Mmesikia, kumbe Bale anashabikia Arsenal bana

SUPASTAA wa Real Madrid, Gareth Bale amekiri kuwa shabiki wa Arsenal na amekuwa hivyo tangu alipokuwa mdogo!

Wakati sasa akiwa kwenye kikosi cha Real Madrid ambacho kila mchezaji yeyote wa soka duniani angependa kwenda kuitumikia timu hiyo, staa huyo wa kimataifa wa Wales alifichua ushabiki wake kwa Arsenal, ambao ni mahasimu wakubwa wa timu yake ya zamani, Tottenham Hotspur.

Bale alisema kwenye kipindi chake cha utoto amekua kwa kuwatazama mastaa Thierry Henry na Dennis Bergkamp walipokuwa pamoja huko kwenye kikosi cha Arsenal na alitumia wachezaji hao kama dira katika kuendeleza soka lake.

“Nilikuwa nawatazama sana Arsenal na hakika nilikuwa nikifurahi sana kuwatazama watu kama (Thierry) Henry,” alisema Bale.

“Nilikuwa nikimtazama pia Dennis Bergkamp. Walikuwa na timu nzuri. Nafahamu mashabiki wa Tottenham hawawezi kulifurahia hili nimekuwa nikiishabikia Arsenal!.”

Staa huyo kwa sasa anatajwa huenda akarudi kwenye Ligi Kuu England akiwindwa na Manchester United na hata timu yake ya zamani ya Spurs na haifahamiki mashabiki wa timu hiyo watampokeaje baada ya kukiri huku yeye tangu utoto wake alikuwa akiishabikia Arsenal.