Yanga ilivyovunja rekodi ya Mbao FC Kirumba

Muktasari:

  • Timu ya Yanga Sc iliyopo chini ya mkongo Mwinyi Zahera ilifanikiwa kuvunja kasumba ya muda mrefu baada ya kuifunga Mbao FC mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

KAMA juzi Jumatano ingekuwa mara yako ya kwanza kutua Bongo, basi ungedhani Yanga ndio imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa jinsi ilivyosherehekea kuifunga Mbao FC mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Kwa mara ya kwanza tangu Mbao FC ipande Ligi Kuu ukiwa ni msimu wa tatu sasa, Yanga haikuwahi kupata ushindi kwenye uwanja huo ilipocheza wapinzani wao hao na hata mechi hiyo Mbao ndiyo iliyotangulia kutikisa nyavu za Yanga.

Ushindi huo umeweka rekodi kwa Yanga kama ilivyokuwa upande wa Simba ilivyokuwa ikisumbuka kuifunga Mbeya City misimu mitatu ya mwanzo ilipokuwa ikicheza Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mechi tatu ilizocheza Uwanja wa Kirumba, Yanga ilipoteza zote na sasa imefuta rasmi uteja kwa Waranda Mbao hao.

Katika dakika 90 za mchezo huo uliokuwa na upinzani mkali Mwanaspoti lilishuhudia mambo mbalimbali.

YANGA ILIVYOINGIA

Iko hivi, mabasi yanayobeba wachezaji mara nyingi huingia uwanjani na kwenda moja kwa moja kwenye mlango wa kuingilia vyumbani lakini juzi Yanga iliingia kwa staili mpya.

Basi lililowabeba wachezaji hao liliwasili na kwenda moja kwa moja kwenye mstari wa uwanja kisha kusimama hapo na wachezaji kuanza kushuka mmoja baada ya mwingine.

Hata hivyo, wachezaji hao walipita katikati ya mstari ambao utenganisha timu moja na nyingine na kwenda vyumbani huku mashabiki wake wakiwashangilia.

SHABIKI ATINGA NA PUNDA

Hii ni mara ya kwanza kwenye soka nchini shabiki maarufu wa Mbao FC, Samuel Kitundu ‘Mbeba Chungu’ kuingia uwanjani akiwa amepanda kwenye mnyama aina ya punda.

Shabiki huyo mwenye mbwembwe nyingi aliingia uwanjani muda mfupi kabla ya mpira kuanza akiwa na wapambe wake huku akiwa amepanda juu ya punda huyo.

Kama kawaida yake, chungu chake kilikuwa kichwani mwake na baada ya kichapo hicho alitoweka ghafla uwanjani hapo.

YANGA YALINDWA NA MAKOMANDOO

Makomandoo wa Yanga walifanya kazi kubwa kwani tangu timu hiyo ilipowasili jijini hapa walikuwa na kazi kuhakikisha hakuna hujuma itakayofanyiwa timu yao.

Kuanzia mazoezini, makomandoo hao waliimarisha ulinzi mkali huku juzi uwanjani hapo walifika mapema kuhakikisha hakuna jambo baya na walionekana wakipambana vikali.

ZAHERA AVAMIWA KIRUMBA

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amekuwa kocha wa kwanza wa kikosi hicho kuifunga Mbao FC jijini hapa na mashabiki wa timu yake walikuwa wakipata tabu na rekodi hiyo mbovu. Mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo mashabiki wa Yanga bila kuogopa polisi walivamia uwanja na kwenda moja kwa moja kumkumbatia kocha wao.

Hata hivyo, polisi waliwatawanya mashabiki hao ambao walionyesha kutojali lolote kutokana na furaha kubwa waliyokuwa nayo.

SHABIKI SIMBA AJICHANGANYA

Shabiki huyo alikaa jukwaa ambalo lilitawaliwa na mashabiki wa Yanga, akiwa amevaa jezi nyekundu na kukutana na kichapo kikali.

Lakini alipopata upenyo aliponyoka mikononi mwa mashabiki hao na kutoka nduki akiwakimbilia polisi ili wamwokoe na kichapo.

MAKAMBO AWEKA REKODI

Mshambuliaji Heritier Makambo ndiye mchezaji wa kwanza wa Yanga kuifunga Mbao FC Uwanja wa Kirumba.

Makambo alifunga bao la kusawazisha dakika ya 50 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Papy Tshishimbi huku bao la pili likifungwa kwa mkwaju wa penalti na Amissi Tambwe.

WAAMUZI WAKIONA CHA MOTO

Baada ya mwamuzi, Ally Simba kupuliza kipyenga cha kuashiria mapumziko alitoka yeye na wasaidizi wake kwenda kwenye vyumba vya kupumzikia.

Lakini wakati wanakwenda ghafla walianza kushambuliwa kwa kurushiwa chupa za maji na mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga walioonyesha kukasirishwa na maamuzi ya mwamuzi huyo kwamba alikuwa akiwapendelea wapinzani wao.

Hata hivyo, ilibidi waamuzi hao kukimbia na kurudi uwanjani na polisi waliwatawanya mashabiki wao waliokuwa wamekaa katika jukwaa la mzunguko la uwanja huo.