Man United waambiwa mbebeni N’Golo Kante

Sunday April 7 2019

 

MANCHESTER United wameambiwa hivi wasiogope kupeleka ofa Chelsea kwa ajili ya kumsajili kiungo mkata umeme, N’Golo Kante kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Staa wa zamani wa Ligi Kuu England, Robbie Savage alisema anaamini mfumo wa kutumia wachezaji vijana huko Man United unaweza kumshawishi Kante kwenye kujiunga na timu hiyo na kutengeneza rekodi yake bora kabisa ya kwenda kusaka ubingwa mwingine wa Ligi Kuu England.

Kante amebeba taji la Ligi Kuu England mara mbili, akiwa na vikosi vya Leicester City na Chelsea, lakini sasa anaweza kuondoka huko Stamford Bridge kwa sababu kocha Maurizio Sarri hamchezeshi kwenye namba yake anayoimudu vyema na kumtumia Jorginho tangu alipotua Stamford Bridge.

“Kante ameshinda Ligi Kuu England akiwa na Leicester City na Chelsea, nani anasema kwamba hawezi kushawishika kwenda kunyakua medali ya tatu ya ubingwa wa ligi hiyo huko Old Trafford?” alisema Savage. Msimu huu Kante amefunga mabao manne na kuasisti mara nne pia katika mechi 44 alizochezea Chelsea.

Wakati huo huo, imeelezwa kwamba Man United wamefuta mpango wa kumnasa Gareth Bale. Bosi anayefanya usajili huko Old Trafford, Ed Woodward, ameamua kufuta mpango huo baada ya kudai kwamba anataka kusajili mchezaji ambaye atauzika tena, pia hataki kumnasa mchezaji ambaye atakuja kwenye timu na kutaka alipwe mshahara mkubwa.