Vita ilikuwa pale kwa viungo

Monday February 18 2019

 

By KHATIMU NAHEKA

SIMBA imeshinda juzi Jumamosi kwa bao 1-0, shukrani kwa mshambuliaji wake Meddie Kagere akimalizia kwa kichwa kazi ya nahodha wake John Bocco.

Wakati mashabiki wengi wa Simba wakimsifu Kagere kwa bao hilo lakini asikwambie mtu kulikuwa na vita kubwa katika safu ya kiungo kwa timu zote mbili na Simba hapo ndipo walipotengeneza ushindi wao.

Simba ilikuwa na viungo watatu halisi wawili wa kukaba, Jonas Mkude na James Kotei lakini Chama akiwa mchezeshaji huku Emmanuel Okwi akichagiza katika eneo hilo.

Kule Yanga nako alikuwa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ juu yake akiwa Feisal Salum, Pappy Kabamba Tshishimbi na nahodha wao Ibrahim Ajib.

MKUDE ALITISHA- PASI 48

Jonas Mkude ndiyo kiungo aliyepiga pasi nyingi kwa timu zote akipiga jumla ya pasi 42 mpaka mchezo huo unamalizika ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika alikuwa tayari amepiga jumla ya pasi 30 na katika hizo 26 zikifika sehemu husika huku akipoteza nne.

Kipindi cha pili Mkude akapiga jumla ya pasi 18 katika hizo 16 zikifika kwa walengwa huku mbili zikipotea na mchezo mzima alipokonya mipira mara mbili.

JAMAES KOTEI- PASI 46

Ukiacha Mkude nyuma yake kulikuwa na mtu anaitwa Kotei ambaye mpaka anamaliza dakika 45 za kwanza alikuwa ameshapiga jumla ya pasi 32 katika hizo 25 zili fika kwa muhusika, saba zikipotea, na za kupokonywa mara mbili. Kipindi cha pili raia huyo wa Ghana akafanikiwa kupiga pasi 14 ambapo 12 zilifika, mbili zikapotea lakini akafunika katika kupokonya mipira ya wapinzani na kuharibu mashambilizi ya Yanga mara tatu.

CLATOUS CHAMA

- PASI 33

Mwamba wa Lusaka kama wanavyomuita Chama hakuwa katika ubora wake shughuli yake ilikuwa ni ya dakika 45 kisha akatolewa na mpaka anamaliza mechi yake hiyo alikuwa amepiga jumla ya pasi 33 ambapo 26 zilifika na saba zikipotea.

EMMANUEL OKWI- PASI 24

Okwi aliyedumu uwanjani dakika za 80 alifanikiwa kupiga jumla ya pasi 16 mpaka anamaliza dakika 45 za kwanza katika hizo 12 zikifika na akipotena nne huku kipindi cha pili akipiga pasi nane, sita zikifika na kupoteza mbili.

HASAN DILUGA- PASI 18

Wakati Chama akitoka nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Dilunga ambaye aliingia dakika 45 za pili na kufanikiwa kupiga jumla ya pasi 18 katika hizo 16 zikifika na mbili zikapotea.

MZAMIRU YASIN

- PASI 7

Okwi alitolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Mzamiru Yasin ambaye alifanikiwa kupiga jumla ya pasi saba, sita zikifika na moja ikapotea.

FEISAL

- PASI 40

Kule Yanga mbabe wao alikuwa ni fundi Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye mpaka anamaliza dakika 45 za kwanza alikuwa amepiga jumla ya 19 katika hizo 16 zikifika na akipoteza tatu akipokonya mpira mara tatu.

Kipindi cha pili kiungo huyo alipiga jumla ya pasi 21 ambapo katika idadi hizo zilizofika zilikuwa 19 akipoteza pasi mbili akipokonya mpira mara moja.

TSHISHIMBI- PASI 37

Mkongomani Tshishimbi alipomaliza dakika 45 za kwanza alikuwa amepiga jumla ya pasi 19 akifikisha kwa walengwa pasi 16 akipoteza tatu na katika kipindi cha pili alipiga pasi 18 na zilizofika zikawa 14, kupoteza na kupokonya nne.

AJIB- PASI 30

Nahodha wa Yanga Ajib alimaliza kipindi cha kwanza akiwa amepiga pasi 17 akifikisha pasi 12 na kupoteza tano na kipindi cha pili mpaka anatolewa dakika ya 61 alikuwa amepiga pasi 13 akifikisha tisa na kupoteza nne.

NINJA- PASI 13

Ninja alikuwa katika safu ya kiungo akicheza karibu sana na safu ya ulinzi alimaliza dakika 45 za kwanza akiwa amepiga pasi saba akiwa hajapoteza hata moja lakini pia akipokonya mpira mara tatu. Kipindi cha pili beki huyo wa kazi alipiga pasi sita, tano zikifika na moja ikapotea huku akipokonya mpira mara tano na kumfanya mchezaji aliyepokonya mipira mara nyingi.

BANKA- PASI 11

Kiungo Mohamed Issa ‘Banka’aliyeingia uwanjani dakika ya 61 alifanikiwa kupiga jumla ya pasi 11 uwanjani akipoteza mbili.

JUMLA YAO

Mchezo mzima viungo hao wa Simba walipiga jumla ya pasi 176, huku Yanga wao wakipiga pasi 131.