AMUNIKE: Winga teleza aliyeweka rekodi tamu Taifa Stars

Kocha Emmanuel Amunike.

MASHABIKI waliimba jina lake baada ya filimbi ya mwisho ya mechi ya Tanzania dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 24.

Ilikuwa ni haki yao kupagawa kwa furaha baada ya mechi hiyo waliyoshinda 3-0 dhidi ya The Cranes kwa sababu hapakuwa na kingine zaidi ya ushindi ambacho kingetosha kuwafanya wafuzu kwenda kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.

Dua za Watanzania za kutaka mechi nyingine ya kundi lao baina ya Cape Verde na Lesotho iishe kwa wenyeji Cape Verde kuepuka kichapo, zilijibiwa kwa timu hizo mbili kutoka sare.

Stars ikafuzu kwa mara ya kwanza katika miaka 39 na ya pili jumla tangu fainali za Mataifa ya Afrika zilipoanzishwa 1957.

Hata hivyo, safari ya kufuzu kwenda Misri kwenye fainali hizo zitakazofanyika Juni, haikuwa nyepesi kwa Kocha Emmanuel Amunike.

Mnigeria huyo alikosolewa vikali wakati wa kampeni hizo za kufuzu, huku wengine wakitaka atimuliwe.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na kocha huyo kuzungumzia mipango yake na mambo kibao aliyokutana nayo akikinoa kikosi cha Taifa Stars.

Hotelini kwake ambako Mwanaspoti lilitia nanga lilimkuta nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Zamalek akiendelea kupanga mikakati ya AFCON, pia kuinua soka la vijana na kwa sasa pia anasimamia mazoezi ya timu ya Taifa ya U19.

AVUTIWA NA SOKA LA BONGO

Kutokana na mengi yanayotokea nchini likiwamo la Ligi Kuu kushindwa kumshawishi mdhamini kuwekeza pesa na hivyo ligi hiyo kuelekea ukingoni bila ya kudhaminiwa;

Au pia ligi hiyo ya juu kuwa na baadhi timu zenye viporo vingi kufikia mechi 10 mkononi, inashtua kidogo ukiambiwa soka letu limepiga hatua.

Amunike anaamini soka la Bongo limepiga hatua akisisitiza tangu ametua Tanzania ameona juhudi kubwa za maendeleo ya soka zikifanyika nchini kuanzia katika ngazi ya klabu hadi za taifa.

“Soka ni mchezo wa kuwekeza na nimeona uwekezaji ukifanywa katika kuhakikisha wanapatikana vijana na kuwa na miundominu inayosaidia vijana kukua. Kufuzu kwa Simba katika robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika pia ni kubwa hatua ya kimaendeleo katika soka la hapa,” anasema.

Aliongeza kuwapo na Simba na Yanga kunazidi kulifanya soka la Bongo kuendelea kutokana na timu hizo kuwa na ushindani wa kutosha ukiwagawa mashabiki pande mbili.

“Kuna timu kubwa mbili hapa ambazo zimegawa mashabiki nusu kwa nusu ni jambo kubwa hili. Simba kufuzu kwao kutazidi kuongeza spidi soka la Bongo.

MZUKA TAIFA STARS

Kuna kipindi mashabiki walikuwa na hofu juu ya namna ambavyo kikosi cha Taifa Stars kinavyocheza, wengine wakisema kwamba Stars haichezi soka la kuvutia.

Amunike kwa upande wake ameitazama tofauti Stars.

“Mimi ni kocha na lengo langu la kwanza niliongea na wachezaji wangu tunataka kwenda Afcon na tumefuzu. Wamecheza mpira mzuri ndiyo maana leo hii tumefanikiwa kuingia AFCON.”

AFUMUA KIKOSI STARS

Ebhana eeh kama ulikuwa unadhani kikosi kilichoitwa na kuipiga Uganda 3-0 ndiyo kitaenda nchini Misri hiyo ishu ifute kabisa akilini mwako kwa sababu Amunike sio wa hivyo.

Amunike amekuwa akikosolewa vikali kila anapoteua wachezaji wa kuunda kikosi chake, moja ya sababu ikiwa ni kuita wachezaji ambao wanachezea timu za kawaida katika Ligi Kuu.

Hata hivyo, hakuwahi kuonyesha kutetereka katika kile anachokiamini. Aliendelea kusimamia anachokiamini hadi anaipeleka timu Afcon.

“Hii ni timu ya kila mchezaji wa Tanzania mwenye pasipoti ya kusafiria ya nchi hii, kwa hiyo wote wana nafasi ya kucheza. Siangalii huyu katoka Simba au Yanga, naangalia yule ambaye anapambana akiwa katika klabu yake na tunampa nafasi.

“Nina furaha kufuzu Afcon kiukweli na hili ni jambo zuri ambalo nilikuwa nalihitaji. Kama tusingeweza kuingia mashabiki wangekosa furaha, lakini hivi sasa ukiwaangalia kila mmoja ana sura ya furaha,” anasema.

Winga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, anaongeza kuwa huwa hana wasiwasi wowote anapoita kikosi chake kwasababu anaamini kitu anachokifanya daima anamshirikisha Mungu.

“Najua kwamba kila mtu huwa ana kikosi chake kichwani, lakini mimi ni kocha wa timu ya Taifa natakiwa kuwapa nafasi wachezaji, nasisitiza atakayecheza ni yule mwenye uwezo na kujituma.

ASHINDWA KUJIZUIA

Mechi dhidi ya Lesotho inakumbukwa na wengi baada ya Stars kuchezea kichapo 1-0.

Ilikuwa ni mechi iliyowavuruga kabisa Watanzania kwani ilikuwa ni mechi pekee ambayo Stars ingeweza kwenda moja kwa moja Afcon bila ya kuhitaji mbeleko ya mtu kama ingeshinda.

Wadau wa soka walitoa maneno makali kuhusu mbinu za ufundishaji za Amunike baada ya Stars kujiweka katika mazingira magumu kabisa ya kufuzu kufuatia kipigo hicho ambacho hakikutarajiwa.

Kutokana na kipigo hicho, Stars sasa ikahitaji mambo mawili ili ifuzu kwa mara ya kwanza Afcon katika miaka 39 tangu 1980 ilipofuzu kwa mara ya kwanza na ya mwisho.

Stars ilihitaji kuifunga Uganda nyumbani Dar es Salaam katika mechi yao ya mwisho ya kundi, na pia ilihitaji kuombea Cape Verde isipoteze nyumbani dhidi ya Lesotho katika mechi yao ya mwisho.

Haikuwa rahisi kwa Amunike kujitokeza mbele ya umati baada ya matokeo hayo yaliyomkera kila mmoja, wakiwamo wale waliosafiri kutoka Bongo mpaka Lesotho.

Hata hivyo, sasa Mnigeria huyo anaweza kusimama kifua mbele.

“Nina furaha na mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuishangilia timu katika kila hatua. Hata tulipoenda Lesotho walikuja pia, jambo ambalo ni kubwa sana. Nina furaha kuwaona waliendelea kutusapoti mpaka tumefanikiwa kufuzu.

“Nilikuwa nahitaji kuona mashabiki wana furaha. Mwanadamu anatakiwa awe na furaha muda wote.”

Je, unajua mikakati ya Amunike baada ya kuipeleka Tanzania kwenye fainali hizo za AFCON na vipi ishu yake ya kutaka kutimuliwa Stars? Kuna mengi ameyaweka wazi hivyo, hakikisha unasoma mwendelezo wa simulizi yake kesho Jumatatu.