa mshangao wa kila aliyekuwepo uwanjani, wachezaji wawili mmoja kutoka Simba na Lipuli hawakuwa sehemu ya vikosi vyao vilivyoelekea vyumbani, haikueleweka mara moja lengo lao lilikuwa ni nini.

Hali hiyo ilidumu kwa zaidi ya dakika tano wakiwa wanaviziana mmoja wao atangulie kutoka kiwanjani na kuwafuata wenzake kule ndani.

Hakika halikuwa tukio la kawaida na lililozoeleka, kitendo hicho kilisababisha minongono na mawazo ya wapenzi wa soka waliohudhuria kukihusisha na imani za kishirikina.

Katika mazingira ya kawaida ni rahisi kuona ni jambo la kawaida, lakini lazima TFF na Bodi ya Ligi wajipange upya kupiga vita kwa nguvu zao zote tabia za namna hii.

Jamii yetu haiko nyuma kiasi hicho na si kama hatuna ustaarabu, bila woga wala aibu wachezaji tena wa Ligi Kuu wanafanya vitendo hivyo hadharani. Nini kitatokea kwenye timu za madaraja ya chini?

Lakini wachezaji wadogo wanaoibukia wanajifunza nini kutoka kwa kaka zao? Bahati mbaya wakati tukio hili na mengine yanayotokea kwenye viwanja vingine nchini wapo vijana wadogo wenye jukumu la kuokota mipira (ball boys), jamii lazima ijiulize hawa watoto wanajifunza nini?

Kwa sababu wengi wao wanatamani kuwa wachezaji wakubwa baadaye. Ni wazi tayari wanaanza kupandikizwa mawazo yasiyokubalika katika fani ya michezo.

Lazima tufike mahali tujiulize kwa kila mmoja katika umri wake alionao, tangu ameanza kusikia au kuyaona mauzauza haya kwenye mpira, timu zetu zimefanikiwa kiasi gani, zimecheza nusu fainali au fainali ngapi katika mashindano yoyote ya Caf au Fifa?

Kama hiyo haitoshi tumefanikiwa kutwaa mataji mangapi makubwa ya kimataifa?

Lakini pia hata ukiangalia namna timu zetu zinavyopata ugumu kufuzu kwenye michuano mikubwa ni kasheshe, hiyo inatosha kabisa kutuonesha kuwa wakati wa kupoteza muda kwenye imani za ushirikina umekwisha.

Kwani pasipo kufanya mapinduzi ya kweli katika akili zetu na tukawekeza zaidi kwenye utaalamu au kusoma vizuri masuala ya michezo na tukakubali kuwatumia wataalamu wetu.

Safari yetu bado itaendelea kuwa ndefu kuyafikia mafanikio halisi.

Tumechelewa kufika pale tunapostahili, mambo mengine yanayotuathiri siyo magumu sana kuachana nayo isipokuwa kuna kila sababu ya kuweka nia zetu ili kuyaondoa, kwani hata juhudi za kupata wachezaji wa kwenda kucheza soka la kulipwa nje zitashindikana licha ya wachezaji wetu kuwa na vipaji vikubwa.

Kikwazo kimojawapo ni kuwajengea imani bila utamaduni huu katika soka mchezaji hawezi kupata mafanikio.