Lile Bao la England, zimepigwa pasi kama zote

ENGLAND wameipiga Czech Republic Tano Bila kwenye kufuzu michuano ya Euro 2020. Kwenye mechi hiyo, staa wa Manchester City, Raheem Sterling alipiga hat-trick na kumfanya aendelee kuonyesha kwa sasa anacheza soka la kiwango cha ubora wake.

Hata hivyo, achana na mabao yote hayo matano, bao la kwanza la England kwenye mechi hiyo lilikuwa matata kwelikweli. Bao hilo hadi linafungwa lilihusisha wachezaji 10 kati ya 11, huku zikiwa zimepigwa pasi 25 kabla ya Sterling kuweka mpira kambani. Mpira ulianzia kwa kipa Jordan Pickford na uliguswa na kila mchezaji wa England isipokuwa Dele Alli tu ndani ya uwanja kabla ya Sterling kufunga kutokana na asisti moto kutoka kwa Jardon Sancho aliyepata mpira baada ya kupenyezewa na nahodha Harry Kane.

Katika mchezo huo uliofanyika uwanjani Wembley, England ilipata pigo kwenye dakika ya 17 tu baada ya kiungo wao wa kati, Eric Dier kutolewa uwanjani kutokana na kuwa majeruhi.

Hata hivyo, dakika chache baadaye, Sterling aliwapa bao la kuongoza vijana hao wa Kocha Gareth Southgate baada ya asisti tamu kutoka kwa Sancho.

Three Lions walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 baada ya Kane kufunga kwa mkwaju wa penalti.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Sterling akifunga tena mara mbili, huku bao jingine Czech wakijifunga baada ya Callum Hudson-Odoi kupiga shuti lililomshinda kipa Kiri Pavlenka na mpira kwenda kwenda kumbabatiza Tomas Kalas akiusukumia nyavuni kuwapa England ushindi huo mnono kabisa.