Wangekuwa Azam, Liverpool wangemfukuza Klopp

Muktasari:

  • Pointi 97 ambazo vijana wa Jurgen Klopp walimaliza nazo, zingeweza kuwafanya wawe mabingwa katika misimu 25 iliyotangulia, kasoro misimu miwili tu, ile ambayo Mkatalunya Pep alikuwa bingwa; 2017/18 ambao alivuna Pointi 100 na huu wa 2018/19 ambao amevuna pointi 98.

MSIMU wa 27 wa Ligi Kuu ya England (EPL), ulifikia tamati Jumapili iliyopita kwa kila mtu kuvuna alichopanda.

Huu ulikuwa msimu wa maajabu, kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo, timu imemaliza ligi ikiwa na zaidi ya pointi 90, lakini imekosa ubingwa.

Hapo nawazungumzia vijana wa Jurgen-pressing (gegenpressing) Liverpool ambao msimu huu walijipanga kuwa mabingwa na walistahili kabisa, kama sio Pep Guardiola na wananchi wake wa Manchester City kuharibu mipango.

Pointi 97 ambazo vijana wa Jurgen Klopp walimaliza nazo, zingeweza kuwafanya wawe mabingwa katika misimu 25 iliyotangulia, kasoro misimu miwili tu, ile ambayo Mkatalunya Pep alikuwa bingwa; 2017/18 ambao alivuna Pointi 100 na huu wa 2018/19 ambao amevuna pointi 98.

Hii ina maana kwamba Sir Alex Ferguson asingeweza kuchukua ubingwa hata mara moja mbele yao, kwani mara 13 ambazo ‘babu’ alizochukua ubingwa, ni mara moja pekee (2008/09) ndio aliifikisha pointi 90, hizo nyingine zote alishinda na pointi pungufu ya 90, zikiwemo 75 za msimu wa 1999/00.

Hali kama hii ilikuwa ilitokee Tanzania msimu wa 2015/16. Msimu huo, Yanga ya Babu Hans na Azam FC ya Stewart Hall, zilifukuzana mbio zisizo za kawaida kwenye historia ya ligi yetu.

Hadi zinakutana kwenye raundi ya 7, Oktoba 17, 2015 katika sare ya 1-1, zilikuwa zimeshinda mechi zao zote 6 zilizotangulia.

Mwisho wa msimu, Yanga wakawa mabingwa kwa pointi 73 huku wakipoteza mchezo mmoja pekee, dhidi ya Coastal Union.

Azam wakashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 64, wakipoteza michezo miwili; mmoja uwanjani dhidi ya Coastal Union na mwingine mezani dhidi ya Mbeya City.

Pointi 64 za Azam zingeweza kuwafanya wawe mabingwa katika misimu yote iliyotangulia, kasoro mmoja tu wa 2006 ambao Yanga walivuna pointi 70.

Hata ule msimu ambao Azam wenyewe walikuwa mabingwa, hawakuweza kufikisha pointi 64, waliishia 62 tu.

Na baada ya msimu ule, hawakuwahi tena kuzifikia pointi zile hadi msimu huu, ambao una timu 20, ikiwa na maana kwamba mechi zimekuwa nyingi zaidi.

Kwa hiyo Azam ingeweza kuwa bingwa msimu ule, kama sio babu Hans na vijana wake wa Jangwani kuwa katika ubora usio wa kawaida.

Lakini cha kushangaza, mwisho wa msimu, Azam wakamfukuza Kocha wao, Stewart Hall. Badala ya kumuacha aendelee kuanzia pale alipoishia, wakamfukuza ili waanze upya. Matokeo yake, kila siku wanakuja na porojo mpya.

Unaweza ukajiuliza lile swali ambalo mmiliki wa Liverpool, John W. Henry, alijiuliza kuhusu Arsenal wakati wa sakata la usajili wa Luis Suarez, “Hivi pale Chamazi huwa wanavuta nini?”

Unaanzaje kumfukuza kocha kama huyu ambaye timu yake ilipata matokeo bora kitakwimu kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia yenu? Ina maana huwa

hawafanyi tathmini ya kiufundi kufikia maamuzi yao?

Matokeo yake, hadi leo Azam haijawahi kuwemo kwenye mbio za ubingwa, tangu wafanye kosa lile.

Kila msimu hujikuta wakiwa nje ya mbio za ubingwa inapofikia Machi na kuwaacha wazee wa Kariakoo wakiliendeleza libeneke.

Mafanikio ya kwenye mpira yanahitaji vitu viwili vikubwa, uimara (stability) klabuni na uwekezaji sahihi kwenye timu.

Kwa misimu kadhaa sasa, Azam imekosa vyote viwili. Imekosa uimara klabuni na imekosa uwekezaji sahihi kwenye timu.

UIMARA KLABUNI

Ebu dhania, klabu iliyo ‘serious’ na ubingwa, inaanzaje kuruhusu wachezaji wake watano Bora wanaopata nafasi ya kwanza kwenye timu ya taifa, kuondoka bure?

Ebu dhania, klabu ambayo katika kipindi cha miaka mitano, imekuwa na watendaji wakuu watatu?!

Ebu dhania, klabu ambayo katika kipindi cha miaka mitano imekuwa na makocha 8?!

Klabu kama hii haina sifa nyingine zaidi ya ulegevu (instability) kwenye safu ya uongozi, yaani kukosa uimara (stability).

Katika mazingira kama haya, huwezi kuwa kuwania ubingwa katika nchi ambayo mifumo yote imetengenezwa kuwapendelea Simba na Yanga.

UWEKEZAJI SAHIHI

Ebu dhania usajili walioufanya kuziba nafasi za wachezaji waliondoka. Kuanzia wale watano waliokimbilia Kariakoo hadi wale walioenda nje ya nchi.

Anaondoka John Bocco, nafasi yake inachukuliwa na Ditram Nchimbi. Mnagundua mmekosea, mnamleta Danny Lyanga. Halafu mnataka kushindania ubingwa na Simba yenye Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere.

Anaondoka mgonganaji Himid Mao halafu mnamleta Stephan Kingue Mpondo. Kiungo mgumu asiyejua kulenga lango. Anamaliza mchezo kwa majaribio matano langoni, halengi lango hata mara moja.

TANZANIA NCHI NGUMU

Ili uwe bingwa wa Tanzania, lazima uwe imara mara mbili au tatu zaidi, kulinganisha na Simba na Yanga. Achilia mbali kuwa sawa nao, hata ukiwazidi mara moja na nusu, huwezi kuwa bingwa.

Yanga na Simba zipo serikalini, bungeni, TFF, kwa waamuzi na kwingine kote. Hawa wote ni binadamu...hawawezi kukubali kila mwaka waumizwe roho na wewe...watakuhujumu tu!

Ebu Azam ijiulize ilipotezaje pointi dhidi ya Mbeya City kwa kadi tatu za Erasto Nyoni, ambaye hakukatiwa rufaa, huku Simba ikinusurika kwa kadi ya Novalty Lufunga dhidi ya Polisi kwenye Kombe la Shirikisho ilihali ilikatiwa rufaa?

Au ijiulize kwanini mchezo wao dhidi ya Mtibwa mwaka 2012 uliamriwa na Kamati ya Karia, urudiwe katika uwanja wa Uhuru wakati Mtibwa ndio walisusa na kutoka uwanjani?

Ule msimu ninyi mlikuwa mnafukuzana na Simba kwenye ubingwa. Mngeshinda ile mechi, mngewatia presha sana kwa sababu ungebaki mchezo mmoja na wao walikuwa wanamaliza na Yanga. Nani anajua matokeo ya mechi hii? Kwa hiyo walihakikisha mnadhibitiwa mapema

Kwa hali kama hiyo mtapenyea wapi?

Ni kwamba, Yanga na Simba huandaliwa mazingira ya kuwaletea raha wakuu kwenye mamlaka mbalimbali. Wewe mwenzangu na mimi ukitaka kuvunja utawala wa hawa

mapacha, unakuwa unawakera wakuu...ni lazima wakushughulikie.

Kwa hiyo, inabidi uwe imara mara mbili au tatu zaidi mbele yao...hapo ndipo unaweza kufidia ombwe la upendeleo.

La sivyo, unaweza kuwa bingwa mbele yao mara moja tu, halafu wakakushughulikia na ukapotea kabisa.

Wako wapi Cosmopolitan, wako wapi Mseto, wako wapi Pan Africans, wako wapi Tukuyu Stars, wako wapi Coastal Union, wako wapi Pamba, wako wapi African Sports, wako wapi Mtibwa Sugar...mko wapi nyinyi wenyewe?

Ukichukua ubingwa mbele ya hawa jamaa halafu ukawa dhaifu kiuongozi, watakushughulikia na kukupoteza. Utabaki kwenye makaratasi tu, lakini kwenye ubingwa haupo.

Matokeo yake, mnawafukuza makocha wanaowaletea mafanikio na kujikuta mkihaha kuishi kwa kuunga unga.

Liverpool wanajua wanachokifanya, hawawezi kumfukuza Klopp, lakini wangekuwa Azam FC, wangemfukuza kwa kukosa ubingwa!