TFF/ TPLB wakati mwingine mnapenda kubebeshwa mizigo ya ajabu ya lawama

Sunday May 26 2019

 

HUENDA mashabiki wengi wa soka hawana habari, lakini ukweli ni kwamba jana asubuhi imechezwa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya JKT Tanzania na wageni wao Kagera Sugar.

Mechi hiyo ambayo ratiba ilionyesha ilipaswa kuchezwa Alhamisi jioni, lakini ikapigwa danadana kabla ya kuchezwa jana saa 2 asubuhi katika Uwanja wa JMK Youth Park, Kidongo Chekundu, jijini Dar es Salaam.

Ni mara ya kwanza kwa uwanja huo kutumiwa kwa mechi ya Ligi Kuu Bara na haikuwahi kufikiriwa kama ungeweza kutumiwa kwa mchezo wa ligi.

JKT inafahamika inatumia Uwanja wa Isamuhyo kama wake wa nyumbani, lakini kwa kilichoelezwa mvua kuuharibu uwanja huo, ghafla mechi ikaangukia JMK na mchezo kupigwa asubuhi. Imeshangaza kidogo mechi kupigwa asubuhi, pia imeshangaza zaidi kupangwa Uwanja wa JMK.

Inashangaza kwa kurejea ukweli Uwanja wa JMK haujawahi kuhusishwa kwa mechi yoyote ya Ligi Kuu na wala Daraja la Kwanza na kama kweli Uwanja wa Isamuhyo ulitibuliwa na mvua, bado mechi hiyo huenda ingepelekwa Azam Complex ambao umezoeleka kuchezwa mechi za ligi. Hata kama uwanja huo umeshindikana kupatikana (jambo ambalo bado hatuliamini kwani hauna ratiba yoyote hata ile ya Ligi ya U20), bado ni vipi mechi imepigwa asubuhi huku mashabiki wakiwa hawana habari na mchezo huo?

Kadhalika kama Bodi ya Ligi ilikuwa inafahamu mechi inaenda kuchezwa JMK na kurushwa na Azam Tv, lakini ni wachache waliokuwa wanajua kama unarushwa hewani ili hata kama kuna ujanja ujanja umepangwa kufanyika kwenye mechi hiyo iwe rahisi kuonekana hadharani. Tunalisema hili kwa kurejea mkasa wa msimu uliopita wa mchezo ulioleta utata kiasi cha Simba kuamua kukimbilia FIFA kudai alama tatu dhidi ya Kagera Sugar.

Mechi ya Kagera dhidi ya Simba katika msimu huo, iliibua utata juu ya tuhuma za beki Mohammed Fakhi kudaiwa kuonyeshwa kadi ya njano kwenye mchezo wa timu yake ya Kagera dhidi ya African Lyon ambao haukuonyeshwa hewani.

Mzozo huo ulikolezwa zaidi baada ya ripoti ya mwamuzi wa mchezo huo na ile ya kamisaa kukinzana na mwisho pointi ambazo Kagera ilikuwa imenyang’anywa awali na Kamati ya Saa 72 kurudishwa kwao na Simba kuamua kukimbilia FIFA bila mafanikio.

Kwa nini tunaizungumzia mechi hii na kurejea tukio la mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya African Lyon uliochezwa kinyemela bila hata kufahamika kwa mashabiki wengi wala kituo cha Azam wanaorusha matangazo ya Ligi Kuu kutourekodi, ni kwa vile ligi ya msimu huu kwa sasa imebaki kwenye vita ya timu za kushuka daraja.

Bingwa wa msimu huu tayari ameshapatikana mapema kwa Simba kutetea taji lake na jana Jumamosi, wababe hao walikabidhiwa rasmi, huku nafasi ya pili hadi ya tano nazo ni kama zimeshafahamika kama ilivyo kwa African Lyon iliyotangulia Ligi Daraja la Kwanza.

Kabla ya mchezo huo wa jana, JKT walikuwa kwenye nafasi ya 19 katika msimamo, ikiwa sawa na Mwadui, huku Kagera ikiwa nafasi ya 16 na zote zikiwa kwenye janga la kushuka daraja kuifuata Lyon ama kujiweka kwenye hatari ya kucheza play-off. Hivyo mchezo huo wa jana ulikuwa muhimu kwa timu zote katika dakika 90 na hata kama limetokea la kutokea basi ushahidi uwe rahisi kupatikana kwa mashabiki wengi kulishuhudia pambano hilo.

Iwapo mechi imeisha salama bila mizengwe itakuwa jambo jema kwani haitaleta tatizo, lakini kama kuna jambo ambalo linaweza kulalamikiwa, isije ikatibua ligi hii inayotarajiwa kumalizika Jumanne kabla ya kucheza Fainali ya Kombe la FA Jumamosi.

Ieleweke hatuishutumu timu yoyote wala kumlaumu mtu, ila kwa kutaka ligi imalizike bila lawama na dosari ndio maana tunahoji hivyo kwa sababu tuliona sakata la Fakhi lilivyoitia doa TFF na Bodi ya Ligi na hata Kamati ya Saa 72 kutokana na kushindwa kuwepo kumbukumbu ya mchezo wa Lyon na Kagera Sugar. Halafu katika dunia ya sasa, wasimamizi wa ligi wanapaswa kujipanga mapema pale inapotokea tatizo mechi kushindwa kufanyika ndani ya tarehe ya ratiba kama ilivyojitokeza mechi ya jana kwa nia ya kuondoa utata.

Kwa mfano kwa sasa ratiba inaonyesha Ligi Kuu inamalizika keshokutwa Jumanne, huku jiji la Mbeya timu zake zote za Tanzania Prisons na Mbeya City zinamalizia nyumbani hivyo ni lazima ipangwe mapema uwanja wa mechi mojawapo itachezwa wapi. TFF na TPLB wanapaswa kuwa makini hasa na mechi kama hizi za lala salama ili kuepuka kuangushiwa mzigo wa lawama kwa mambo yenye utata kama ya mechi hiyo kuhamishiwa JMK ana kuahirishwa kwa shangwe za Simba jana Taifa.