Mzunguko wa kumi umeanza kutoa mwelekeo wa msimu

Friday November 2 2018

 

WATANZANIA tukiwa tunaendelea na shughuli zetu za kila siku katika ujenzi wa taifa katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni sote kwa pamoja na kila mtu kwa sehemu yake tunaamini tutafikia malengo yetu kama nchi. Miongoni mwa shughuli kubwa zinazofanyika kwa kuzingatia kalenda ni michezo yote kwa jumla yake. Kwa mantiki hiyo, soka ni kati ya michezo inayojumuishwa kwenye kalenda ya TFF kwa mujibu wa shughuli mbalimbali za shirikisho kwa mwaka mzima.

Wakati wadau mbali mbali wa kandanda wakiwa wanaendelea kujadili matokeo ya michezo inayopigwa ya ligi katika viwanja tofauti tofauti, muda nao unaonekana siyo rafiki tena kwani ni kama vile msimu wa 2018/19 unaelekea kufika katikati, ambapo timu nyingi zina wastani wa michezo zaidi ya kumi sawa na nusu ya michezo yote inayotakiwa kupigwa na kila timu kabla ya kufika tamati ya mzunguko wa kwanza. Hii inatokana na ongezeko la timu msimu huu kutoka kumi na sita hadi ishirini, maana yake ni kuongezeka kwa idadi ya mechi kutoka thelathini za msimu wa 2017/18 hadi thelathini na nane msimu huu.

Kwa kuzingatia hali halisi ya mambo yalivyo katika uendeshaji na usimamizi wa ligi kuu msimu huu, klabu zote za ligi kuu zinastahili pongezi kwa jinsi kila timu ilivyojipanga kushiriki na kutafuta nafasi ya kupata ubingwa ama nafasi za juu mwishoni mwa ligi ifikapo May mwakani licha ya changamoto nyingi mbali mbali mabazo zimeanza kujitokeza katika hatua hii ya mwanzoni. Tunafahamu siyo kazi nyepesi na rahisi kucheza ligi kuu kwa kuwa kila timu inatamani kufanya vizuri lakini haiwezekani kwa sababu kanuni ya kushindana haiko hivyo ni lazima awepo wa kushinda na kushindwa.

Wakati msimu mpya ulipoanza mwezi wa nane, kila mmoja alikuwa na hamu ya kujua nini kitatokea, ni timu gani itakuwa na nguvu zaidi kuliko nyingine, mabenchi ya ufundi yatakuwa na mchngo gani katika kuziwezesha timu kuhimili kishindo na mikimikiki ya ligi kuu, aina ya wachezaji waliosajiliwa, pia ubora na uwezo wa timu kucheza soka la kuvutia, viwango vya wachezaji wa kigeni kwa baadhi ya timu zilizowapa kandarasi, viwango vya waamuzi, mifumo itakayotumika, ratiba na mambo mengine mengi yanayouzunguka mpira wa ushindani.

Kimsingi baada ya ligi kuanza pole pole kadiri muda unavyozidi kusogea mbele picha na majawabu ya kila ambacho wadau walitamani au walitarajia kionekane/ kitokee kimeanza kujibiwa na kuonekana, mathalani uwezo wa wachezaji mmoja mmoja, timu na mabenchi ya ufundi yanavyowajibika na kuviongoza vikosi. Siyo hivyo tu lakini pia ugumu na uwepesi wa ligi kwa ujumla. Kwa kuangalia kalenda na idadi ya mechi zilizosalia katika ligi ni rahisi sana kusema ligi bado kama jinsi ambavyo wengi wanavyoamini lakini kiufundi na kwa namna hali ilivyo, mwenendo wa ligi katika mzunguko wa kumi/kumi na moja umeanza kuonesha dalili za matabaka.

Mara nyingi ligi ya Tanzania ina kawaida ya kuanza kwa nguvu kubwa kila timu ikionesha kucheza kwa malengo ya kuutaka ubingwa, na hata zile timu zinazosadikika kuwa ni kubwa zina kawaida ya kupata matokeo ushindi kwa taabu sana, lakini pia kuna timu ambazo zimezoeleka kuanza kwa kasi ya ajabu zikiwa zinapata ushindi mfululizo lakini taratibu huwa zinaanza kurudi chini mfano Mtibwa, Mbao n.k, wakati huo huo timu zinazopanda ligi kuu kutoka ligi daraja la kwanza,

ukichukulia wastani wa asilimia thelathini na saba hadi arobaini na saba ya timu hizo huwa zina kawaida ya kuanza kwa kushindwa kuhimili vishindo na wakati mwingine kujikuta zikitermka daraja msimu huo huo, kama tulivyoshuhudia timu ya Njombe mji msimu wa 2017/18.

Mazingira yaliyopo sasa ligi ikiwa imefika mzungunguko wa kumi na moja kwa timu zote kasoro Yanga peke yake, msimamo wa ligi kwa kuangalia takwimu zilivyo unaweza kujiuliza maswali ambayo huenda yakakupatia matumaini ya kubadilisha sura na mwelekeo wa hiki tunachokizungumza kwa sasa, lakini nadhani uwezekano huo utakuwa ni mdogo mno.

Kwa mujibu wa mtindo wa ligi yetu muda siyo mrefu kuanzia sasa ligi itasimama kwa muda ili kutoa nafasi kwa wachezaji kupumzika na kuruhusu zoezi la usajili wa dirisha dogo kwa kila timu itakayohitaji kufanya hivyo.

Hii ni fursa pekee kwa walimu kufanya maboresho ya vikosi vyao ili kuzifanya timu kuendelea kuwa na nguvu ya kucheza mzunguko wa mwisho kwa kiwango kinachostahili.Kuna ukweli usiopingika kwamba timu zinafaidika na usajili wa dirisha dogo, lakini pia wakati mwingine baadhi ya timu hazipati faida ya fursa hii, hii inaweza kusababishwa na mbinu, mipango na maandalizi mazuri ya timu husika yaliyowekwa kabla ya kufungua dirisha la zoezi zima.

Wakati mwingine maandalizi na mipango inaweza kuwa mizuri lakini timu ikakwama kutimiza malengo yake kutokana na kukosekana kwa fedha ya kutosha.Na hapo ndipo tofauti ya vilabu vyetu inapoanzia.Tunaona ukubwa wa vikosi, aina ya wachezaji na mabenchi ya ufundi, maandalizi ya yanayofanyika kabla ya msimu kuanza (pre – season), miundo mbinu na kadhalika.Katika uhalisia mwisho wa siku nguvu kubwa ya uchumi wa timu inayotumika katika yote hapo juundiyo hiyo hiyo inaamua uwezo wa timu katika utendaji kiwanjani na hatimaye tunaouona mgawanyiko wa kimatabaka wa vilabu vyetu wakati wa ligi.

Leo hii katika mzunguko wa kumi na moja timu ina alama saba (7) mathalani, ikiwa imefungwa mabao kuanzia kumi na tano (15 na kuendelea), imefunga mabao saba au nane (7-8 ), na timu nyingine ina alama ishirini na tano au zaidi, imefunga mabao kumi na tano (15) na imefungwa matatu/ manne ( 3-4) unatarajia nini? Kwamba hawa waliotangulia kitasibu kitu gani ili wabaki pale pale hadi aliyeko chini apande na hatimaye awazidi?

Katika soka kuna misemo na nadharia nyingi sana, lakini ipo nadharia ambayo haikukaa kisayansi kuweza kujibu hoja za kitaalamu na hesabu katika soka, wengi wanatamka na kuamini kwamba, kwa vile mpira umetengenezwa kudunda basi yeyote anaweza kushinda. Ni kweli kila timu ina nafasi sawa ya kushinda mbele ya mpinzani wake lakini hoja ya msingi ni kwamba je? timu imejiandaa kushinda? Ndiyo maana tunaona ligi nyingi duniani zipo timu ambazo zimejidhatiti kupata ushindi mara kwa mara kutokana na mipango yake hususani uwekezaji mkubwa unaosaidia timu kupata mahitaji muhimu yanoyofanana na ukubwa wa ligi katika mazingira husika.

Timu zetu zote za Ligi Kuu zinatakiwa kuangalia vizuri nafasi zake kwa wakati huu ili kuona ni nini cha kufanya kwa ajili ya kujiweka katika nafasi nzuri zaidi.