Hii ya bosi Bayern, Guardiola noma sana

RAIS wa Bayern Munich, Uli Hoeness amefichua ameelezwa kila kitu na swahiba wake, Pep Guardiola jinsi Manchester City inavyofanya inapohitaji kusajili mchezaji kwa pesa nyingi.

Hoeness amedai Mhispaniola Guardiola alimweleza vile mabosi wa Man City wanavyofanya kila wanapohitaji mchezaji mpya kwenye klabu hiyo wakimnasa kwa pesa ndefu.

Alisema Sheikh Mansour amekuwa akitoa pesa inayohitajika kwenye usajili wa mchezaji, lakini baadaye anarudisha ndani ya kipindi kifupi tu kwa kuongeza bei kwenye mafuta.

Hoeness alisema kwenye mkutano mmoja huko Munich: “Rafiki yangu Pep ameniambia kinachotokea wakati anapohitaji mchezaji wa pesa nyingi zaidi ya Euro 100 milioni au Pauni 86 milioni.

“Anakusanya video za mchezaji huyo na kuziunganisha pamoja na kwenda kumwonyesha Sheikh. Anapokuwa huko anamwelezea mchezaji huyo kwenye hiyo video na hapo tu, pesa inatumwa. Siku inayofuatia, Sheikh anaongeza pesa kidogo kwenye bei ya mafuta kurudisha pesa iliyotumika.”

Siku za karibuni kumeelezwa Man City inafanyiwa uchunguzi kuhusu usajili wao wanaofanya ambao kimsingi unadaiwa kukiuka utaratibu unaoelezwa na Uefa kwenye suala la usawa kwenye mapato ya timu na matumizi kwenye usajili.