UKWELI NDIVYO ULIVYO: Simba bado ina nafasi ya kuzidi kushangaza

SIMBA imeshangaza wengi na pengine inajishangaa yenyewe. Ndio, Simba imewashangaza hata wachezaji wake. Imewashangaza mabosi na makocha wa timu hiyo.

Hakuna aliyetarajia au kuamini kuwa, mwaka 2019 ingeandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kuvuka hatua ya makundi kuingia robo fainali.

Ndio, Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019. Iliiduwaza AS Vita ya DR Congo. Wakongo hawa walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Simba na Al Ahly pamoja na klabu nyingine sita zilizokuwa katika Kundi ya A, B na C zikienda hatua nyingine na Jumatano iliyopita droo imefanyika na kila moja ameshajua atakutana na nani.

Tuelewane mapema, Simba sio klabu ya kwanza kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (zamani Klabu Bingwa Afrika). Yanga ndio walioasisi kwa timu za Tanzania kucheza hatua hiyo waliposhiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika 1969 na kufika hatua hiyo na kurudia tena mwaka uliofuata 1970.

Pia Simba ilishafuzu hatua hiyo mwaka 1994 kabla ya Yanga kurudia tena mwaka 1998 ilipofuzu makundi baada ya michuano hiyo kubadilishwa mfumo mwaka 1997.

Enzi hizo ikiwa ni Nane Bora. Ilichokifanya Simba ni kwa mara ya kwanza kwa klabu za Tanzania kuvuka makundi ya michuano ya CAF. Haikuwahi kutokea kama ambavyo haijawahi kutokea tena kwa klabu za Tanzania kucheza nusu fainali tangu Simba hao hao walivyofanya katika Klabu Bingwa (sasa Ligi ya Mabingwa) mwaka 1974.

Ni Simba hao hao walioandikisha rekodi ambayo haijawahi kuguswa na timu za Tanzania pale ilipofika fainali ya michuano ya Kombe la CAF (lililounganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika). Ilikuwa mwaka 1993.

Malindi ya Zanzibar, Yanga na hata Simba zilishawahi kufika robo fainali ya Kombe la Washindi kwa nyakati tofauti, ndio maana sio ishu sana kwa Simba kufika robo fainali, ila kuwa klabu ya kwanza kuvuka makundi ni heshima kubwa kwao na Tanzania kwa jumla.

Yanga na Simba kwa miaka tofauti zilishatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 na 2003, lakini kote walitoka kapa. Kadhalika Yanga walishacheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa klabu pekee ya Tanzania kufanya hivyo katika michuano hiyo mwaka 2016 na 2018, lakini waliambulia patupu. Kwa namna yoyote Simba inastahili pongezi, kwani ilichokifanya sio heshima kwao tu, lakini imesaidia kuipeperusha Tanzania katika anga hilo la kimataifa. Klabu zilizokuwa zikiitazama Tanzania kama nchi kibonde, zimepata mshtuko. Ni kama ambavyo Kocha wa AS Vita Frolent Ibenge alivyopata mshtuko baada ya timu yake kutupwa nje na Simba aliyokuwa akiitazama kama dhaifu kundini.

Ushindi wa mabao 5-0 iliyopata nyumbani ilimfanya Ibenge aamini wangekuja kuifunga Simba ugenini jijini Dar es Salaam, lakini ikakumbana na aibu kwa kulala 2-1 na kutupwa nje ya michuano.

Kwa hali hiyo, hata TP Mazembe inayotokea DR Congo iliyopangwa kucheza na Simba katika robo fainali, huenda huko walipo presha imeanza kuwapanda na wanakuna kichwa kuwafikiria Msimbazi. Ni kweli sio mara yao ya kwanza kukutana, lakini kutolewa kwa AS Vita kunaweza kuwapata mshtuko wakiamini wana kibarua kizito kwa wababe hao wa Tanzania.

Kwa nafasi hiyo, Simba inapaswa nao kuitumia kama faida kwao kuiduwaza Mazembe. Wautumie mchezo wao wa nyumbani kupata matokeo mazuri ili kwenda kumaliza kazi ugenini. Rekodi zinaibeba Simba nyumbani na kuiangusha ugenini.

TP Mazembe sio timu nyepesi, hata Simba wanaikumbuka mwaka 2011 walikutana nao na walifungwa nje ndani, ila ilipenya baada ya Wakongo hao kufanya udanganyifu kupitia Javier Besala Bokungu.

Simba ilifungwa 3-1 ugenini. Bao la Emmanuel Okwi liliwashtua Wakongo wakijua ugenini watakuwa na kazi kubwa mbele ya Simba. Bahati mbaya ni kwamba Simba ilijikuta ikilala tena ikiwa nyumbani kwa 3-2 na kutupwa nje.

Hata hivyo ilikuja kubainika TP ilimchezesha Bokungu isivyo halali na kuondolewa michuanoni, nafasi yake kaachwa mikononi mwa Simba na Wydad Casablanca ya Morocco.

Katika mchezo huo uliopigwa Misri, Wekundu walipigwa 3-0 na kuanguka katika play-off ya Kombe la Shirikisho kwa kukutana na DC Motema Pembe ya DR Congo na kutolewa kwa mabao 2-1.

Ni wazi Simba inajua inaenda kukutana na kigogo, lakini silaha yao kubwa ni kuhakikisha wanapata ushindi mnono nyumbani ili hata kama itaenda kuanguka ugenini, basi ibebwe na ushindi wa awali.

Kocha Patrick Aussems na Msaidizi wake, Dennis Kitambi lazima warekebishe ukuta wao, Simba imekuwa ikiruhusu mabao mengi na hatua hiyo ya mtoano mabao ndio yanayobeba timu kusonga mbele.

Kama Simba itaendeleza udhaifu wao wa kuruhusu mabao kama ilivyofanya katika mechi zao zilizopita kuanzia hatua ya awali hadi makundi, Simba isitarajie miujiza tena. Itang’olewa na kushindwa kuifikia rekodi yao ya 1974 ya kucheza nusu fainali.

Lazima kina Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Juuko Murshid kama sio Zana Coulibaly na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ au yeyote yule atakayepangwa kumlinda Aishi Manula, lazima wazuie mabao.

Tabia yao ya kukaba kwa macho kama wataendelea nayo inaweza kuigharimu timu mbele ya Les Corbeaux, ambayo inapocheza uwanja wa nyumbani huwa moto zaidi na hata ugenini haitabiriki.

Lakini pia kina Meddie Kagere, John Bocco, Okwi na hata kina Clatous Chama ambaye amekuwa kiibeba Simba kwenye mechi ngumu, wafanye kila njia kufunga kadri wapatavyo nafasi.

Hii itaisaidia Simba kuzidi kushangaza Afrika na itakuwa na kazi nyepesi ugenini mjini Lubumbashi wakienda kurudiana na wenyeji wao TP Mazembe.

Kubwa zaidi ni kuhakikisha ikicheza nyumbani inashinda si chini ya mabao matatu bila kluruhusu wavu wao kutikiswa, vinginevyo tutarajie mkwamo kwa wawakilishi wetu hao, ambao hata hivyo kufika hatua hiyo tu ni heshima kwao. Kwani hakuna aliyetarajia!