NO AGENDA: TAIFA STARS IMEPEWA LESENI HALALI YA KUTEKELEZA MAUAJI

LESENI ya kuua haitolewi kila wakati. Hutoka kwa wakati maalumu kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli ya lazima kwa nchi. Novemba 2, 1978, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alilikabidhi Jeshi la Wananchi, leseni ya kumshughulikia Iddi Amin.

Leseni ilitumika vizuri kabisa. Amin alichezea kichapo, Kagera yetu ikakombolewa, utawala wake ukapinduliwa. Hata Waganda wakafurahia. Ndiyo maana, wakati sisi Vita vya Uganda na Tanzania huviita Vita ya Kagera, Waganda kwao huita Vita vya Ukombozi.

Leseni ya kuua haitolewi ovyo. Mfano, kila nyumba imepewa leseni halali ya kutekeleza mauaji dhidi ya mbu ili kupamba na malaria.

Kila familia ina leseni ya kutekeleza mauaji dhidi ya njaa. Zimejengwa shule na vyuo, walimu wamepewa leseni halali ya kuunyanyasa ujinga mpaka ufe.

Kama nchi, leseni halali imetolewa tena leo kwa ajili ya kutekeleza mauaji. Bahati nzuri, si mauaji ya umwagaji damu, bali ndani ya dimba la soka. Hakuna namna, kwani wanaotakiwa kuuawa ndiyo walewale jeshi letu liliowakomboa mikononi mwa Amin Juni 1979, Uganda.

Yes, kama jeshi lilivyopewa leseni ya kumpa kichapo cha damu Amin, ndivyo Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imekabidhiwa leseni halali ya kuibomoa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’. Sharti, mauaji lazima yatekelezwe ndani ya dakika 90. Hakuna dakika 30 za nyongeza wala penalti.

Kinacholeta raha, yatakuwa mauaji yenye tabasamu. Stars haina budi kuua leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Baada ya mchezo, mashujaa wetu watakumbatiana na ‘askari’ wa Uganda. Maana, safari ya Misri itakuwa imeiva.

Waganda hata wakiuawa kwa mabao 200 bila leo, wao wameshafuzu safari ya Misri, pointi zao hakuna wa kuzifikia. Wanasubiri muda tu ili wakaitetee nchi yao kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazochukua nafasi kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

HESABU ZETU

Matokeo ya kufungwa, sare au suluhu, yataitupa nje Stars. Mchezo kati ya Cape Verde na Lesotho leo, utakuwa na nafasi kubwa kuamua kuhusu tiketi ya Stars Afcon 2019. Hata hivyo, muhimu ni Stars kwanza washinde ndipo wachungulie kwingine.

Uganda, Tanzania, Lesotho na Cape Verde, zipo kundi L. Msimamo ni kuwa Uganda wanaongoza kwa pointi 13, Lesotho ya pili ina pointi 5, Tanzania ya tatu na pointi 5, wakati Cape Verde ipo namba nne na pointi zake nne.

Uchambuzi ni kuwa Uganda imeshafuzu, maana imecheza mechi 5, imeshinda nne na kutoka sare moja. Nafasi kwenye kundi inawaniwa na timu zote tatu zilizobaki. Kila timu, kwa maana ya Tanzania, Lesotho na Cape Verde, inaweza kupata tiketi ya kwenda Afcon leo.

Tukianza na Cape Verde inayoshika mkia. Ikishinda leo dhidi ya Lesotho, itafikisha pointi 7. Endapo Stars itapigwa na Uganda, maana yake wao ndiyo watamaliza wa pili kwenye msimamo nyuma ya Uganda.

Vilevile Uganda na Stars wakitoka suluhu au sare, bado Cape Verde wakiifunga Lesotho watakwenda Afcon, kwani Stars itafikisha pointi 6, wakati Cape Verde watakuwa na 7.

Lesotho ina pointi sawa na Stars. Kwa leo, ndiyo timu ambayo inapaswa kupigana ili ishinde na moja kwa moja itafuzu Afcon hata kama Stars itaifunga Uganda kwa ushindi wowote ule. Lesotho wanabebwa na kanuni za Caf za uendeshaji wa michuano ya Afcon.

Kwa mujibu wa ibara ya 14 ya Kanuni za Afcon (Regulations of the Africa Cup of Nations), timu zinapolingana pointi (Tiebreakers), kinachotazamwa ni sheria ya head-to-head, yaani katika timu mbili zilizolingana, zilipokutana, nani alipata nini dhidi ya mwenzake?

Kama timu zimepata pointi sawa, yaani katika mechi mbili, kila timu ikapata pointi 3, kinachofuata ni kutazama ni nani kapata magoli mengi walipokutana. Kisha yupi anakuwa na kashinda magoli mengi ugenini.

Kama kote watakuwa wamelingana ndiyo inatazamwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kwenye kundi zima. Mwisho ndiyo bahati nasibu kama kote wamelingana asilimia 100.

Kanuni zinasema Stars akishinda na Lesotho akampiga Cape Verde, moja kwa moja Lesotho anakwenda Afcon. Maana wote watafikisha pointi 8, halafu kanuni ya kwanza kutazamwa ni ibara ya 14.1.1, inayosema aliyepata pointi nyingi katika mechi zilizokutanisha timu mbili zinazolingana pointi, ndiye anakwenda.

Katika pointi 5 za Lesotho, 4 imezipata kutoka Stars. Ilitoka sare ya 1-1 na Stars Chamazi Complex, kisha ikaifunga Stars 1-0 kwenye Uwanja wa Setsoto, jijini Maseru. Hivyo kikanuni, Lesotho wakishinda leo, moja kwa moja wanakwenda Afcon.

Kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, Stars ipo mbele ya Lesotho. Stars in hasi 2, Lesotho ni hasi 4. Hata hivyo, tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ipo ibara ya 14.1.5. Yaani ni kipengele cha tano kutazamwa. Ni mbali mno.

UTAMU ULIPO

Utamu kwa Stars ni kuwa Lesotho wanacheza ugenini leo. Cape Verde watakuwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Taifa (Estádio Nacional de Cabo Verde) na wanahitaji ushindi ili wasikilizie Uganda kuifunga Stars, waweze kwenda Afcon. Hivyo, si mechi mchekea kwa Lesotho.

Lesotho wakiwa nyumbani, walipokutana na Cape Verde, Septembs 9, mwaka jana, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Hiki ni kipimo kuwa Cape Verde wanawamudu sana Lesotho. Endapo Cape Verde watashinda au watatoka sare, Stars akishinda, safari ya Afcon inakuwa imeiva.

Hii ndiyo sababu Stars wamepewa leseni ya kuua. Sare haiihitajiki na kufungwa hatutaki kusikia. Tunataka ushindi, halafu tungoje Cape Verde watupe tabasamu dhidi ya Lesotho.

Kama jeshi lilivyotumia ilivyotakiwa leseni halali waliyopewa na Mwalimu Nyerere Novemba 2, 1978 dhidi ya Amin. Tunataka kuona mashujaa wa Stars wakitumia vema leseni halali waliyopewa kwa ajili ya kuiteketeza Uganda leo.

Kama Mwalimu Nyerere alivyosema: “Tufanye nini? Tunayo kazi moja tu, Watanzania sasa. Ni kumpiga. Uwezo wa kumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo. Na nia ya kupiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine.”

Leo pia, Stars ina uwezo, sababu na nia ya kuwapiga Waganda. Dunia ielewe kuwa hatuna kazi nyingine zaidi ya kuwapiga Waganda leo. Mwalimu Nyerere alipotoa tamko la vita alisema, “Tulieni muone vijana wetu watafanya nini”, tamko la leo ni kwenda kuujaza Uwanja wa Taifa ili kushuhudia vijana wetu watafanya nini, huku tukishangilia mwanzo mpaka mwisho.