Yanga hii ya Zahera, ni mpyaaa!

Friday August 10 2018Mwinyi Zahera.

Mwinyi Zahera. 

By KHATIMU NAHEKA

KAMA ni gari, basi liko gereji. Yanga inendelea kusukwa pale Mji Kasoro Bahari, Morogoro mwanzoni kabisa mwa Milima ya Uluguru ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera na msaidizi wake, Noel Mwandila.

Zahera raia wa DR Congo anaonekana kudhamiria kubadilisha mambo katika kikosi chake na mpaka sasa tayari sura kamili ya Yanga anayoitaka imeanza kuonekana, angalia aliyoyabadilisha.

VIUNGO USIPIME

Kitu kikubwa ambacho kitaipa nguvu Yanga na kugeuka shubiri kwa wapinzani wao ndani ya msimu ujao ni uwepo wa viungo wa kazi katika kikosi hicho.

Kwanza Yanga imemrudisha kiungo wake, Deus Kaseke. Jamaa sio mvivu uwanjani. Anakaba, anakimbiza na kufunga. Kwa kifupi, yuko tayari hasa baada ya mazoezi makali wanayopokea kutoka kwa Kocha Zahera.

Kiungo mwingine ni ingizo lingine, Feisal Salum, fundi mmoja kutoka Zanzibar.

Zahera amemwongezea kitu na sasa amekuwa fundi haswa. Amekuwa na uwezo mkubwa wa kukaba na zaidi, ni hatari kwa kupiga pasi zilizokwenda shule.

Kuna Jafary Mohamed na Mohamed Issa, huyu bado hajaanza kazi na kama akicheza sambamba na Pappy Kabamba Tshishimbi na Raphael Daudi, wapinzani wataomba po.

PUMZI, STAMINA DEBE ZIMA

Hakika hapa Kocha Zahera amefanikiwa. Ameweza kuitengeneza Yanga isiyochoka ndani ya muda mchache.

Wakati wote wao ni mchakamchaka wakionyesha uwepo wa pumzi kutokana na dozi ya mara mbili kwa siku ya mazoezi. Kwenye mazoezi yao, sio rahisi umwone mchezaji anatembea zaidi ya sekunde saba.

KUTEMBEA MARUFUKU

Mazoezini ni marufuku kutembea na kwa hilo, Kocha Zahera hataki masikhara. Hii sio mazoezini tu, hata kwenye mechi hataki kuona mchezaji anatembea wakati timu imepoteza mpira. Mrisho Ngassa tayari ameshakumbana na wakati mgumu na amekuwa akikaribiwa kila anapotembea. Kwa kifupi kocha huyo haangalii sura, zoezi la ukabaji litakuwa kwa wote.

LANGONI HAINA KUREMBA

Kama kuna eneo ambalo ukifanya vizuri Kocha Zahera anakusifia, ni hili. Hapendi watu wanaopaka rangi mipira wafikapo golini mwa timu pinzani.

Anapenda wachezaji wanapofika langoni kwa wapinzani wajaribu kupiga mashuti makali. Hata hivyo, hilo limekuwa somo tosha hasa kwa washambuliaji na viungo wake kwani wamekuwa wakijaribu hayo na wanaweza.

FIRST 11 MTIHANI

Wewe unaweza ukaiona Yanga kisha ukapanga kikosi chako. Kocha Zahera pia anaweza kupanga wake tofauti na wako. Hii ni kutokana na ubora wa wachezaji walioko kwenye kikosi hicho tofauti na msimu uliopita na hivyo kushindwa kujua apangwe nani na nani aachwe. Pengine ni sehemu mbili pekee unaweza kutabiri atacheza nani na ikawa hivyo. Beki wakulia na mshambuliaji wa kati.

ZAHERA KISWAHILI IMO

Kocha Zahera ni Mkongomani anayeishi Ufaransa. Hata hivyo, kama ulikuwa hujui, anafahamu Lugha ya Kiswahili na ndiyo amekuwa akiitumia mazoezini na hata nje ya uwanja kuwaelekeza wachezaji wake.

Utasikia tu Mupe (mpe) mwenzako, ukipata mpira angalia fasi (nafasi) ya mwenzako na mambo kama hayo.

INAWAKOSA WAWILI TU

Kuna watu wawili tu, Zahera akiwapata amemaliza kazi. Beki wa kulia na mshambuliaji wa kati.

Beki wa kulia anayetafutwa ni wa kusaidiana na Juma Abdul baada ya Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kuondoka. Pia mshambuliaji wa kati atakayesaidiana na Heritier Makambo wakati huu mkongwe Amissi Tambwe akirudisha makali yake.

NINI KIFANYIKE?

Kama ni kikosi, tayari kipo tayari kwa mapambano. Jambo pekee lililobaki uongozi wa Yanga kulifanyia kazi ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa sawa kisaikolojia ili waweze kujituma. Hii ni pamoja na haki zao kushughulikiwa kwa wakati na hapo ni wazi Yanga itakuwa na ushindani mkubwa msimu ujao.