MKWABI: Mbona mwarabu kafa, acheni kuichafua Simba

JANA Jumamosi tulianza mfululizo wa makala iliyotokana na mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi ambaye kwa kuanza aliweka bayana hatma ya nyota wa klabu hiyo wanaomaliza mikataba yao pale klabuni Msimbazi.

Pia, alifichua ishu za mechi za viporo kwa timu yake na suala zima la usajili wa kikosi cha Simba na katika muendelezo wa makala hizo leo Jumapili, Mkwabi anaanika namna fedha walizovuna kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu zilivyowapa mzuka kinoma wa kupambana.

Simba haikuwa imeshiriki ligi hiyo tangu mwaka 2013, pia haikuwahi kufika hatua ya makundi tangu walivyofanya hivyo mwaka 2003, lakini Mkwabi anasema kwa kufuzu robo fainali kumewafanya wafikirie upya na kujipanga vyema ili msimu ujao wakishiriki tena mambo yawe bambam...Kivipi? Endelea naye...!

FEDHA ZA CAF

Kabla ya mabadiliko hayo, fedha zote za Simba zilizopatikana ziwe kwa viingilio vya mlangoni wakati wa mechi, wadhamini mbalimbali, mauzo ya bidhaa zao, majengo na rasilimali watu kwa maana ya michango ya wanachama zilisimamiwa na kuamuliwa na Kamati ya Utendaji iliyokuwa inaongozwa na Rais/ Mwenyekiti.

Mkwabi anafafanua juu ya masuala ya fedha yalivyo kwa sasa baada ya mabadiliko hayo;

“Kutokana na mfumo wetu wa sasa, mimi kama Mwenyekiti siruhusiwi kuzungumzia suala lolote linalohusiana na mambo ya fedha ama mengine ambayo yapo chini ya Bodi ya Wakurugenzi, jukumu hilo lipo chini ya CEO Magori (Ofisa Mtendaji Mkuu) maana ndiye kiongozi anayehusika na masuala yote kwa mujibu wa taratibu zetu.

“Lakini niseme tu kwamba, bodi ya wakurugenzi itakutana hivi karibuni ambapo masuala yote yanayohusu fedha na mengine yatazungumzwa na wanachama wa Simba wataelewa nini kinaendelea.

“Nafahamu wanachama wanatamani kujua nini kinaendelea ndani ya Simba ila wavumilie utaratibu upo unaofuatwa, hata ningekuwa na mamlaka ya kufanya jambo lolote kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla ya mabadiliko haya napo nisingeweza, kwani bado sijakabidhiwa nyaraka kutoka uongozi uliopita kujua hiki kikoje na hiki kiko vipi, hivyo bodi inajua inafanya nini kwa manufaa ya klabu yetu.”

MZUKA KIMATAIFA

Hata hivyo, Mkwabi anafichua kuwa malengo ya awali ya Simba yalikuwa ni kufika hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Malengo hayo yalitimia na wamevuka na kuingia hatua ya robo fainali. Ni hatua nzuri kwa Simba ambayo baada ya kutolewa dhidi ya TP Mazembe, mipango yao ya baadaye ni kuingia nusu fainali na fainali zenyewe.

Mkwabi anasema mzuka walioupata wa kufika hatua hiyo ni kubwa na kuamini kama watajipanga vyema wanaweza kufika mbali, muhimu ni kujipanga tu na kutenga bajeti itakayohimili vishindo vya michuano hiyo ya Afrika.

Anasema kwa msimu huu walipoingia kwenye michuano hiyo Simba ilitenga bajeti yao ingawa haikuwa kubwa, huenda hii ilitokana na kutojiamini kwamba watafika mbali ndiyo maana bajeti iliishia kwenye hatua ya makundi.

Simba ilipoingia hatua ya robo fainali ilipewa dola 650,000 zaidi ya Sh 1.5 bilioni ambazo tayari wamelipwa kiasi.

Mkwabi anaeleza; “Bajeti yetu kwenye michuano ile ilikuwa haitoshi, ila tulifanya vizuri na tulilipwa pesa kutoka CAF ambazo zimetusaidia kwenye shughuli za maandalizi ya mechi na mambo mengine.”

Mkwabi hakuweka wazi kiasi cha pesa walicholipwa mpaka sasa na CAF huku akisisitiza kwamba, ni siri ya Bodi ambayo baadaye itaelezea juu ya hilo baada ya kikao chao kijacho, lakini akisisitiza imewafanya kuona umuhimu wa kuelekeza nguvu mechi za kimataifa ili wavune fedha za kutosha.

ISHU ZA UPULIZWAJI SUMU

Simba imelalamikiwa katika mechi dhidi ya AS Vita kwamba ilipulizia dawa yenye sumu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji ili kuwadhoofisha wapinzani, jambo ambalo liliifanya timu hiyo ya DR Congo kugomea kuingia kwenye vyumba na kukaa koridoni huku wachezaji wakiwa wamevaa maski puani ili wasipate madhara.

Baadaye uongozi wa AS Vita ulidai kuiripoti Simba CAF kuhusu tuhuma hizo na Wacongo wenzao TP Mazembe nao walipokuja kucheza dhidi ya Simba mechi ya robo fainali walitoa tahadhari hiyo kwamba, wamepata taarifa juu ya mbinu chafu za Simba.

Mkwabi analezea zaidi; “Watanzania tunakosea sana kwenye mpira, tunaonyesha kutopendana na kutotakiana mema. Hili suala lilianzia kwa Watanzania wenyewe kupeleka taarifa ambazo si za kweli, wao wakaingiwa kwa mambo ambayo hayana ukweli wowote.

“Mara nyingi haya mambo yanaanza kuzungumzwa na timu za ndani kutokana tu na ukaribu waliona na watu wa Congo, huwezi kuzuia mazungumzo kama hayo ila yanapaswa kuwa na ukweli wenye uthibitisho.

“Timu kuja hapa nchini si mara ya kwanza, mbona JS Saoura walikuja, Mbabane Al Ahly kwanini hao wasilalamike ila iwe kwa Wacongo tu, hapo kuna namna kwamba wanalishwa mambo ambayo hayana ukweli wowote.

“AS Vita wamekuja uwanjani wakiwa tayari wamevaa maski nani amewathibitishia hilo, wakati huduma zote tulizokuwa tumewaandalia walikataa, tulisikia hata hotelini walikuwa wanajihudumia wenyewe mambo ya chakula, sasa hizo dawa nani aliwapulizia.

“Soka ni mchezo unaonekana wazi, watu tushindane uwanjani na kila mtu apate matokeo kutokana na kiwango ambacho wachezaji wanakionyesha, tusiharibu sifa za nchi kwa mapenzi na ukaribu na watu wa nje,” alisema Mkwabi

TOFAUTI YA UENDESHAJI

Mkwabi anasema kuna tofauti kubwa ya uendeshaji klabu yao kwa sasa na zamani walipokuwa wanatumia mfumo wa uanachama.

“Zamani timu ilikuwa inaongozwa na Kamati ya Utendaji ambapo Mwenyekiti ndiye alikuwa kiongozi, lakini hivi sasa maamuzi yote yapo chini ya Bodi ya Wakurugenzi na timu inaendeshwa na Mtendaji Mkuu (CEO), hiyo ndiyo tofauti kubwa hivyo hakuna mtu kuamua kufanya jambo lake mwenyewe kulingana na nafasi aliyonayo.

Anasema mfumo huo ndio umekuwa ukitumika kwa klabu kubwa na za kisasa na kupiga hatua kimaendeleo na anaamini hata wao wana muda mfupi wa kuthibitisha kuwa, mfumo huo ni sahihi kwa zama hizi ambazo soka linaendeshwa kama biashara inayolipa na kutajirisha.

Je, unayajua malengo ya Simba? Vipi kuhusu ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mchuano mkali uliopo sasa? Ungana na Mkwabi kesho Jumatatu upate majibu ikiwamo ishu nzima ya udhamini ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Hakikisha unapata nakala yako kuona nini kimewekwa bayana na Mkwabi.