Wauzwe, wabaki Man United

MANCHESTER, ENGLAND. LINALOONEKANA kwa sasa Ole Gunnar Solskjaer anakwenda kukabidhiwa kikosi cha Manchester United moja kwa moja mwisho wa msimu.

Kocha huyo wa muda huko Old Trafford amekutana na vipigo mfululizo kwa siku za karibuni, lakini amefanya kazi kubwa kwenye kikosi hicho tangu alipochukua mikoba ya Jose Mourinho Desemba mwaka jana na hilo ndilo linalompa nafasi ya kupewa kibarua cha kuwaongoza wababe hao kuanzia mwanzo kwenye msimu wa 2019/20.

Lakini, swali la kujiuliza kikosi chake kitakuwa na mwonekano gani kwa msimu huo ujao? Mashabiki wa Man United duniani kote wamekuwa na hamu ya kufahamu majina mapya yatakayotua kwenye kikosi chao baada ya sasa kuhusishwa na mastaa kibao. Lakini, wakihitaji kufahamu pia ni wachezaji gani waliopo kwa sasa wanapaswa kubaki kuendelea kuwa chini ya Solskjaer? Kwenye hilo ndipo unapoibuka mjadala huu wa nani wa kuuzwa na nani wa kubaki kwenye kikosi hicho cha Old Trafford ili kufahamu itakavyokuwa msimu ujao

MAKIPA

David de Gea

Kwa sasa ndiye namba moja kwenye kikosi hicho cha Old Trafford na kwamba, Man United inapambana kwa nguvu zote kumsainisha mkataba mpya ili abaki kwa muda mrefu kwenye kikosi chao baada ya Real Madrid kuripotiwa kumtaka. Kiwango cha De Gea hakina shaka na hakika ni mchezaji namba moja anayehitajika kwenye timu hiyo kuliko wengine wote. ABAKI.

Lee Grant

Kipa huyo veteran amesainishwa mkataba wa miaka miwili wakati anasajiliwa mwaka jana kuja kufanya kazi ya kuambukiza uzoefu wake kwa makipa waliopo kwenye kikosi hicho. Ni kipa chaguo la tatu, hivyo uwepo wake kwenye kikosi haina shida yoyote kwa sababu ni mtu anayetumika zaidi mazoezini katika kutambua nguvu za washambuliaji wa timu hiyo. ABAKI.

Sergio Romero

Anapokosekana David De Gea, Man United inakuwa bado ipo kwenye mikono salama kutokana na uwepo wa kipa wa Kiargentina, Sergio Romero. Wakati sasa De Gea akiwa kwenye chokochoko za wababe wa Real Madrid, Man United hawawezi kufanya ujinga wa kuamua kumuuza Romero kwa sababu ndiye anayewaondolea stresi wakati Mhispaniola huyo atakapoamua mpango wa kutimkia Bernabeu. ABAKI.

MABEKI

Victor Lindelof

Mwanzoni alionekana kama kichekesho tu kwenye kikosi hicho cha Man United chini ya Mourinho kwa sababu Lindelof hakuwa akitumika ipasavyo. Lakini, baada ya kuja Solskjaer kila kitu kimebadilika na Lindelof amekuwa beki, ambaye anapokosekana kwenye mechi basi mashabiki wa Man United wanakuwa kwenye shaka kubwa. ABAKI.

Eric Bailly

Beki, Bailly ameshindwa kupandisha ubora wake wa kiuchezaji tofauti na matarajio ya wengi kwamba angekuwa mchezaji wa kutumainiwa kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo. Majeraha ya mara kwa mara pia yamekuwa yakimtibulia mchezaji huyo na sasa amejikuta akionekana kuwa ni nyongeza tu kikosini. AUZWE.

Phil Jones

Beki, Phil Jones alisaini mkataba mpya hivi karibuni tu. Mwanzoni alikuwa mchezaji ambaye wengi waliamini asingesaini dili jipya la kuendelea kubaki kwenye timu hiyo, lakini kutokana na ule uwezo wake wa kucheza mechi za mipango Man United inaona ni sahihi kubaki na mchezaji wa aina hiyo kikosini. ABAKI.

Chris Smalling

Mchezaji mwingine huyo ambaye hakuna mtu anayemwaamini kabisa. Smalling amekuwa na kiwango kinachofanana na homa za vipindi, kuna wakati anacheza kwa kiwango cha juu sana, lakini kuna siku nyingine amekuwa na makosa mengi ndani ya uwanja. Siku za karibuni ameonekana kuelewana vyema na Lindelof, hivyo katika kipindi ambacho Man United haijasajili beki mpya, Smalling anaweza kuwafaa. ABAKI.

Marcos Rojo

Muargentina, Rojo nyota imemkataa kwenye kikosi cha Man United. Anapokuwa kwenye timu yake ya taifa mambo yanakuwa tofauti kabisa. Jambo jingine linalomtatiza beki huyo ni majeruhi ya mara kwa mara ambayo yanamfanya kutokuwa na muda wa kutosha wa kuitumikia timu yake. Man United inaona inalipa tu mshahara wa bure na ndiyo maana haioni kama inamhitaji sana beki huyo. AUZWE.

Ashley Young

Kama ilivyo kwa Jones, beki huyo mkongwe, Young alisaini mkataba mpya mwezi uliopita tu hapo wa kuendelea kukipiga kwenye kikosi hicho. Halitakuwa jambo la kushangaza kama atateuliwa kuwa nahodha wa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao baada ya sasa kukivaa kitambaa hicho. Young bado anacheza soka lenye umuhimu mkubwa kwenye timu hiyo. ABAKI.

Diogo Dalot

Kinda, Dalot hana muda mrefu kwenye kikosi cha Man United na hakika huu ni msimu wake wa kwanza na kiwango bora kutoka upande wake kimeonekanna. Ni mchezaji kijana ambaye Man United wanaamini watavuna matunda makubwa sana kutoka kwake kutokana na kile ambacho amekionyesha hadi sasa katika mechi alizocheza. ABAKI.

Luke Shaw

Kitu anachofurahia Luke Shaw kwa sasa ni vita alivyoweza kuikabili vita ya Mourinho na kuishinda kutokana na alivyokuwa akimshambulia kwenye vyombo vya habari kwa kila mechi. Beki huyo wa kushoto kwa sasa ametulia na kucheza soka la ubora wake linalothibitisha kwanini Man United walitoa pesa nyingi kunasa huduma yake walipomsajili kutoka Southampton. Shaw ni muhimu kwenye kikosi hicho kwa sasa. ABAKI.

Antonio Valencia

Beki, Antonio Valencia amekuwa mtumishi bora kwenye kikosi cha Man United kwa zaidi ya miaka 10 na hakika sasa anastahili kupumzika. Akiwa na miaka 33, humwoni kama beki huyo anaendelea kutamba zaidi kwenye soka la kiushindani hasa kutokana na Man United kwa sasa kuhitaji kuwekeza kwenye nguvu mpya. Valencia hana kitu kipya atakachoweza kuifanyia Man United tena. AUZWE.

Matteo Darmian

Mara kadhaa beki wa Kitaliano, Darmian amekuwa akihusishwa na mpango wa kuihama Man United kitu ambacho kilisubiriwa sana kitokea kwenye dirisha lililopita, lakini kilishindikana. Kwa hali ilivyo ni jambo la kawaida kama ukisikia beki huyo amefunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu kwa sababu haonekani kuwapo sana kwenye mipango ya Solskjaer. AUZWE.

VIUNGO

Paul Pogba

Chini ya Mourinho, kundi kubwa la mashabiki wa Man United walikuwa wameshamchoka Pogba na kama angeuzwa basi isingekuwa ishu kubwa kwao. Lakini, tangu Solskjaer alipokuja kuchukua timu hiyo, Pogba amekuwa mchezaji tofauti kabisa na hakuna shabiki wa timu hiyo anayemtaka aondoke tena. Ubora wake bado unahitaji kwenye kikosi hicho hasa ukizingatia kwamba bado umri wake ni mdogo na atatumika kwa miaka mingi. ABAKI.

Juan Mata

Kwenye timu yoyote unaambiwa hivi ni jambo la msingi kuwa na mchezaji mwenye ufundi mkubwa wa kuuchezea mpira ili iwe rahisi kupenya kwenye ngome za timu ngumu. Katika kikosi cha Man United mchezaji wa aina hiyo ni Juan Mata. Mkataba wake unaelekea kufika mwisho na bado hakuna makubaliano ya dili jipya, lakini jambo la wazi kabisa Man United haitakuwa na kitu kizuri kama itakubali kumpoteza Mhispaniola huyo. ABAKI.

Jesse Lingard

Mipango ya muda mrefu ya Man United ni kuwekeza kwenye soka la vijana na hilo linaanzia na kuwa na wachezaji kama Lingard kwenye kikosi. Staa huyo ni muhimu kwenye timu hasa ukizingatia ni zao la akademia ya timu hiyo. Lingard amekuwa chaguo la Solskjaer hivyo, kuondoka ni ishu kubwa. ABAKI.

Andreas Pereira

Kama ingekuwa kuondoka basi Pereira angeihama Man United katika kipindi cha Mourinho. Mbrazili huyo ana kipaji na ndio maana hata Mourinho aligoma kumuuza au kumtoa kwa mkopo msimu huu. Solskjaer ameona umuhimu wa kuwa na Pereira kikosini kwake, ni mchezaji anayekupa kitu cha ziada wakati wa shida. ABAKI

Fred

Katika mechi za karibuni, Fred alicheza kwa kiwango kikubwa baada ya kuaminika na Soskjaer. Fred ni usajili wa Mourinho, ambaye alitumia Pauni 52 milioni kupata huduma yake. Kipindi chake alimweka benchi tu kabla ya kuja Solskjaer na kumpa nafasi taratibu. ABAKI.

Ander Herrera

Mkataba wake unaelekea mwisho, lakini kama kuna mchezaji ambaye mashabiki wasingependa aguswe basi ni Ander Herrera. Siku za karibuni imeonekana wazi kabisa anapokosekana kwenye kiungo ya katikati hata floo ya mchezo wa Man United inakuwa ngumu. PSG wanaripotiwa kumhitaji, lakini jambo hilo halionekani kama Man United watakubali kirahisi. Herrera ni muhimu kwa Man United. ABAKI.

Nemanja Matic

Alikuwa askari matata katika kipindi cha Mourinho. Lakini, kwa sasa chini ya Solskjaer ambapo Man United inahitaji kucheza soka la kasi zaidi, Matic anaonekana mzigo na tatizo kikosini. Mechi za karibuni ambazo amecheza ameonyesha uchovu ambao umeifanya Man United kushindwa kupata matokeo. Matic ni kiungo mzuri, lakini si mchezaji anayeifaa katika soka la Solskjaer. AUZWE.

Scott McTominay

Bado amekuwa akijifunza kutoka kwa viungo wenzake. Hakika kiungo McTominay ana kipaji kikubwa sana na kama ataendelea kupata nafasi ya kucheza basi atakuja kuwa mchezaji mkubwa sana.

Kutokana na Man United haitakuwa na muda wa kutosha wa kumpa nafasi ya kucheza kila mara basi njia nzuri ya kulinda kipaji cha mchezaji huyo ni kumtoa kwa mkopo akacheze timu itakayompa nafasi ya kucheza kila wiki kisha akirudi atakuwa tayari amekuwa mtamu na kuchukua nafasi za wakongwe klabuni hapo. ABAKI

WASHAMBULIAJI

Alexis Sanchez

Man United wanamlipa Alexis Sanchez mshahara mkubwa sana kwa wiki. Lakini, kiwango chake cha uwanjani hakuna kitu cha ajabu alichokifanya mshambuliaji huyo kwa kulinganisha na kiwango anacholipwa tangu alipotua kwenye kikosi hicho cha Old Traffford.

Umri wake nao umeshakwenda, hivyo ni nusu kwa nusu kama Sanchez anaweza kuwa kwenye viwango bora tena na kuipa faida Man United. Bado ni suala ambalo limekuwa likizusha mjadala mpana ila matokeo ni haya hapa. AUZWE.

Romelu Lukaku

Hapo katikati kama kulikuwa na mshambuliaji aliyekuwa akiwaudhi Man United badi ni Romelu Lukaku. Mchezaji huyo alionekana kuwa mzito sana na kuhitaji nafasi nyingi kufunga bao. Lakini, chini ya Solskjaer mambo yamebadilika na Lukaku ameonyesha kuwa tofauti katika kufunga mabao akihitaji nafasi chache kuweka mpira kwenye kamba.

Kwa sasa Lukaku si mchezaji, ambaye Man United watathubutu kumwaacha aondoke kwa kile anachoweza kuwafanyia ndani ya uwanja. Kwani mbali na kufunga, pia anatoa pasi za mabao na kuongeza hofu kwa mabeki wa timu pinzani. ABAKI.

Marcus Rashford

Huyu ndiye Harry Kane wa Man United. Kwenye orodha ya washambuliaji wote wa timu hiyo, Rashford ni silaha ambayo wanaamini wataitumia kwa miaka mingi sana. Umri wake bado ni mdogo, lakini amekuwa akicheza soka kwa ukomavu mkubwa unaowafanya mashabiki wote wa Man United kuamini katika huduma yake.

Vigogo wengine huko Ulaya wanamtaka pia kwa shughuli yake ya uwanjani. Man United bado inamhitaji zaidi Rashford. ABAKI.

Anthony Martial

Mchezaji mwingine huyo, ambaye ingekuwa nguvu sana kubaki kwenye kikosi cha Man United kama kingeendelea kuwa chini ya Mourinho. Walitibuana kinoma na Mourinho na alishawekwa kwenye orodha ya kuuzwa. Staa huyo wa Ufaransa alivurugzwa sana na Mreno huyo na kitu ambacho alikuwa akikifiria ni kuachana tu na maisha ya Old Trafford.

Lakini, ujio wa Soskjaer umebadili kila kitu na Martial amesaini mkataba mpya kwenye kikosi hicho. Bado kijana na anatazamwa kwenye anga za juu sana kisoka na kuibeba Man United siku za baadaye. ABAKI.