Zizou ashindwa kujizuia, amwambia Ronaldo ‘uko juu’

Tuesday May 21 2019

 

Wakati msimu ukiendelea, Messi aliweka rekodi nyingine mbili, alikuwa mchezaji wa kwanza wa La Liga kufunga mabao 300 na Aprili 20 akafikisha rekodi ya mabao ya jumla 500, mengi kati ya mabao hayo yakiwa yamefungwa kwa mguu wake wa kushoto (zaidi ya asilimia 80).

Kati ya mabao hayo 25 yalitokana na mipira ya adhabu, 64 yalikuwa mabao ya penalti na 411 ni mabao ya kawaida ya ndani ya mchezo. Mabao 450 aliifungia Barca na mengine aliifungia Timu ya Taifa ya Argentina.

Mafanikio mengine binafsi aliyapata katika Uwanja wa Riazor wakati wa mechi dhidi ya Deportivo la Coruna, mechi iliyomalizika kwa ushindi wa mabao 8-0.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo kwa Messi, wiki chache za mwisho wa msimu zilikuwa ngumu zaidi kuliko ilivyotarajiwa, Barca ilitolewa na Atletico Madrid katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku mahasimu wao Real Madrid wakiwa katika mwelekeo mzuri wa kutwaa taji la La Liga.

“Tulikuwa na faida lakini baadaye tulijikwaa, ni hatua ambayo hatukuitarajia, mara tu baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa Real wakaanza kukabiliana nasi, Atletico wakatutoa katika ligi ya mabingwa, pia kuna mechi za La Liga ambazo tulipoteza pointi nyingi lakini jambo zuri ni kwamba bado tunajiamini,’’ alisema Messi katika kilichoaminika kuwa ni kuwatuliza mashabiki wa Barca.

Kimsingi Real na Atletico si tu kwamba walitakiwa kushinda, bali pia walitakiwa kuomba Barca iteleze lakini Barca haikuyumba kwa sana, na Mei 14, 2016 waliichapa Granada mabao 3-0 katika mechi yao ya mwisho.

Advertisement

Messi akafanikiwa kwa kushinda taji lake la nane la La Liga katika msimu wa 11, wiki moja baadaye walibeba Kombe la Mfalme baada ya kuichapa Sevilla mabao 2-0.

Vipi kuhusu taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya? Safari hii lilikuwa mali ya Cristiano Ronaldo ambaye msimu huo ataukumbuka kuwa ndio msimu uliomwezesha kubeba taji la tatu la Ulaya.

“Nilikuwa na mtazamo wangu, nilijua ningefunga bao la ushindi na hilo nilimwambia Zizou (Zinedine Zidane ambaye ni kocha wake), niache hadi mwisho katika mikwaju ya penalti kwa sababu nitafunga penalti ya ushindi.” Na hivyo ndivyo hasa ilivyokuwa.”

Ronaldo au CR7 alikuwa kiwango cha juu, hakukuwa na cha kuonea aibu, Ronaldo alizungumzia kilichotokea katika mechi ya fainali dhidi ya Atletico Madrid iliyopigwa mjini Milan, Mei 28, 2016.

Ni ushindi ulioamuliwa kwa mikwaju ya penalti na penalti ya mwisho iliyopigwa na Ronaldo ilikuwa na maana kubwa katika ushindi huo hadi kubeba taji hilo la Ligi ya Mabingwa.

“Wewe uko katika kiwango cha juu,’’ Zidane alisikika akimwambia wakati wa kufurahia ushindi huo. Huo ni ukweli walau unapozungumzia mabao aliyoyafunga katika mashindano hayo. Ronaldo alikuwa ndiye mfungaji bora na mabao yake 16 karibu zaidi ya nusu ya aliyofunga straika wa Bayern Munich, Robert Lewandowski aliyeshika nafasi ya pili.

Kwa Barca, Suarez aliibuka mfungaji bora na kutwaa kiatu cha dhahabu katika La Liga na hivyo kuibeba tuzo ambayo msimu uliopita ilichukuliwa na Ronaldo lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuna aliyemsogelea Ronaldo.

Itaendelea Jumamosi ijayo…