MSALA: Cheki wachezaji wa mkopo wanavyofeli kutoboa Arsenal

MAJALIWA ya Denis Suarez kwenye kikosi cha Arsenal anakocheza kwa mkopo yametajwa kuwa kwenye wasiwasi mkubwa kutokana na kutokuwapo na uwezekano wa Mhispaniola huyo kupata dili la kudumu la kuendelea kucheza kwenye kikosi hicho itakapofika mwisho wa msimu huu.

Suarez, 25, alinaswa na Arsenal akitokea Barcelona kwenye dirisha la Januari na kwamba hadi sasa amecheza dakika 67 tu huku kocha Unai Emery akionekana wazi kwamba bado hajafurahishwa na kiwango cha mchezaji huyo.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya soka wanasema hivi Arsenal haijawahi kuwa na rekodi nzuri kwa wachezaji wake inaowabeba kwa mkopo kwamba wengi wamekuwa wakifanya hovyo tu.

Junichi Inamoto - (Gamba Osaka, 2001)

Watu wengi walitaka kufahamu kulikoni wakati Arsenal ilipomsajili kwa mkopo kiungo wa Kijapani, Junichi Inamoto, ambaye baadaye walipaswa kumbeba jumla kwa ada ya Pauni 4 milioni.

Akiwa kinda, Inamoto alitua Arsenal akiwa kwenye moto kwelikweli akitamba kwenye J-League na hilo ndilo lililomvutia Arsene Wenger, ambaye alikuwa na ufahamu mzuri wa ligi ya Japan kwa sababu alikuwa katika timu ya Nagoya Grampus Eight. Lakini, kitu pekee ambacho kilikuwa na faida kwao Arsenal kwa kuipata huduma hiyo ya Inamoto ni kuongeza mauzo tu ya jezi zao huko Mashariki ya Mbali.

Inamoto aliichezea Arsenal mechi tatu tu, mbili kwenye Kombe la Ligi na moja kidogo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Leverkusen. Baadaye akatolewa kwa mkopo wa miaka miwili huko Fulham kabla ya kutimkia zake Uturuki, Ujerumani na Ufaransa. Kwa sasa anaripotiwa kuchezea timu ya Daraja la Tatu huko Japan, SC Sagamihara.

Julio Baptista - (Real Madrid, 2006)

Msimu wake wa kwanza Arsenal kucheza kwenye Uwanja wa Emirates, walimnasa kwa mkopo straika wa Real Madrid, Julio Baptista, huku wakimshuhudia staa wao Jose Antonio Reyes akitimkia zake Bernabeu.

Mshambuliaji huyo wa Kibrazili alifunga mabao matatu tu katika mechi 24 alizocheza kwenye ligi, lakini alikuwa moto kwenye Kombe la Ligi akifunga mabao sita na kuwafanya Arsenal kufika fainali na kufungwa na Chelsea iliyokuwa chini ya Jose Mourinho. Kumbukumbu zake nzuri kwenye kikosi kile zinakuja kwenye robo fainali ya Kombe la Ligi ambapo alifunga hat-trick dhidi ya Liverpool wakati Arsenal ilipoibuka na ushindi wa 6-3 uwanjani Anfield. Baptista alirudi zake Real Madrid na hakuonekana tena kwenye Ligi Kuu England huku mara ya mwisho akionekana kwenye klabu ya Cluj ya Romania.

Yossi Benayoun - (Chelsea, 2011)

Uhamisho wa kushtukiza iliyofanya Arsenal kwa kumbeba kwa mkopo Muisraeli Yossi Benayoun kutoka Chelsea. Licha ya kucheza mechi 19 tu za Ligi Kuu England, Yossi ambaye kipindi hicho alikuwa na miaka 31 alikuwa na mchango mkubwa kwa Arsenal. Kiungo huyo alianzishwa kwenye mechi muhimu dhidi ya Tottenham , Liverpool na Manchester City na alifunga pia mabao na kusaidia timu hiyo kukamatia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya mahasimu wao Spurs. Benayoun alirudi Chelsea mwishoni mwa msimu na kutolewa tena kwa mkopo kwenda West Ham.

Thierry Henry - (New York Red Bulls, 2012)

Kinara wa mabao wa muda wote Arsenal, Thierry Henry alirudi kucheza kwa mkopo wa miezi miwili akitokea Marekani kwenye kikosi cha New York Red Bulls. Msimu wa Ligi Kuu England ulikuwa umefika mwisho, hivyo Henry alirudi Arsenal kuja kuziba pengo la Marouane Chamakh na Gervinho waliokuwa wamerudi Afrika kucheza kwenye Afcon 2012. Walau Henry alikuwa na wakati mzuri alipocheza kwa mkopo akiifungia Arsenal bao la ushindi kwenye mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Leeds United, ambapo The Gunners walishinda 1-0.

Straika huyo alicheza mechi sita na kufanya mabao yake yawe yamefikia 228 wakati alipofunga kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Sunderland iliyokuwa mechi yake ya mwisho.

Emiliano Viviano - (Palermo, 2013)

Emiliano nani? Yawezekana wengi wakauliza swali hilo. Katika siku ambayo Arsenal ilifanya usajili wa Mesut Ozil uliovunja rekodi ya klabu kwenye uhamisho, wababe hao wa Emirates walimnasa pia kipa Emiliano Viviano kwa mkopo kutoka Palermo ya Serie B huko Italia. Lakini, hakucheza mechi yoyote akiwa Arsenal akikosa namba mbele ya Wapolandi wawili, Wojciech Szczesny na Lukasz Fabianksi.

Mechi aliyocheza kwenye timu hiyo ni huko ya kikosi cha U21, ambapo alipigwa bao tano wakati walipochapwa 5-1 na Sunderland.

Kim Kallstrom - (Spartak Moscow, 2014)

Katika dirisha la usajili wa Januari 2014, Arsenal walikwenda Spartak Moscow kumsajili Kim Kallstrom kwa mkopo baada ya wakali wake Jack Wilshere na Aaron Ramsey kuwa majeruhi na Mathieu Flamini alikuwa na adhabu. Wenger aliona suluhu ni kumnasa kwa mkopo Kallstrom, wakati huo akiwa na miaka 31. Lakini, mkopo huo ulionekana kama kichekesho tu, maana Kallstrom ndiye mwenyewe aliyekuja kupata majeruhi tena ambayo yalimfanya asicheze kwa wiki sita na hivyo mechi ya kwanza akacheza Machi. Kiungo huyo alicheza mechi nne tu kwenye kikosi hicho ikiwamo ile ya nusu fainali ya Kombe la FA aliyotokea benchi na kuja kufunga penalti dhidi ya Wigan Athletic.

Denis Suarez - (Barcelona, 2019)

Kuna huyu Denis Suarez. Arsenal ilimnasa kwa mkopo kutoka Barcelona kwenye dirisha la uhamisho wa Januari mwaka huu. Matumaini yaliyopo ni kwamba, mchezaji huyo abebwe jumla mwishoni mwa msimu.

Lakini, jambo hilo halionekani kama litakuwa na nafasi kubwa kutokana na mchango wake hafifu anaotoa tangu alipotua Emirates. Mhispaniola huyo bado hajaanza mechi yoyote kwenye kikosi hicho cha Arsenal akiwa ametumiwa mara nne kutokea benchi kwenye Ligi Kuu England na mara mbili kwenye Europa League. Suarez ana kazi kubwa ya kuifanya kumshawishi kocha Unai Emery kumbakiza kwenye timu yake.