ALLY BUSHIRI: Kaushusha msala kwa Mayanga

KLABU ya Mbao FC hivi karibuni ilitangaza kuvunja mkataba na aliyekuwa Kocha wao, Ally Bushiri ‘Benitez’ baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu juu ya matokeo na kumtangaza Salum Mayanga kuwa kocha mpya hadi mwishoni mwa msimu huu.

Uongozi wa Mbao FC, ulifikia maamuzi hayo ikiwa aliyekuwa Kocha mkuu Amri Said ‘Stam’ kuachana nao baada ya kugom akufanyakazi na Benitez ambaye wanalingana kiwango cha elimu (Leseni B).

Stam aliiacha Mbao nafasi ya nne ikiwa na pointi 24 baada ya kuiongoza timu hiyo mechi 17, alishinda sita, sare sita na kupoteza tano mechi za Ligi Kuu Bara.

Kuondoka kwa Stam ambaye alitimkia Biashara United, ilionekana wazi kuwaumiza wadau wengi wa soka jijini hapa hasa mashabiki wa Mbao ambao hadi sasa wanaendelea kukumbuka mchango wa kocha huyo.

Baada ya Benitez kutua Mbao hakuweza kumaliza muda mrefu ambapo amefundisha kwa kipindi cha miezi mitatu (siku 90) na kumwachia msala Mayanga wa kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi.

Makala haya yanakuletea mazuri na mabaya aliyoyaacha Benitez kwa siku alizodumu ambazo atakumbukwa na mashabiki wa soka jijini hapa na msala alioachiwa Mayanga.

Benitez alianza kazi rasmi ya kuiongoza Mbao tangu Desemba 23 mwaka jana licha ya kudumu kwa miezi mitatu ameweza kuisaidia timu hiyo kwa mafanikio kadhaa.

Michuano ya SportPesa

Pamoja na kutodumu kwa muda mrefu Benitez atakumbukwa kwa jinsi alivyoonyesha ubora wake kwenye michuano ya kombe la SportPesa iliyomalizika hivi karibuni.

Benitez aliweka rekodi tamu ambayo timu kongwe Simba na Yanga zilikuwa hazijawahi kufanya hasa kuifunga Gor Mahia na kuiondosha kwenye mashindano hayo.

Ukiachana na nafasi ya nne waliyoambulia kwa mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo, Benitez alisifiwa zaidi kwa jinsi kikosi chake kilivyopambana na kuonyesha ushindani wa hali ya juu.

Kutokana na mchango huo, Mbao na mashabiki wake wataendelea kumkumbuka kwani aliitangaza zaidi katika medani za soka kimataifa kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu.

Pamoja na mafanikio aliyoyaacha Benitez alifeli katika baadhi ya mambo na huenda ndio sababu zaidi ya uongozi kushindwa kuvumilia na kuamua kuvunja mkataba wake.

Michuano ya FA

Kwa misimu miwili mfululizo Mbao FC iliogopwa sana kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na awali ikiwa chini ya Mrundi, Ettiene Ndayiragije ilifika fainali na ilicheza na Simba huku Simba wakichukuwa ubingwa kwa ushindi wa bao 2-1, mechi iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Hata hivyo, baadaye ikiwa chini ya Mrundi huyo iliishia robo fainali huku ikionyesha ushindani wa hali ya juu tofauti na ilivyokuwa msimu huu ambao imeishia hatua ya awali.

Benitez mechi yake ya kwanza kuiongoza Mbao ilikuwa ni mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Dar City inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na ilitolewa kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao moja.

Kuanza vibaya mechi hiyo ya kwanza, haikuwa ishara nzuri kwake katika kazi yake kwani mashabiki na viongozi wa timu hiyo walianza kupatwa hofu juu yake ya uwezo wa kocha huyo kufungwa na timu iliyokuwa inaburuza mkia kundi A kwenye ligi yao.

Kuhusu Ligi Kuu

Kama haitoshi Benitez alianzia ugenini dhidi ya KMC na aliambulia suluhu, matokeo ambayo yaliendelea kumwonyesha ishara mbaya kuendelea kuwa na Mbao.

Mbali na hilo, kati ya mechi 13 alizoongoza Kocha huyo ameshinda tatu, sare tatu na kupoteza saba na kuifanya Mbao kuwa na pointi 36 ikishika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kutokana na matokeo hayo iliwalazimu viongozi wa Mbao kufumba macho na kuamua kumfungashia virago na kumpa shavu Mayanga.

Msala wa Mayanga

Licha ya Benitez kuondoka klabuni hapo, Mayanga amepewa jukumu la kuongoza jahazi hilo kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi.

Mkataba wa Mayanga na Mbao unamalizika mwishoni mwa msimu huu na endapo atatimiza lengo la klabu ndipo watakapofanya mazungumzo ya kumwongeza mkataba.

Mayanga lazima mwisho wa msimu akumbane na lawama au pongezi kutokana na mechi zilizobaki na ukizingatia ushindani ulivyo kwa timu nyingi kupambana kukwepa rungu la kushuka daraja.

Katika msimamo wa ligi timu kuanzia ya tano haiwezi kutamba kubaki kwenye ligi msimu ujao kwani kama itazubaa inaweza kuondoka na maji kulingana na pointi zao, hivyo Mayanga atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha Mbao haichezi hata ‘Play Off’.

Mbao yaweka rekodi

Mbao msimu huu imeweka rekodi ya kipekee kwa kuwatumia makocha wanne ndani ya msimu mmoja, ikianza na Amri Said, Ally Bushiri kisha kuwaleta Salum Mayanga na Msaidizi wake, Novatus Fulgence.

Ofisa habari wa klabu hiyo, Chrisant Malinzi alinukuliwa akisema wazi kuwa wao hawaogopi kubadilisha makocha hata wakiwa 10 kwa mpigo lakini malengo yao ni kuona Mbao inafanya vizuri.

Anasema kuwa hata timu zingine zikiwamo za Ulaya hufanya hivyo pale inapobidi, hivyo si jambo la kushangaza kwa Mbao kubadili makocha ikitokea matokeo hayajaridhisha.

“Hatuogopi kubadilisha Makocha hata wawe 10,kwa sababu na Ulaya wanafanya hivyo pale inapobidi kwa mustakabali wa Klabu, Mbao haina uvumilivu inapotokea matokeo kutoridhisha,” anasema Malinzi.

Mayanga afunguka

Mayanga aliyekuwa Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar, alisema mechi zilizobaki ni fainali kwake kutokana na malengo yake yalivyo katika kuibakiza timu kwenye ligi na kwamba anachohitaji ni ushirikiano kwa kila mmoja.

Alisema anafahamu wazi kwa sasa Ligi ilivyo ngumu na ushindani mkali kutokana na timu nyingi zinavyopambana kukwepa kushuka daraja.

“Mechi zote zilizobaki ni fainali katika kufikia malengo yangu ya kuinusuru timu, nafahamu kwa sasa ligi ni ngumu hasa timu nyingi zinavyopambana kukwepa kushuka daraja,” alisema Mayanga.