Vigogo wavutana huko kisa Yanga, Simba

WATANI wa jadi, Simba na Yanga wanahesabu saa tu ili kukata mzizi wa fitina msimu huu watakapokutana katika mechi ya mzunguko wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo kongwe nchini zimebamba mashabiki kila kona, si mabondia, wanariadha, viongozi wa Serikali na hata kwenye netiboli, habari ya mjini ni mechi ya Simba na Yanga.

Japo Yanga inatajwa kuwa dhaifu msimu huu mbele ya Simba, lakini mashabiki wake wanakwambia mnyama lazima achinjwe pale kwa Mchina.

Hata hivyo Simba wamejibu mapigo wakiwakebehi Yanga kuwa hata kabla ya mechi wamekwishafungwa kisaikolojia, kwani safari hii kumfunga Yanga kwao ni sawa na kusukuma mlevi, endelea....

Hassan Mwakinyo- Simba

Bondia huyu maarufu nchini hivi sasa anakwambi yeye ni Simba damu na mechi ya kesho licha ya kwamba hatokuwepo nchini, lakini hana presha nayo kabisa.

“Kama tumemfunga Mwarabu, Vyura FC ni nani hadi wasifungwe? Hii mechi wala haina presha kwa Simba ya kimataifa,” alisema Mwakinyo.

Japhet Kaseba- Simba

Bondia bingwa wa Afrika wa ngumi na mateke (kick boxing), Japhet Kaseba anakwambia kwa Simba hii wala umwambii chochote kuhusu kuchukua pointi tatu pale kwa Mchina.

“Hasira zote sasa najua tunahamishia kwa Yanga, zile bao tano walizokuwa wakishabikia za Mwarabu sasa kibao kitageuka,” alisema Kaseba.

Kick boxer huyo alisema atakwenda Taifa kifua mbele tena akiwa amelamba uzi mwekundu kwani Simba anaielewa sana tu na anafahamu haitomuangusha, japo anajua Yanga itajitutumua kucheza, lakini watake wasitake, Yeboyebo lazima wafungwe.

Judith Ilunda- Yanga

Mtendaji huyu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) anakwambia wako tayari kufungwa na timu nyingine yoyote lakini sio Simba, hivyo wasijidanganye Jumamosi kuwa watashinda kwa kuichukulia Yanga poa.

“Kocha Zahera (Mwinyi) ameshawambia mpira sio hesabu, mpira unachezwa uwanjani na bahati nzuri kocha wetu hana mambo ya kubahatisha, kumfunga Mwarabu wala kusiwape jeuri, sababu Al Ahly ya safari hii sio bora kiivyo,” alisema Ilunda ambaye ni katibu mkuu wa Chaneta.

Chief Kiumbe- Simba

Kigogo huyu ambaye jina lake halisi ni Khalfa Kiumbe Moto anakwambia hesabu za haraka haraka Mnyama atachomoza na ushindi usiopungua mabao 2-0.

Chief Kiumbe aliyewahi kuwa bosi wa Judo nchini anakwambia kwa kasi ya Simba, Yeboyebo atapitia wapi Jumamosi?.

“Simba ya sasa! Haiwezi kufungwa na Yanga, never ever, hata wakiroga namna gani, Yeboyebo haituwezi, wasubiri tu muda ufike wakafungwe midomo,” alijinasibu Chief Kiumbe.

Gabriel Geay- Simba

Nyota huyu wa Riadha za mbio ndefu za uwanjani na barabarani nchini naye ni Simba damu na anakwambia katika mechi ambazo hazimpi presha ni hiyo ya Jumamosi, kwani tayari mshindi anaoneka.

“Simba hii ifungwe na Yanga! Mnacheza nyie, wacha wajifariji tu, lakini Jumamosi bora wasiende Taifa kwani zile tano za Misri kibao kitawageukia wao,” alisema Geay.

Anthony Mtaka-Yanga

Bosi huyu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na ‘Rais’ na Mkuu wa mkoa wa Simiyu ambako amekuwa akifanya vizuri ni Yanga damu, na amewahi kueleza kuwa anampango wa kuongoza klabu hiyo mara atakapostaafu majukumu ya serikali miaka ijayo, jamaa wala hana presha na mechi ya Jumamosi.

“Mnyama atachinjwa tu atake asitake,” alisema Mtaka kwa kifupi.

Mrisho Gambo- Yanga

‘Mkuu wa mkoa wa Arusha naye hajivungi linapokuja suala la Simba na Yanga jamaa anakwambia yeye ni shabiki kindaki ndaki wa timu ya wananchi na usijekushangaa Jumamosi ukimkuta ameulamba uzi wa njano na kijani kama ishara ya kuisapoti Young African kama ilivyozoeleka.

“Timu imefungwa mabao 10 jamani mechi mbili! Haya tusubiri tuone hiyo Jumamosi,” alisema Gambo ambaye ni miongoni mwa wakuu wa mikoa vijana wachapa kazi.

Mada Maugo- Simba

Bondia huyu anayejitabiria kuwa ni Mbunge mtarajiwa wa Rorya ni mnazi mkubwa wa Simba na Jumanne iliyopita baada ya Simba kumchapa Mwarabu bao 1-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi alisema, ushindi huo umemuongezea morali ya ‘kumuua’ mpinzani wake, Twaha Kiduku watakapozichapa mwezi ujao mkoani Morogoro.

Kama haitoshi bondia huyo anakwambia kipigo kwa Mwarabu ni salamu tosha kwa Yanga Jumamosi kwani Yanga hamfikii Mwarabu hata robo.

“Huyo Yeboyebo wala hatusumbui, watembeze bakuli halafu wanajifariji eti watatufunga! Wanacheza hao, bora wasije tu Taifa,” alijinasibu Maugo.

Mzunguko wa kwanza katika mchezo uliopingwa Septemba 30 mw aka jana ti mu hi zo zilitoka suluhu zilipokutana.