Simba ya dewji yavuna bil 2.2 za kina okwi

NDANI ya miaka 13, Simba imekuwa ikijivunia kuuza wachezaji wake nje ya nchi. Imekuwa miongoni mwa klabu ambayo haina uchoyo wa mafanikio ya wachezaji wake hasa pale wanapoona kuna masilahi kwa mchezaji na klabu husika.

Kuanzia mwaka 2006 imekuwa ikiendelea kuuza nyota wake ukiachana na miaka ya nyuma ya hapo ambapo hadi sasa imekusanya jumla ya Dola 915000 ambayo ni zaidi ya Sh2.2 bilioni.

Pesa hiyo ni ndefu mno ambayo inaweza kutosha kuendeshea shughuli za klabu hiyo hasa usajili wa kikosi cha maana.

Mwanaspoti inakuleta usajili wa wachezaji nane ambao ni baadhi tu ya waliouzwa kwa pesa ndefu wakiwa mikononi mwa Simba ambayo sasa inaendeshwa kwa mfumo wa kampuni baada ya kuachana na mfumo wa zamani wa wanachama.

EMMANUEL OKWI - Sh946 milioni

Mganda Emmanuel Okwi ndiye mchezaji pekee ambaye hadi sasa ameiingizia kiasi kikubwa cha pesa ambapo ameingia jumla ya Dola 410000 zaidi ya Sh946 milioni akiwa na timu mbili tofauti.

Simba ilimsajili Okwi akitokea SC Villa msimu wa 2010 ikiwa ni mara yake ya kwanza mshambuliaji huyo kucheza Ligi Kuu Bara, alipewa mkataba wa miaka miwili lakini kabla mkataba haujamalizika aliuzwa klabu ya Etoil du Sahel ya Tunisia msimu wa 2013 kwa Dola 300,000 zaidi ya Sh600 milioni.

Okwi aliamua kuvunja mkataba na klabu hiyo ambapo alirudi klabu yake ya zamani ya Villa inayoshiriki Ligi Kuu Uganda na baadaye kujiunga Yanga ambako alivunja mkataba wake baada ya Yanga kushindwa kutimiza makubaliano ya kimkataba.

Hakumaliza hata msimu na kutimkia Simba alikosaini mkataba.

Alirudi Simba kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia 2015 hadi 2017 lakini hakumaliza mkataba huo na kupata dili la kuichezea timu ya S¯nderjyskE kuaniza msimu huo huo wa 2015-17, huko alilamba mkataba wenye thamani ya dola 110000 zaidi ya Sh 250 milioni. Hivyo kuipa Simba jumla ya dola 41,000.

MBWANA SAMATTA - Sh300 milioni

Samatta anayekipiga KR Genk kwasasa alisajiliwa Simba akitoka African Lyon msimu wa 2010, alidumu na Wekundu hao kwa msimu mmoja pekee na kupata ofa ya kwenda TP Mazembe (2011-2016).

Ofa ya Samatta ilikuwa Dola 150,000 zaidi ya Sh300 milioni ambayo kwa Simba isingekuwa rahisi kuitema, ofa hiyo pia iliambatana na mgao wa asilimia 20 kama TP Mazembe wakimuuza timu nyingine.

Ndivyo ilivyokuwa hata pale ambapo Genk walipomnunua Samatta msimu wa 2016 na Simba ilipata mgawo wao huo wa asilimia 20 ambayo yalikuwa ni makubaliano yao ya kimkataba kutokana kwamba ndiyo waliomlea.

Mpaka sasa Samatta bado yupo Genk ambapo mwaka jana ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ingawa kuna timu nyingi zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.

PATRICK OCHAN - Sh300 milioni

Simba ilimsajili kiungo Patrick Ochan raia wa Uganda akitokea timu ya St George FC ya Ethiopia msimu wa 2011 ambapo alidumu hadi masimu wa 2014 akiwa ameichezea timu hiyo misimu miwili na kutimkia TP Mazembe msimu uliofuata.

Ochan ambaye aliichezea timu ya URA ya nchini kwao aliuzwa kwa dola 150,000 zaidi ya Sh 300 milioni kwa matajiri hao wa DR Congo. Ochan aliungana na Samatta ambaye pia alitokea Simba ingawa Samatta alitangulia kuingia Mazembe.

SHIZA KICHUYA - Sh196 milioni

Ni mauzo mapya kwa Simba ambayo wameyafanya tangu mwaka huu uanze, Kichuya ameuza kwa Dola 85,000 zaidi ya Sh 196 milioni.

Simba wamefikia hatua hiyo baada ya kufikia makubaliano ya kibiashara na klabu ya Pharco FC ya Misri ambao pia wamemtoa kwa mkopo katika klabu ya ENPPI inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Kichuya ni mwendelezo wa faida ambazo Simba inazipata kupitia mauzo ya wachezaji wake wanapokwenda kucheza soka la kulipwa na wamekubali kuvunja mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja wa Kichuya uliokuwa umebaki.

HENRY JOSEPH - Sh90 milioni

Kiungo wa zamani wa Simba na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Henry Joseph Shindika ni miongoni mwa nyota ambao kwa miaka ya nyuma alivumilia kuzivumilia changamoto za ugenini alipokwenda kucheza soka la kulipwa katika timu ya Kongsvinger IL Toppfotball iliyopo Norway mwaka 2009.

Simba ilimuuza Shindika kwa Dola 40,000 zaidi ya Sh 90 milioni, pesa ambayo kwa wakati huo ilikuwa nyingi mno kutokana na thamani yake ukilinganisha na sasa ambapo gharama za maisha zimepanda. Shindika alidumu kwa miaka minne nchini huo.

HARUNA MOSHI ‘BOBAN’ - Sh100 milioni

Mwaka 2009, Simba ilimuuza kiungo wake Haruna Moshi ‘Boban’ katika klabu ya Gefle IF ya Sweeden ingawa hakukaa kwa kipindi kirefu kwa kile kilichoelezwa kwamba hakuwa tayari kukatwa kodi kutoka kwenye mshahara wake uliotajwa kuwa Dola 5,000 kwa mwezi.

Ilielezwa kwamba klabu hiyo haikuwa na pesa za kuilipa Simba hivyo wakala wake ndiye aliyelazimika kuilipa Simba kiasi hicho cha pesa cha Dola 45000 zaidi ya Sh 100 milioni kwasasa.

SELEMAN MATOLA - Sh57 milioni

Mwaka 2006, kiungo wa zamani wa Simba, Seleman Matola ambaye sasa ni kocha wa Lipuli FC ya Ligi Kuu aliuzwa katika klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka miwili.

Matola ni miongoni mwa nyota wa mwanzoni kuuzwa Simba wakipokea kitita cha Dola 25000 zaidi ya Sh57 milioni kwasasa. Pesa hizo kwa wakati huo zilikuwa ni nyingi mno kutokana na thamani yake.

DANNY MRWANDA - Sh23 milioni

Mshambuliaji wa zamani wa Simba alicheza soka la kulipwa kwa mafanikio makubwa ambapo alipitia timu mbili tofauti.

Kabla ya kutua Simba aliichezea Arusha United (2003ñ2005), Simba alisajiliwa msimu wa (2006-2008) na kuuzwa Al Tadamon ambako alicheza msimu mmoja (2008ñ2009) na kurejea Simba kwa msimu mmoja kabla ya kwenda Dong Tam Long An (2010-2011) na baadaye kujiunga na Hoang Anh Gia Lai msimu uliofuata.

Simba kwa mara ya kwanza walimuuza Mrwanda kwa Dola 10,000 zaidi ya Sh 23 milioni huku akilipwa mshahara mnono.