Wachana nyavu wa mwaka 2018

Tuesday January 1 2019

 

LONDON, ENGLAND. HUU ni Mwaka Mpya 2019. Mwaka uliokwisha wa 2018 umeshuhudia mengi kwenye soka ikiwamo mchakamchaka wa mastaa katika kufunga mabao ili kuwania tuzo za ufungaji bora.

Baada ya kuingia mwaka mpya wa 2019 hii hapa ndio orodha ya masupastaa matata kabisa kwenye soka waliofunga mabao mengi kwa mwaka 2018 katika mechi za klabu na timu zao za taifa kwa ujumla wake.

5.Harry Kane - mabao 42

Harry Kane anatajwa kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora kabisa duniani kwa sasa na hakika kwa mwaka 2018 alikuwa kiwango bora kabisa kwa klabu yake ya Tottenham Hotspur na Timu ya Taifa ya England.

Kane alishinda Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizofanyika huko Russia ambapo aliisaidia England kufika nusu fainali. Kwa mwaka 2018, Kane alifunga mabao 42 katika mechi 63.

4.Mohamed Salah - mabao 44

Mohamed Salah amekuwa na mwaka mzuri wa 2018 tangu alipojiunga na Liverpool 2017. Kiwango chake cha soka kwa mwaka uliopita, staa huyo wa Anfield alifunga mabao 44 katika mechi 55 alizochezea klabu yake na Timu ya Taifa ya Misri.

Soka maridadi alilokuwa akicheza Mo Salah lilimfanya watu waanza kumweka kwenye paa moja na wakali kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

3.Robert Lewandowski - mabao 46

Supastaa wa Poland na Bayern Munich, Robert Lewandowski hakika anafunikwa tu na uwepo wa wakali kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, lakini fowadi huyo amekuwa bora kabisa kwa mwaka 2018.

Kwa mwaka wote wa 2018, Lewandowski alicheza mechi 56 na kufunga mabao 46, ikiwa ni rekodi tamu kabisa kwenye maisha yake ya kisoka.

Hakika staa huyo anatarajia kuendelea kutamba mwaka huu 2019.

2. Cristiano Ronaldo - mabao 49

Cristiano Ronaldo aliushangaza ulimwengu wa wapenda soka baada ya kuchukua uamuzi wa kuihama Real Madrid alikodumu kwa miaka tisa na kwenda kujiunga na Juventus kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2018.

Uhamisho wake haukuonekana kumgharimu chochote kwa sababu huko Italia amekuwa na kiwango bora kabisa na kuendelea kupiga mabao. Mwaka 2018, Ronaldo amefunga mabao 49 katika mechi 53.

1.Lionel Messi - mabao 51

Lionel Messi ameonyesha kiwango bora kabisa mwaka 2018 akifunga mabao 51 katika mechi 54 alizochezea klabu yake ya Barcelona na Timu ya Taifa ya Argentina. Lakini, ilishangaza wengi kumwona mchezaji huyo akishika namba tano kwenye Ballon d’Or.

Supastaa, Messi amekuwa hachuji kwenye suala la kutupia kwenye nyavu za wapinzani na amekuwa bora ndani ya uwanja hasa Barcelona inapohitaji huduma yake kufanya vyema kwenye michuano mbalimbali.