Vichwa sita vinavyotoana jasho tuzo ya England

Sunday April 21 2019

 

LONDON, ENGLAND. ORODHA ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa kulipwa kwenye Ligi Kuu England imeshawekwa hadharani, huku kinyang’anyiro hicho kikienda kuwaingiza vitani wachezaji sita.

Virgil van Dijk, Eden Hazard na Raheem Sterling watachuana jino kwa jino na wakali Sadio Mane, Bernardo Silva na Sergio Aguero katika kuisaidia tuzo hiyo inayotolewa na Chama cha Wachezaji wa kulipwa wa Ligi Kuu England.

Mabingwa watetezi Manchester City imeingiza wachezaji watatu kwenye orodha hiyo, huku wawili wakitokea kwenye kikosi cha Liverpool kinachochuana kusaka taji lao la kwanza la Ligi Kuu England huku Chelsea ikiwa na staa mmoja, Hazard.

Kwenye orodha hiyo hakuna mchezaji yeyote kutoka kwenye vikosi vya Manchester United, Arsenal na Tottenham Hotspurs na hivyo kufanya kuwa vita ya timu tatu tu, huku mbili Man City na Liverpool zikitajwa kuwa kwenye vita ya kali.

Staa wa Liverpool, Mohamed Salah aliyeshinda tuzo hiyo msimu uliopita hayumo, wakati Sterling, aliyebeba tuzo hiyo kwa wachezaji vijana, anapewa nafasi kubwa ya kutamba msimu huu.

Wachezaji wengine watakaochuana kwenye tuzo ya vijana, inawahusu pia wakali Marcus Rashford wa Man United, Trent Alexander-Arnold wa Liverpool na kiungo wa West Ham United, Declan Rice sambamba na kiungo mwingine wa Bournemouth, David Brooks.

Advertisement

Katika kipengele cha wachezaji vijana, wanaopaswa kuwania ni wale wenye umri wa miaka 23 kushika chini kwa wakati msimu utakapokuwa unaanza. Yote kwa yote hii hapa orodha ya wachezaji sita wanaowania tuzo hiyo ya mchezaji bora wa kulipwa wa mwaka huu kwenye Ligi Kuu England.

Raheem Sterling

Fowadi wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Raheem Sterling amekuwa kwenye kiwango bora kabisa akifunga mabao 23 katika michuano yote. Ni rekodi nzuri kabisa kwa upande wake katika kufunga mabao huku huduma yake ikiwa kitu muhimu kwa kocha Pep Guardiola katika kusaka mataji ya kikosi hicho, ambapo kwa sasa wanachuana kupambana kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu England.

Sterling amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha Man City katika harakati zao za kubeba mataji matatu ya michuano ya ndani ya England, baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Tottenham Hotspur Jumatano iliyopita.

Unafahamu? Sterling amehusika kwenye mabao 36 kwenye michuano yote msimu huu, akifunga mara 23 na kuasisti mara 13 na hivyo kuwa mchezaji muhimu kabisa huko Etihad.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 45

Mabao: 23

Asisti: 13

Sergio Aguero

Straika wa Kiargentina, Sergio Aguero ameendelea kuonyesha kwamba, yeye ni kiboko kwelikweli linapokuja suala la kutamba kwenye Ligi Kuu England na ndio maana Manchester City muda wote wamekuwa kwenye ubora wao kwenye michuano hiyo wakipambana kutetea ubingwa wao. Staa huyo alikuwamo kwenye kikosi bora cha msimu wa 2017-18, huku akiendelea kuonyesha ubora mkubwa kwa kufunga mabao 30 ya michuano yote mara tano katika misimu minane.

Mabao yake 17 kwa msimu huu amefunga kuanzia Januari huku akiwa na mabao 19 kwenye Ligi Kuu England na kufanya achuane na Mohamed Salah jino kwa jino kwenye kuwania Kiatu cha Dhahabu licha ya kwamba, amecheza kwa dakika 900 pungufu ya zile alizocheza staa huyo wa Liverpool.

Unafahamu? Aguero amefunnga mabao 30 katika michuano yote msimu huu na hiyo linamfanya kuwa mchezaji aliyefunga mara nyingi zaidi kuliko yeyote.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 41

Mabao: 30

Asisti: 9

Virgil van Dijk

Usajili wa beki wa kati Virgil Van Dijk kwa Pauni 75 milioni Januari mwaka jana umewafanya Liverpool kuwa kwenye mikono salama na hivyo kuwafanya kushika nafasi za juu kwenye Ligi Kuu England kutokana na kuwa na ulinzi mkali. Mdachi huyo amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha Anfield, ambapo katika mechi 17 kati ya 34 alizocheza kwenye ligi, Liverpool haijaruhusu bao.

Kitu kingine kinachomfanya Van Dijk kuwa mchezaji bora kabisa kwa msimu huu ameisaidia Liverpool kuruhusu mabao 15 pungufu ukilinganisha na msimu uliopita ilivyokuwa walipocheza idadi kama hiyo ya mechi. Liverpool wanachuana jino kwa jino na Man City kwenye mbio ya ubingwa, shukrani kwa huduma bora ya Van Dijk.

Unafahamu? Van Dijk ameibuka mshindi kwenye ushindani wote wa ana kwa ana na mshambuliaji akishinda mara 25 katika matukio ya aina hiyo kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 43

Kutofungwa: 22

Mabao: 5

Sadio Mane

Fowadi wa Kisenegali, Sadio Mane alikuwako kwenye timu bora ya msimu ya wachezaji wa kulipwa kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2016-17 na tangu hapo amekuwa akicheza soka lake kwa kiwango cha juu sana. Kuzipa mateso safu za mabeki za timu pinzani ndicho kitu anachokiweza zaidi Mane hasa anapokuwa na washambuliaji wenzake huko kwenye kikosi cha Liverpool, Mohamed Salah na Roberto Firmino.

Kwa msimu huu, Mane amefunga mabao 22 katika michuano hiyo na kuonyesha ubora wake mkubwa ndani ya uwanja jambo linalowafanya Liverpool kuwa na wakati mzuri. Staa huyo amekuwa na ubora mkubwa wa kufunga kwenye mechi kubwa ambapo alifunga mara mbili katika hatua ya 16 bora wakati Liverpool ilipowatupa nje Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Unafahamu? Ni Steven Gerrard pekee ndiye aliyefunga mabao mengi kwenye michuano ya Ulaya akiwa na Liverpool kuzidi Mane. Nahodha huyo wa zamni wa Anfield amefunga mara 21, wakati Mane amefunga 14.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 43

Mabao: 22

Asisti: 5

Bernardo Silva

Kufuatia kutokuwapo kwa Kevin de Bruyne, Mreno Bernardo Silva akajitengeneza vyema kwenye kikosi cha Manchester City na kukamatia sehemu ya kiungo iliyofanya timu hiyo ya Etihad kutamba. Ikiwa ni msimu wake wa pili kwenye kikosi hicho tangu alipojiunga akitokea Monaco kwa ada ya Pauni 43 milioni mwaka 2017, Silva ameanzishwa katika mechi 31 za ligi, ikiwa nyingi kwa karibu mara mbili kutokana na zile alizocheza katika msimu wa 2017-18.

Mechi nyingi alizocheza msimu huu amekuwa akitamba kwenye kiungo ya kati ambapo alitengeneza kombinesheni moto sambamba na David Silva na Mbrazili, Fernandinho.

Unafahamu? Silva amehusika kwenye mabao 23 katika mechi 45 alizocheza kwenye michuano yote akiwa na Man City msimu huu, amefunga 12 na kuasisti 11, ikiwamo ni mabao manne zaidi ya yale aliyofunga msimu uliopita katika mechi 53.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 45

Mabao: 12

Asisti: 12

Eden Hazard

Wakati kukiwa na tetesi nyingi za kuhusu kuhama tangu Eden Hazard aliposaidia Ubelgiji kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 huko Russia, staa huyo alituliza daluga zake na kuendelea kucheza soka la kiwango bora kabisa kwenye kikosi cha Chelsea.

Kocha Maurizio Sarri amekuwa kwenye kipindi kigumu kwa msimu wote kutokana na maneno yaliyokuwa yakiendelea kuhusu mchezaji huyo kuhusishwa na Real Madrid. Hazard hakuteteleka na kuendelea kucheza soka la juu linalomfanya kuwamo kwenye vita ya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa kulipwa wa mwaka kwenye Ligi Kuu England.

Unafahamu? Hazard amehusika kwenye mabao 28 katika Ligi Kuu England msimu huu, akifunga mara 16 na kuasisti mengine 12. Katika mchezaji mwingine aliyefanya hivyo.

Rekodi zake msimu huu

Mechi: 44

Mabao: 19

Asisti: 12